Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote, kwa kuwa leo ni mara yangu ya kwanza kuchangia, ninawashukuru wananchi wangu kwa kuendelea kuniamini kwa awamu ya tatu, na mimi ninawaambia bado nipo na nitawatumikia na hata wanaonitikisa ninaamini bado hawanisumbui kwa sababu kazi naziweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kuchangia kwenye fedha za 10%. Tunatenga fedha nyingi sana kwenye 10%, lakini ukweli hata tuliposimamisha kutoa mikopo, tulifikiri tutakuja na utaratibu mzuri, lakini ninaona kama tunarudi kule kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao vijana wengi sana wamesoma mambo ya fedha, mambo ya mikopo, mambo ya benki, lakini Serikali bado tunarudi kule kule kutumia Maafisa Maendeleo. Niliwahi kuchangia humu nikasema, Afisa Maendeleo kazi yake ni kwenda kuhamasisha, lakini tunampa jukumu la kwenda kukopesha na kudai madeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaotoka huko vijijini, tunaona mengi. Ukiangalia kwenye vikao tunavyotoa fedha na makusanyo, ni vitu viwili tofauti. Wakusanyaji wetu hawana utaalamu wa kukusanya yale madeni, wanaenda kudai madeni wanarudi na magunia ya mkaa kwenye gari; wanaenda kudai madeni, wanarudi na kuku kwenye gari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninajiuliza, sisi tunaoishi na mikopo, kwa nini tusiajiri kitengo? Kuna Halmashauri hapa zinakopesha mpaka shilingi bilioni saba kwa mwaka, kwa nini tusiwe na vijana hata wanne tu waliosoma hayo mambo? Kwa nini benki zinafanikiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuwa na fedha, tunatoa kweli, lengo ni zuri, lakini hazirudi, na hakuna wa kumlaumu. Ni sawa na kumkabidhi mwalimu asimamie mambo ya engineer. Huyu kazi yake siyo hiyo, na vijana wapo wanatafuta ajira. Kweli tunashindwa kwa makusanyo tuliyonayo! Halmashauri kama za Dar es Salaam, zinatoa shilingi bilioni saba, kitengo cha watu wanne, watano professional.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumeenda kuwalundikia Wakuu wa Wilaya, tunaenda kumpelekea Mtendaji wa Kata eti ndio anafanya assessment ya mkopo. Uliona wapi? Si ninyi wasomi, kila mtu ana kitu alichokisomea? Kwa nini tusitafute watu competent tukawapa wakafanya hiyo kazi? Tunaenda kuchukua hiyo document unapeleka, kwa mfano, Halmashauri moja inaweza kuwa na vikundi 100 labda 120 vinapata mkopo. Haya, wapelekee Kamati ya Ulinzi na Usalama ku-assess hivyo vikundi na kuvitembelea, watafanya kazi gani nyingine kwenye Wilaya ya kujadili mambo ya Wilaya? Si itakuwa ni kazi ya kukagua vikundi peke yake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninashauri sana, ni vizuri tukaunda vikundi. Tunao vijana wengi sana waliosoma na wanafanya vizuri. Tunaona benki zinawatumia na yanaenda mbele kuliko sisi. Kila mwaka Serikali inatoa shilingi bilioni, bilioni halafu hazirudi na hazina maendeleo kule zinakoenda. Mara nyingi vinakuwa ni vikundi hewa, na watumiaji hewa, halafu hela nazo zinakuwa hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nitajadili ukubwa wa Halmashauri yangu ya Geita. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, nilikuwa ninajaribu kuangalia mtandaoni hapa, Halmashauri ya Geita peke yake Mkurugenzi ana Wabunge watatu. Tunayo population ya watu 1,200,000. Nikawa ninaangalia kwa ndugu zetu Lindi, Mkoa mzima una watu milioni moja na laki moja na kidogo. Sisi Halmashauri moja, ina watu milioni 1,200,000, kuna ugumu gani kutugawanya tukapata angalau Halmashauri mbili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anatoka kilometa zaidi ya 89, hadi 100 kupeleka tatizo la kugongewa muhuri na Mkurugenzi! Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri katika vipaumbele vya TAMISEMI, ni vizuri kwa sababu Mkurugenzi mmoja huwezi kuwa na kichwa cha ku-manage Wabunge watatu, wenyewe watata kama akina Musukuma, tutauana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri mkatutenganisha tukawa na Halmashauri mbili na majengo yapo tumeshajipanga, wakikata Halmashauri nyingine majengo ya kuanzia yapo, na hospitali tunazo mbili, hakuna ugumu wa kutugawanya tukawa Halmashauri mbili. Oneeni huruma watu 1,200,000 tunazidi Mkoa wenye Majimbo karibu ya saba, haiwezekani! Ninaomba hili suala tulipe kipaumbele.
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninataka kujadili kuhusiana na suala la stendi. Ninasikia watu tunazungumzia stendi na masoko. Ni kweli tunahitaji kuwa na stendi nzuri, tunahitaji masoko mazuri, lakini tunahitaji pia kujifunza wapi tumekosea?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Joseph Musukuma, kuna taarifa.
TAARIFA
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninampa taarifa Mheshimiwa Mbunge, kwanza, amesema ana miaka 20 kwenye Bunge hili, na wakati anachangia suala la 10% kwamba sheria ile imeelekeza Wakuu wa Wilaya, Kamati za Ulinzi na Usalama zisimamie, je wakati huo inapitishwa Mheshimiwa Msukuma hakuwepo?
MWENYEKITI: Usiulize swali, si unatoa taarifa!
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampa taarifa hiyo tu kwamba hakuwepo?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma huna haja ya kushughulika na hilo ni swali.
Waheshimiwa Wabunge, ninaomba mtu anayetoa taarifa akae kwenye kiti chake. Huyu aliyetoa taarifa anasomeka kama ni Mheshimiwa Nassari hapa, lakini ninajua siyo Mheshimiwa Nassari.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, ninamshauri njuka ajifunze kwanza, asiende speed.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, nilikuwa ninazungumza suala la stendi na masoko. Ni vizuri tukajifunza tulipokosea. Kweli mimi ninajaribu kuangalia, angalieni uwekezaji wa Dar es Salaam kwenye stendi ya Magufuli, angalieni stendi ya Ndugai, angalieni stendi ya Mwanza - Nyegezi, angalieni Nyamhongolo ni mabilioni ya fedha tumewekeza, lakini haifanyi chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukusanyaji wa mapato ya stendi hauendani na majengo mazuri wanayoweka ya vioo na maghorofa. Abiria anatoka nyumbani anajua anakosafiri anaenda wapi? Kama tumefeli, bado tena tunaenda kulundika, kwa nini hizo fedha tusizigeuze tukaenda kuboresha shule zetu za msingi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunajivuna tuna shule nzuri za sekondari. Mheshimiwa Mbunge yeyote asimame hapa, akafanye ziara kwenye shule za msingi za watoto wetu muone jinsi wanavyokaa, na ule ndiyo msingi unaomtengeneza mtoto kwenda sekondari. Watoto wanakaa chini, watoto wako 400 kwenye darasa moja, lakini tunaenda kulundika stendi ambazo zinabaki kuwa majengo ya popo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Stendi ya Ndugai hapo, nendeni mkaone, na soko la Nane Nane, nendeni Mwanza. Hakuna mtu anatoka nyumbani anawahi safari. Unamwambia akakae ghorofa ya tatu, hakuna hicho kitu. Mtu anatoka nyumbani na mawazo yake ya kwenda kusafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tukatengeneza vitu ambavyo vina uhitaji. Kwa sasa, tuache kwenda kuiga vitu ambavyo pengine hatujafika muda wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu vikao. Kwenye halmashauri zetu sisi Wabunge tuko kwenye Kamati za Fedha, ni kweli tunakubali, lakini sasa vikao vinakuwa vinapishana. Yaani wewe uko huku busy na kule kuna kikao. Kwa nini vikao visifuatane na ratiba za Kibunge? Kuwepo na waraka, na Waheshimiwa Wabunge wapewe heshima kualikwa na siyo kushtukizana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemi kwa ubaya. Sasa, inawezekana kulingana na ugumu wa maisha au nini, hakuna kitu kinachofanyika. Ni mara chache kukuta watu wanasoma na kujadili. Unakuta vitu vibaya vinapita wakati sisi Waheshimiwa Wabunge tuko kwenye vikao vyetu vya muda mrefu, kama hivi vya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninashauri upelekwe waraka, Waheshimiwa Wabunge wapate muda wa kwenda kujadili mambo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu TARURA. Kwa kweli ninampongeza sana Mtendaji Mkuu wa TARURA. Hakuna Mheshimiwa Mbunge hatampongeza Seff humu ndani. Ninajua kwamba na fedha zinakuja kidogo, lakini anazi-manage vizuri. Watu kama hawa kwa kweli ikifika muda, hata kama anastaafu, ukimwekea songesha au bando, siyo mbaya kwa sababu utendaji wake ni mzuri na sisi tunamkubali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, kama kuna uwezekano, tuendelee kumpatia fedha, kwa sababu matatizo mengi ya Waheshimiwa Wabunge humu ndani yanasaidiwa sana na TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu miradi. Ni vizuri tuwe tunaanzisha miradi halafu tunaimaliza. Huko kwetu tuna vituo vya afya vimepewa fedha tangu mwaka 2022, lakini mpaka leo vitendea kazi hatujapeleka kule ndani, yamegeuka tena kuwa majengo ya popo, au yanageuka kuwa vituo vya kupima kliniki. Siyo matarajio ya watu, na sisi Waheshimiwa Wabunge tulioenda kuyasema. Kwa hiyo, ni vizuri sana tujitahidi kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni la kushauri. Wabunge hawa ndio wanaosimama kuzungumza huko majimboni, kwamba mkinichagua, mkiichagua Serikali tutawakopesha 10%. Sasa sijui ni kanuni au sijui ni taratibu gani? Kwenye kupitisha, kufanya kila kitu, kueleza majukwaani, kuulizwa maswali ni Mheshimiwa Mbunge, lakini muda wa kutoa ile mikopo, anayetakiwa kwenda kutoa ni Mkuu wa Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya anawajibikaje kwenye kitu nilichokiahidi mimi? Kwa nini haya mambo yasirudi kwa aliyekiahidi? Mimi si ndiye niliyesema kuwa tutawapa mikopo? Kwani kuna ugumu gani mimi nikienda kukabidhi mikopo, na ndiye nitakayewadai kwenye halmashauri yangu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanatupoka madaraka yetu wanawapa Wakuu wa Wilaya. Mengine watupe sisi, kwa sababu mimi ndiye nitakayeulizwa, kwamba ulituahidi mikopo, mikopo iko wapi? Kama nimeenda, nimetoa, nitakuwa nimefanya kazi yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri tunao Wakuu wa Mikoa, na hapa ninampongeza Mkuu wa Mkoa wangu, yuko hapa na wageni wengine. Mwendokasi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu ndio twende nao huo huo kwenye jamii. Mimi ninaaibika, anafika Mheshimiwa Waziri Mkuu anaanza kuulizwa maswali hadi ya ndoa, na sisi tuko kule. Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa pia, nawaomba, twende na hiyo kasi ya Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)