Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuwa mchangiaji wa kwanza siku ya leo kwenye hotuba hii nzuri ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwa kumpongeza Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa mbele yetu, hotuba iliyojaa matumaini kwa Watanzania, yeye pamoja na wasaidizi wake wote. Hii ni ishara kubwa kwamba Watanzania sasa wanaenda kupata tumaini jipya kwenye hotuba hii ambayo iko mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaendelea kumpongeza Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya, ziara zake zimeendelea kuleta matumaini makubwa sana kwa Watanzania. Nasi tumekuwa mashahidi, tumeona namna ambavyo Watanzania wengi wanatoka eneo moja kwenda eneo lingine kufuatilia hotuba zake na kupeleka kero zao. Hii yote ikiwa ni ishara kwamba wanayo matumaini makubwa sana kwake na wasaidizi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa na la msingi ambalo tunapaswa kumshauri Waziri Mkuu, ni namna bora ya kuimarisha mifumo ya kiutendaji ili changamoto hizi zisimfikie peke yake, kwa sababu Waziri Mkuu hawezi kutembea mikoa yote, hawezi kuwa siku zote anawasikiliza wananchi hawa. Hivyo, wasaidizi wake kwenye ngazi za mikoa, wilaya mpaka vitongoji, waweze kufanya kazi vizuri zaidi ili hizi changamoto ziweze kutatuliwa, na baadaye yeye akifika akutane na mambo makubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea pia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna ambavyo imeendelea kuwajali Watanzania, namna ambavyo imeendelea kutoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo, hii yote ikiwa ni ishara ya upendo wa Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi tunavyozungumza hapa, fedha za miradi ya maendeleo zimeendelea kushuka. Mimi kwenye Wilaya yangu ya Chunya tumeona namna mwezi uliopita tumepata fedha za miradi ya maendeleo. Tumepata zaidi ya shilingi milioni 750 kwa ajili ya kujenga kituo kipya cha afya kwenye Kata ya Mbugani, tumepata shilingi milioni 486 kwenye kituo cha Afya cha Isangawana na shilingi milioni 250 kwa ajili ya zahanati ya Matwiga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mifano michache ya namna ambavyo Serikali imeendelea kutoa fedha na zimeendelea kufika huku chini kwa wananchi na kwenda kutatua changamoto mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa wasimamizi, waendelee kwenda kuzisimamia hizi fedha ili thamani ya fedha iweze kuonekana. Miradi iwe katika ubora unaotakikana na iishe kwa wakati ili Watanzania waendelee kukipenda Chama Cha Mapinduzi, kumpenda Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, pia waone yale waliyotutuma, tumeyafikisha Serikalini na Serikali inaendelea kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapotoa hizi fedha siyo kwamba bajeti itaendelea kutosheleza muda wote, tumeona namna ambavyo Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anaendelea kutafuta fedha, na ameendelea kutoa rai kwamba tujibane kwa kile kidogo tulichonacho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake ya hivi karibuni, amesisitiza na kusema kwamba, tuendelee kubana matumizi na kuendelea kubana matumizi huku ili kile kidogo tulichokuwa nacho kiweze kufanya kazi iliyokusudiwa, naye ameweza kuonesha, akasema hata kwenye misafara ya wasaidizi wake iendelee kupunguza idadi ya watu, iendelee kupunguza msafara aliokuwanao na ametuonyesha kwa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati anaenda kuzindua minara ya mawasiliano, alienda na magari machache na wasaidizi wake walienda kupanda mabasi. Hii yote ikiwa inatuonesha kwamba Rais anatuongoza kwa mifano na wasaidizi wake wengine Serikalini waige hilo ili mambo mengine mazuri zaidi yaweze kwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, pamoja na mambo mengi aliyozungumza ameweza kuzungumza namna ambavyo uwekezaji na uendelezaji wa wafanyabiashara unaendelea kukua mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye hotuba yake namna ambavyo uwekezaji mpya umeweza kusajiliwa zaidi ya miradi 927. Miradi 927 ni mingi na yenye thamani zaidi ya dola milioni 11. Hizi fedha ni nyingi sana, na tunaona nchi yetu inavyoendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yako ndani ya nchi yetu, bado tunayo changamoto ya regulatory kuwa nyingi. Kodi za Serikali ni nyingi. Kila mmoja anaangalia mahali pa kupata fedha. Hivyo, tunaona namna ambavyo kwa uwekezaji huu, wawekezaji wetu wengi watashindwa kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalan, kwenye Wilaya yangu ya Chunya, sehemu kubwa ya uwekezaji kule, ni uchimbaji wa madini. Wachimbaji wanazidi kuongezeka, na maeneo ya wachimbaji wengine, lakini tozo na kodi ambazo wachimbaji wanazipitia ni nyingi kiasi kwamba wachimbaji wetu hawa wanapata fedha (kwa maana ya kuangalia maduhuli), lakini hawapati faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalan, tunaona mwekezaji huyu ambaye ni mchimbaji, analipa leseni ya biashara, analipa mrabaha, analipa leseni ya Halmashauri kwa maana ya Service Levy, analipa tozo mbalimbali, analipa TRA, analipa OSHA, analipa fire, analipa Mkemia wa Serikali, analipa NEMC, analipa NSSF, analipa SDL kwa ajili ya vibarua wetu, tozo na kodi ni nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya juhudi za maksudi, wachimbaji wetu na wawekezaji hawa wataweza kuwa tunawatafuta wengi, lakini mwendelezo wao unakuwa haupo. Ninaishauri Serikali ichukue juhudi za makusudi kuona namna ya kupunguza hizi authority, ziwe chache na kodi ziweze kuunganishwa ili kuweza kumsaidia mwekezaji katika nchi yetu. Bila kufanya hivyo, leo kila mmoja ana mamlaka ya kwenda kufungia biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtu wa OSHA anaweza akaja akafungia biashara kwamba hujalipa, TRA akafungia biashara hujalipa, Halmashauri akafungia biashara hujalipa, mpaka mtu wa kijiji anaweza kwenda kufungia biashara. Sasa, hatuwezi tukawa na mfumo ambao uko holela kiasi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima Serikali ione namna kuwe na utaratibu maalum wa watumishi hawa na mamlaka hizi ziweze kuungana kwa pamoja ili kuweza kumsaidia mwekezaji, hasa uwekezaji kwenye sekta ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya, tumeona nchi yetu maeneo mengi mvua nyingi sana zinanyesha. Mvua hizi zimeharibu barabara nyingi na madaraja, na kila Mbunge anayesimama hapa anazungumzia changamoto ya barabara. Naomba Serikali ichukue kwa hali ya udharura kutoa fedha ili barabara hizo ziweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu Serikali ya Awamu ya Sita imepandisha kwa kiasi kikubwa sana bajeti ya TARURA kutoka ilivyokuwa inaingia zaidi ya shilingi bilioni 290 mpaka leo tumefikia shilingi trilioni 1.2. Pamoja na kupandisha bajeti hii kuwa kubwa, bado uhitaji wa barabara zetu hasa za vijijini ni mkubwa sana. Hivyo, tuone namna ya kuzifikia hizi barabara kwa ajili ya wananchi wetu wa kule vijijini ambako zimeharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yangu ya Chunya barabara zimeharibka sana. Kwa mfano, barabara ya kutoka Kiwanja – Mlimanjiwa kwenda Ifumbwa; njia panda kwenda Sangambi; Chunya Mjini – Chokaa – Mapogoro; Lupa – Luhalaje na barabara nyinginezo. Barabara hizi zote zinahitaji fedha nyingi za kutosha ili zikatengenezwe. Bila kuwa na chanzo kingine mbadala hatuwezi kwenda kufikia hatima hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri, pamoja na Serikali kutoa hizi fedha, ione namna Halmashauri ambazo zina uwezo wa kusimamia na kujiendesha ziweze kupunguziwa masharti na ziwekewe masharti maalum ziweze kukopa mikopo ya kibiashara ili wapate fedha watengeneze barabara, hasa barabara za kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatusaidia sana, zitatengenezwa barabara ndani ya muda mfupi, wao wataendelea kulipa kidogo kidogo na wananchi huko wataweza kuona faida. Hii ndiyo ambayo itakuwa imetusaidia na itaweza kusaidia mambo mengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na barabara hizi za TARURA, bado barabara zinazosimamiwa na TANROADS zimeendelea kuwa kikwazo. Barabara hizo ni za Mkoa wa Mbeya hasa tunapozungumza barabara ya TANZAM, barabara ya kuanzia Igawa kupita Mbeya Mjini mpaka Tunduma ambako ndiyo lango kuu la SADC la biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza, barabara ile ndiyo namba moja ndani ya nchi hii, maana yake ni T1, lakini leo barabara hii ni mbovu, haipitiki. Tukumbuke katika mizigo inayopita kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam, zaidi ya 40% inapita barabara ya TANZAM. Hivyo tuangalie kwa jicho la kipekee barabara hii itengenezwe, tena kwa udharura wake ili iweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ‘B’ yake ni barabara inayotuunganisha Mkoa wa Mbeya inapita Chunya – Makongorosi kwenda mpaka Singida, kwa maana barabara inayoanzia Makongorosi – Mkiwa na yenyewe iangaliwe, itengenezwe kwa kiwango cha lami, iweze kupitika vizuri, na wananchi wa Chunya hasa Tarafa ya Kipembawe waone namna ambavyo Serikali yao inawajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mengi ya kuishauri Serikali hasa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, lakini pia nitachangia kwa maandishi ili mchango wangu uweze kuingia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)