Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jerry William Silaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi ninaomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa kibali cha kusimama hapa siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru wewe binafsi kwa kutuongozea kikao hiki vizuri. Umekuwa ukifanya hivyo mara nyingi tunaposimama hapa. Kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Wizara na wewe ninakuombea Novemba tukutane hapa na tunaamini kwa jinsi ulivyokuwa ukiongoza vikao vyetu, Waheshimiwa Wabunge watakurejesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi zaidi ninaomba nipongeze, tumepata wachangiaji 11 na mchangiaji mmoja wa maandishi, Mheshimiwa Luhaga Mpina, ametuletea mchango wa maandishi. Wachangiaji wengi wamepongeza sana na kushukuru kazi kubwa iliyofanywa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, minara ya simu inajengwa; ipo ile 758 ambayo ilikuwa inakamilika tarehe 12 Mei, imebaki michache. Alisema Mheshimiwa Sanga, ya maeneo ya hifadhi, maeneo ambayo mvua zimeathiri barabara. Iko minara 636 imeanza kujengwa na kuna awamu nyingine ya 11 ambayo tayari zabuni imetangazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme mbele ya Bunge lako, shukrani na pongezi zote hizi zimwendee Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yeye hasa ndiye kinara wa utekelezaji wa digitalization ya nchi yetu. Amekuwa akituelekeza, amekuwa akitupa fedha na amekuwa akihakikisha miradi hii inakamilika. Vilevile ninawashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha yanafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata maelekezo na maoni ya taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge. Ninakuthibitishia kwamba maoni na maelekezo yale yote tutayatekeleza. Masuala ya startups, masuala ya Digital Technology Institute, masuala ya ujenzi wa Data Centre, masuala ya kujenga zile incubation hubs za startups, masuala ya kuitumia Maabara yetu ya Vifaa vya TEHAMA vizuri, yote tutayatekeleza na tutapeleka utekelezaji wake kwa maandishi kwenye Kamati ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu kwa kifupi nisemee maeneo matatu; Waheshimiwa Wabunge wote wamechangia vizuri na maeneo yote nikiri kwamba tumepokea na kwa sababu Wizara hii ni Wizara ya TEHAMA, tutawajibu. Tutawajibu kwa maandishi, lakini ninaomba niyasemee maeneo matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni Waheshimiwa Wabunge waliochangia kuhusu cashless economy. Ninawathibitishia kwamba maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mradi wa Digital Tanzania Project (DTP) ni kuhakikisha mifumo inasomana na kazi kubwa imefanyika. Unaposikia Jamii Exchange ni mfumo ambao utasaidia taasisi zote za Serikali na binafsi kubadilishana taarifa na kwenye hotuba yangu nimeelezea mifumo ambayo imeshakwisha kusomana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kupitia Jamii Pay tunatengeneza platform ambayo itafanya kile alichosema Mheshimiwa Mtaturu na Waheshimiwa wengine, cashless economy na kwenye Jamii Pay ipo ile kadi iliyokuwa inaitwa N-Card ambayo sasa itakuwa ni Jamii Card, ambayo itakuwa both physical card lakini vilevile tunatengeneza soft card, ili taasisi zote binafsi na za Serikali ambazo zina nia ya kufanya malipo zipitie kwenye platform hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, jana alitembelea NIDC pale Dar es Salaam na amejionea mafanikio makubwa ya kazi inayofanywa na Wizara kwa maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ni matumaini yangu kwamba katika kipindi kifupi kijacho Bunge lako hili likitupitishia bajeti yetu likatupa kazi hii, tutaenda kuifanya kwa kasi na weledi wa hali ya juu na kuhakikisha tuna-integrate miamala ya simu, benki, kupitia mifumo ya BOT ili tuwe na cashless economy na ndio njia pekee ya kuwa na Taifa la watu ambao unaweza kuwajua wapo wapi, Mheshimiwa Bashe leo akitaka kugawa mbolea agawe kwenye mfumo wa pamoja, mikopo ya elimu ya juu ipatikane pamoja, watoto wapangiwe miradi ya elimu pamoja, ndio unified jamii data lake tunaenda kuitengeneza, na ndio kazi tunayoenda kuitekeleza bajeti hii ikipita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ninataka kulisemea kwa kifupi ni suala la utapeli na ulaghai mitandaoni. Amesema vizuri Mheshimiwa Naibu Waziri kuna Kampeni ya Sitapeliki, pia juzi tulizindua mfumo ambao ume-base kwenye artificial intelligence wa Kampuni ya Airtel ambao unatoa sms alert kwa sababu message nyingi zile za kilaghai ni message ambazo akili unde inaweza ikazing’amua na kuweza kuwatahadharisha watumiaji. Nilitoa wito kwenye shughuli ile, lakini ninaomba kutumia Bunge lako Tukufu kuendelea kutoa wito kwa kampuni nyingine kuja na solution za kibunifu, ili tuweze kuwalinda watumiaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza vizuri Mheshimiwa Salome tunaenda kwenye uchaguzi. Kupitia akili mnemba/unde (artificial intelligence) zipo video na sauti zinatengenezwa. Hotuba ninayoitoa hapa kesho mtu anaweza akatengeneza picha ya video niliyopo hapa, lakini ninachozungumza anaweza akakitengeneza kwenye akili mnemba nikazungumza maneno tofauti kabisa ninayozungumza hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuthibitishie sisi ni wanachama wa ITU (International Telecommunication Union). Ukisoma global security index iliyotoka Septemba 2024, Tanzania ni nchi ya tatu kwa usalama wa mtandao na tumewekwa kwenye Tier One ya usalama wa mtandao. Kwa hiyo, niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu kwmaba, TCRA imejipanga na nitoe wito ama onyo kwa Watanzania, wale ambao wanajiona wanapenda kutumia mitandao kwa namna ambayo ni hasi, wengine wanatumia picha ya mtu wanaituma kwa grok wanamwambia hebu tuvulie nguo, tuchezeshee mziki, tunayo mitambo ya kisasa.

Niseme kupitia Bunge lako, sheria zipo na niwaelekeze TCRA waongeze umakini kuwalinda Watanzania, wananchi na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa ambao wanaeda kwenye chaguzi kuwasaidia wananchi wafanye uchaguzi katika hali ambayo itakuwa haijaingiliwa na mitandao hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu limesemwa hapa na Waheshimiwa Wabunge wengi juu ya mandatory listing kwenye stock exchange kwa kampuni za simu na kampuni nyingine za TEHAMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kukiri kwamba tumesikia, Serikali imesikia na imepokea. Kwa uchungu mkubwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia wamenirudisha mimi darasani kwenye darasa la MBA kwenye Corporate Finance, how to raise capital, jinsi ya kuweza kuendeleza mitaji kwenye kampuni na njia hii kama alivyosema Mheshimiwa Kapinga ninaamini ilikuwa ni nia njema ya Serikali kwamba umma wa watanzania umiliki uchumi wa kampuni hizi za simu. Kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge kwamba kilichoenda kutokea inaonekana ni tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri tumelipokea na ninaomba niahidi mbele ya Bunge lako kwamba kwa dhati kabisa nimechukua hoja hii kwa uzito kama Waheshimiwa Wabunge walivyowasilisha hapa. (Makofi)

Mimi ninawaomba watuamini na waniamini, tulichukue nikitoka hapa ninathibitisha na kuomba kusema tena nikitoka hapa muda huu nitakaa na wenzangu Wizara ya Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali tukae na wadau tuliangalie na tutafute solution ya jambo hili bila kuathiri wananchi wetu na sheria za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikushukuru tena kidhati, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, lakini pia ninaomba nimshukuru tena Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye imempendeza nimsaidie kazi kwenye hii Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Ninaomba niendelee kumuahidi kwamba imani yake nitailipa kwa kazi. Nitaendelea kufanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha mkitupitishia bajeti hii tunaenda kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha masuala haya ya communication na ICT tunayafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niendelee kuwashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi anayoifanya kunisaidia, Katibu Mkuu, watendaji, wadau wetu, makampuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niendelee kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ukonga. Sisi tunaopata fursa ya kufanya kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais tunatumia muda mwingi kuwatumikia Watanzania wote. Niwashukuru wananchi wa Jimbo la Ukonga kwa uvumilivu wao, dua zao, na kunistahimilia pale ambapo nitakuwa ninatekeleza majukumu ya kiserikali. Ninaendelea kuwaahidi siku zote interest ya Ukonga itakuwa moyoni mwangu na nitaendelea kuwahudumia kuhakikisha maendeleo yale ambayo Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyapanga kuyatekeleza yataendelea kutelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo ninaomba sasa kwa heshima, taadhima na unyenyekevu mkubwa nitoe hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutoa hoja. (Makofi)