Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mungu anayeendelea kinijalia afya na nguvu za kuendelea kuwatumikia Wana-Kyerwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa na nzuri kwenye sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari bila kuwasahau wasaidizi wake Naibu Waziri pamoja na watendaji wa Wazira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ya simu na redio; naipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha mawasiliano ya simu kwenye maeneo mengi Wilayani Kyerwa. Kyerwa kulikuwa na shida kubwa ya mtandao wa simu ikiwemo internet, sehemu nyingi ulikuwa ni mawasiliano kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda, lakini kwa sasa hali ni nzuri kwa sehemu kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo bado mawasiliano ya redio zinazosikika ni za nchi ya Rwanda na Uganda, niombe sana Serikali kukamilisha mtambo wa redio ili Wana-Kyerwa na wao wasikie matangazo na taarifa mbalimbali zinazohusu nchi yao, hii iwe sambamba na kuboresha mtandao pale makao makuu ya Wilaya ikiwemo kujenga minara maeneo yote yenye shida na mawasiliano ambayo tayari yalishaainishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wizi wa kwenye mtandao; pamoja juhudi zinazoendelea kuchukuliwa bado wizi wa kwenye mtandao ni mkubwa sana, najuliza inakuwaje mtu anakupigia kwa namba unayoijua anakuomba pesa kwa namba hiyo hiyo na ukituma pesa inaleta jina halisi la mwenye namba ila baadae ukifanya mawasiliano na mwenye namba anakuambia hajakuomba hela!
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu wanawezaje kuchezea namba ya mtu bila kuwa na mtu kutoka kampuni ya simu na wanajuaje kwenye simu yako kuna salio kama hana mtu anayewasiliana naye kutoka kampuni ya simu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atupe ufafanuzi juu ya huo wizi wa kwenye mtandao na ni hatua zipi zinachukuliwa kwa wizi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchafu kwenye mitandao ya kijamii; kumekuwapo na mmomonyoko wa maadili kwenye mitandao ya simu, ukifungua mtandao wowote wa kijamii unakutana picha chafu zinakuja zenye uchafu wa kutisha, watoto wetu tunawapeleka wapi? Tunaandaa kizazi cha kingono ngono, kizazi cha uzinzi, hii ni hatari kwa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Serikali imejipangaje kudhibiti uchafu huo kwenye mitandao ya kijamii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na ahsante.