Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry William Silaa (Mb.) na Naibu wake Mheshimiwa Engineer MaryPrisca Mahundi (Mb.), Katibu Mkuu Ndugu Mohamed Khamis Abdallah, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Nicholaus Merinyo Mkapa na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye changamoto kwanza za udanganyifu unaofanywa na matapeli wa mitandaoni; pili, huduma za mawasiliano na kupata habari kwa watu wenye ulemavu wa usikivu (viziwi) na tatu, tatizo la mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya jimbo langu la Moshi Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza utahusu tatizo la changamoto ya udanganyifu unaofanywa na matapeli wa mitandaoni kwa kutumia namba zilizosajiliwa na makampuni yetu ya simu hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa jitihada ilizochukua kuzuia uhalifu na ulaghai wa mitandaoni kupitia Kampeni ya SITAPELIKI na kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama wa mitandaoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada za Serikali, bado kumekuwa na wimbi kubwa la mashambulio ya mtandaoni ambapo maharamia huingilia accounts za wateja za whatsApp au zile za kawaida kwa kutumia namba zilizosajiliwa na makampuni yetu ya simu hapa Tanzania na kutuma sms za kutapeli. Pia kumekuwa na wimbi la matapeli kupiga simu na kufanya udanganyifu wa kuomba pesa kwa kusingizia kutumwa na watu maarufu au wenye majina wakubwa au kwa kutumia vishawishi vikali vya kumhadaa anayetapeliwa. Kwa kiasi kikubwa uharamia huu bado unaendelea na umekuwa ni kero kubwa kwa Watanzania wanaotumia huduma za simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limewaliza Watanzania wengi kwani wamepoteza kiasi kikubwa cha fedha. Kwa hali ilivyo sasa, usalama wa taarifa za simu zetu huko mitandaoni na ulinzi wake wa faragha ni shida kubwa inayokabili wateja wengi wanaomiliki simu hapa nchini Tanzania. Hivyo basi kuna umuhimu wa kuongeza juhudi kukabiliana na changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto hii, sasa ni wakati muafaka wa Serikali kufanya maboresho ya sheria zilizopo au kuanzisha sheria na sera za usalama wa mtandaoni. Serikali inapaswa kuanzisha sheria kali na sera zitakazolinda ulinzi wa taarifa za watu mtandaoni. Kwa mfano, kwa kuwa matapeli hufanya uhujumu kwa kuibia wateja fedha zikiwemo za Serikali, basi watakaonaswa katika uhalifu wa aina hii washtakiwe kwa kosa la kuhujumu uchumi. Sheria kali kama hii itasaidia kupunguza uhalifu wa mtandaoni na kuongeza imani ya watu katika kutumia huduma za kidijitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili unahusu huduma ya mawasiliano na kupata habari kwa watu wenye ulemavu wa usikivu (viziwi) nchini Tanzania; viziwi ni moja kati ya makundi ya watu wenye ulemavu wanaohitaji huduma maalumu kwenye mawasiliano ili waweze kuendana na mambo mbalimbali. Matatizo waliyonayo viziwi huwakwaza kupata mawasiliano katika mazingira wanayoishi na hivyo kuwaathiri kupata haki yao ya elimu, ajira, mahusiano katika jamii na maisha yao kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya viziwi ni ya kimawasiliano, viziwi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kusahaulika katika utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali iwekeze kikamilifu na kuweka miundombinu na rasilimali watu ya kutosha ili kundi hili lipate haki yao ya msingi ya kupata mawasiliano na jamii inayowazunguka. Viziwi wakishatambulika katika jamii, wapelekwe katika shule zao maalumu na wapatiwe elimu ya alama au ya aina nyingine ile itakayowasaidia kwenye mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mikakati ya muda mrefu ya kukabiliana na changamoto hii, ni vyema lugha ya alama ifundishwe kama somo kwa wanafunzi wote kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kurahisisha mawasiliano kwa viziwi pote nchini. Hii ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa wezeshi vinavyohusisha lugha za alama kwa kutumia kitafsiri janja cha viziwi katika kusanyiko na kitafsiri janja cha viziwi cha mtu mmoja.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa tatu utahusu tatizo la mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya jimbo langu la Moshi Vijijini. Kwanza kabisa niishukuru Serikali kwa jitihada kubwa za kupeleka mawasiliano karibu na watu kwani hapa nchini imejengwa minara 758 na kuiongezea uwezo minara 304 kutoka 2G kuwa 3G. Naishukuru Serikali kwani katika Jimbo la Moshi Vijijini nimejengewa minara katika Kata za Mabogini, Kibosho Kati, Kibosho Magharibi na Uru Shimbwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na huduma ya kujengewa minara niliyoainisha hapo juu, bado kwenye jimbo langu kuna maeneo yenye changamoto kubwa ya mawasiliano. Hii imetokana na maeneo haya kutokuwa na mvuto wa kibiashara, na mashirika ya kibiashara (Mix by YAS, Vodacom, TTCL, Halotel, Airtel) hayajawekeza kujenga minara ya mawasiliano kwenye maeneo haya. Maeneo haya ni yale yanahusisha vijiji vinavyopakana na Mlima Kilimanjaro katika Kata za Kimochi, Mbokomu, Kibosho Mashariki na Oldmoshi Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kupitia kwenye Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iwekeze na kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo haya. Kata hizi ni za kimkakati kwani baadhi zina vivutio vya watalii na baadhi kuna njia za kitalii kupanda Mlima Kilimanjaro. Ni muhimu watalii wakiwa katika maeneo haya waweze kutumia simu zao kwa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba kutokana na kushamiri kwa uhalifu wa mitandaoni hapa Tanzania, ni muda muafaka wa kuboresha mazingira ya kisheria na sera ili kulinda taarifa za wateja huko mitandaoni. Kwa kuwa viziwi wamekuwa wahanga wa kutopata huduma stahiki za kijamii hapa nchini, Serikali ichukue hatua za makusudi za kuhakikisha viziwi wanaweza kufanya mawasiliano na jamii inayowazunguka kwa sababu mpaka sasa viziwi wengi wana changamoto kubwa. Teknolojia ya kuwasaidia viziwi kufanya mawasiliano si anasa bali ni haki yao ya msingi na daraja la kuwapatia usawa katika jamii. Mafanikio ya hili jambo litawaongezea matumaini, heshima na nafasi ya kujitegemea. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa maendeleo ya kiteknolojia yanamfikia kila kiziwi bila kumwacha nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.