Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususani barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Jerry William Silaa, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na taarifa ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, inaonesha kuna mafanikio makubwa kwenye sekta za Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hasa katika mikakati ya kupunguza gharama za mawasiliano kwa wananchi. Utendaji kazi ulilenga pia kuboresha miundo ya TEHAMA kuwezesha mwelekeo mzuri wa kuleta ubunifu ili Tanzania iendane na kasi ya dijitali ya kiuchumi (digital economy).
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza msukumo mkubwa kwenye kuendeleza maboresho ya mtandao wenye kasi zaidi na kuhakikisha matumizi mazuri ya Data Center ili kuwezesha ubunifu wa miundombinu ya TEHAMA hasa Serikalini iweze kusomana. Kutokana na kuwepo mifumo tofauti kwenye taasisi za Serikali ni muhimu sana kuunganisha mifumo yote iweze kusomana ili kuleta ufanisi unaoendana na dunia ya leo. Mwelekeo wa dunia ya leo ni kufanya shughuli zote za kitehama, nashauri Serikali kuboresha muundo wa Wizara na taasisi zake ili kuwepo na idara mahususi itakayoongozwa na Afisa TEHAMA Mkuu (CIO) ngazi ya Kamishna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa muunganiko wa mifumo yote (Core Government System), ni muhimu kuboresha e-government na itawezesha ufanisi na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa sana. Kuwepo kwa Mkongo wa Taifa na Data Center ni fursa kwa kuwezesha kutengeneza mfumo wa kuratibu na kuendeleza ubunifu katika TEHAMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, teknolojia imewezesha huduma ya kifedha juimishi (financial inclusion) na hii fursa pia kwa Serikali kuratibu miamala ili iwe sehemu ya mfumo rasmi wa malipo kwa usimamizi wa Benki Kuu na TCRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza maboresho kwenye tozo za miamala itayoongeza mapato ya Serikali, lakini ikizingatia kupunguza mzigo kwa wateja. Serikali kwa kushirikisha wadau, itumie uzoefu wa sasa kuboresha huduma za miamala kwa kuoanisha ufanisi kwa huduma ya kifedha juimishi na tozo mbalimbali na mchango wa huduma hii kwenye kukuza uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Wizara ikiwemo zoezi la postikodi, bado kuna maeneo mengi ambayo bado hayajapata huduma za minara ya mawasiliano na hata kwenye maeneo kadhaa yenye minara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya hayapati huduma ya mawasiliano. Vijiji vingi ikiwemo katika Kata za Ulenje, Iyunga Mapinduzi, Mshewe, Mjele, Ilembo na Ihango havina minara na vingine kuna minara ambayo kwa muda mrefu haina mawasiliano. Kwa kuzingatia lengo la kupeleka TEHAMA kwa kila shule, Serikali iharakishe kujenga minara maeneo yote kwenye vijiji na vitongoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kupitia Tume ya TEHAMA iweke msukumo zaidi wa ujenzi wa vituo vya kukuza bunifu za TEHAMA kwenye mikoa na wilaya zote za Tanzania. Serikali iendelee kutenga fedha kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ili kutekeleza azma ya ujenzi wa minara zaidi nchini kote. Pia Serikali iboreshe usikivu kwenye minara yenye changamoto za usikivu na msukumo uwe kuwekeza kwenye mifumo ya 4G na hata 5G kwa mijini mpaka vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) likamilishe mradi wa ufikishaji Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye nchi jirani zinazotuzunguka ikiwa ni sehemu ya kuboresha mawasiliano na wakati huo huo kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali ifanye maboresho ya Mfumo wa NaPA ambao ni mfumo wa kidigitali wenye kanzidata ya anwani za makazi. Uboreshaji wa NaPA uwezeshe mfumo kusomana na mifumo mingine ya Serikali ikiwemo, mifumo ya ukusanyaji mapato ya TRA na hata mfumo wa TAUSI unaotumika na TAMISEMI kukusanya kodi ya majengo. Pia maboresho yawezeshe upatikanaji wa huduma za anwani za makazi kupitia USSD code na kuwezesha wananchi kutuma maombi ya kupatiwa anwani ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.