Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji kwenye hoja iliyoko mezani leo iliyoletwa na Waziri wetu Mheshimiwa Jerry Silaa.

Mimi ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninachukua fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan, kwenye sekta hii amefanya mambo makubwa ambayo yameleta mageuzi makubwa. Tunapomsifia Mheshimiwa Rais, tunamsifia kwa kazi zake alizozifanya, na kazi alaizozifanya ziko kwenye takwimu, kwenye statistics kwa sababu tunazo takwimu kwenye finger tips zetu za yale mamabo aliyoyafanya Mheshimiwa Rais baada ya yeye kuingia madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Tanzania tumetoka watumiaji wa internet milioni 29 mpaka milioni 49. Machi 2021 tu tulikuwa milioni 29, leo Machi 2025 tumefika watumiaji milioni 49 na ndiyo maana tunasema Mheshimiwa Rais amefanya mambo makubwa kwenye sekta hii pia. Kutoka milioni 29 mpaka milioni 49 kwenye miaka yake minne tu ya utawala akiwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alisema hapa, sasa tunajenga minara ya simu zaidi ya 750 kwenye kata zaidi ya 713. Hayo ni maendeleo makubwa sana. Makubwa mno, kwa sababu ya kutaka sekta hii ya mawasiliano ikue, Mheshimiwa Rais amepambana kadiri ya uwezo wake kuhakikisha kwamba anawekeza fedha nyingi huku ili sekta hii ikue na ilete maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya internet sasa hivi siyo luxury tena, yameshakuwa sehemu ya maisha yetu kama vile tunavyohitaji chakula, tunavyohitaji nguo, tunavyohitaji nyumba za kuishi, pia kwenye maisha yetu ya kila siku tunahitaji matumizi ya mawasiliano, aidha kwa njia ya internet au njia ya simu kupiga au kutuma sms. Tunawasiliana kwa urahisi, tunatuma fedha. Hata operation sasa hivi hospitalini zinafanywa kwa njia hizi za internet. Hizi zote zimekua kwa sababu kuna uwekezaji wa makusudi umefanywa na uwekezaji huu moja kwa moja umeendelea kukuza uchumi wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo limesemwa sana hapa ambalo na mimi ninataka niliseme, ninatoa ushauri wangu kama mwanasheria; jambo la uwekezaji wa wananchi kununua hisa kwenye Kampuni ya Vodacom.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilipata kusikiliza mdahalo wa wadau wa mawasiliano uliofanywa na Mheshimiwa Waziri. Jambo hili pia liliibuliwa sana na baada ya kuibuliwa nikawa curious kutaka kufuatilia, nikasoma kidogo nikaenda kufanya tafiti, research kwenye sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaliyosemwa na wenzangu waliotangulia kuhusu jambo hili ni kweli. Wote walisema kwa usahihi sana, wote walisema kwamba kweli mwaka 2010 tulitunga sheria tukiwa na lengo na Serikali ilikuwa na lengo zuri kabisa. Lengo lake kipindi kile lilikuwa ni kuruhusu Watanzania kuumiliki uchumi wao, locally ownerships, tulikuwa tunataka locally ownership. Pia tulikuwa tunataka kuweka transparency kwa telecommunication companies, ili kuwe na uwazi wa transactions zao za biashara zinazofanywa kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine ilikuwa tunataka kufanya regulatory compliance kwa sababu tulikuwa tunazo kampuni ambazo nyingi zinamilikiwa na wageni. Kwa hiyo, tulipitisha sheria hii ili kufanya regulatory compliance. Kwa hiyo, tulikuwa tuna lengo zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji dada yangu Mheshimiwa Salome amezungumza kwa uzuri zaidi. Tulitunga sheria tukai-enforce zaidi kwa kutunga Finance Act mwaka 2016, tukaja tukafanya marekebisho mwaka 2022, lakini inavyoonekana Mheshimiwa Waziri ni kama vile kwenye kipengele hiki sheria hii kama vile imegonga ukuta. Siyo yote, siyo EPOCA yote, siyo Electronic and Postal Communication Act yote. Hii ni sheria nzuri kwenye maeneo mengine lakini hapa ambapo wachangiaji wenzangu pia walisema, inaonekana imegonga ukuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria kugonga ukuta inatokea, siyo mbaya, inatokea sana kwenye sekta ya sheria. Ni kama vile mnaitunga sheria halafu mnataka kui-test, inafanya kazi? Inaenda mtaani, sasa ikishafika mtaani ina malalamiko. Wenzangu wametoa malalamiko haya kwa mifano na mifano mingi imetolewa hapa kwamba kuna jambo linatakiwa lifanywe, kuna kitu tulikosea wakati wa kupitisha sheria hii. Tunaweza tukakiri tukarudi nyuma kama Taifa, kama nchi, kama Serikali, tukaja tukaleta marekebisho ili tuendelee mbele tujikwamue hapa tulipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ninahisi tulikosea, kwa maoni yangu; moja ilikuwa ni kuweka ulazima. Kwa sababu, kwenye kifungu cha 26(1)(a) kuna neno ‘shall’ limetumika. Wanataka hao internet sub-providers ambao ndiyo telecommunication companies kwa ulazima zikiwa ni private parastatals. Unazichukuaje private parastatals (mashirika ya private) ukazilazimisha kwa sheria yaingie kwenye soko la hisa? Soko la Hisa kampuni zinaamua zenyewe kulingana na market. Market force inavyokwenda ndiyo zenyewe zitaamua au bodi zao zikishakaa huko zikafanya decisions za kwamba tunataka ku-raise capital (investment capital). Kwa hiyo, kama tunataka tu-raise na hatuna hela, hatuwezi kukopa, lets sell our shares ili tupate shareholders, waingie, watupe fedha, tukawekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tuliweka kipengele cha ulazima wa kisheria kulazimisha hizi kampuni ziingie zika-list kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam? Hapo ni moja kati ya kosa tulilolifanya, lakini tunaweza tukarudi nyuma tukatoa hicho kipengele cha ulazima, tukaziacha zi-operate privately. Hizo kuhusiana na regulatory compliance, transparency zitaendelea na tutaendelea kuzitunza kwenye regulation nyingine, kwa sababu tunazo sheria nyingine tutawatungia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa lingine tulilolifanya ilikuwa ni kuwazuia wawekezaji wa kigeni kipindi kile wasizinunue hizi shares ambazo tulikuwa tunazisema. Tulivyowazuia ndiyo maana hiyo drop ya value ya share ilitokea ambayo hawa watu wanaisema hapa ilitoka shilingi 800 mpaka shilingi 200 kwa sababu sasa huna foreigners wanaoweza kuja ku-chip in kuongeza mitaji, na Watanzania hawanunui tena. Kwa hiyo, kulikuwa na makosa yaliyotokea ambayo tunaweza tukajirekebisha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, Serikali nendeni mkakae mfikirie jambo hili, mje na msimamo au maamuzi ya kwamba tunaweza tukaondoa kipengele hiki ili Vodacom waka-delist, wakae na shareholders wao waliozinunua, waki-delist watapatana wenyewe kwamba ngoja tutawarejeshea fedha zenu ili shares zirudi kwetu tu-operate maisha yaendelee. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ndiyo ulikuwa ushauri wangu kwenu. Ninashukuru sana kwa kunisikiliza na ninaunga mkono hoja. (Makofi)