Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi mchana wa leo na mimi nichangie bajeti ya Wizara hii ya Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema kila mmoja wetu kutimiza wajibu wetu, lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amekuwa akiendelea kulea sekta zote bila kubagua sekta yoyote na maendeleo hayo yanaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ongezeko la bajeti hii ya Wizara hii kutoka shilingi bilioni 180 mpaka shilingi bilioni 291 ni nia njema ya Mheshimiwa Rais wetu kuhakikisha sekta hii inafanya vizuri. Niipongeze pia Serikali kwa jinsi ambavyo wamefanya disbursement katika bajeti hii. Ukiangalia bajeti ya maendeleo katika Wizara hii Mheshimiwa Waziri mmefanya disbursement ya 90% katika shilingi bilioni 140 lakini shilingi bilioni 137 kwenye maendeleo imekuwa disbursed na sekta zake zote zimefikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wetu kaka yangu Jerry, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na timu nzima kwa jinsi ambavyo mmekuwa mkifanya kazi, lakini mmekuwa mkitufikia tunapowahitaji katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia ni mnufaika wa huduma za Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na Wizara nzima. Nilikuwa na maeneo matatu ambayo yalikuwa hayana mawasiliano ya Chemchem, Himiti pamoja na Imbilili. Mlituma wataalamu wenu wakafika kuongeza nguvu katika ile minara na inafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze kwa jinsi ambavyo pia hata katika minara hii 758, minara 482 mmeshamaliza kazi na mnaendelea vizuri, hongereni sana na endeleeni kuchapa kazi bila kuchoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize tu kwa sekta zake Serikali inatenga fedha na disbursement katika miradi ya maendeleo inaenda vizuri. Nadhani sekta zenu ziweze kukusanya vizuri kwenye makusanyo naona kama mko 60%, ninyi mkiongeza nguvu katika kukusanya naamini ipo siku mtajitosheleza na nisisitize kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi naona makusanyo ni 20%, kwa hiyo, ni vyema wakaongeza nguvu katika makusanyo kwa sababu hauwezi ukatumia wakati haukusanyi. Kwa hiyo, 20% ni ndogo sana ukilinganisha na wengine ambao wameweza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mawili ambayo ningependa kushauri; jambo la kwanza, ni suala la kuhuisha mfumo wa takwimu ya makosa ya kimtandao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na wenzetu wa TCRA. Hili ni jambo jema. Mheshimiwa Waziri makosa ya kimtandao yamekuwa yakiwakwaza Watanzania wengi sana. Matumizi ya whatsapp zetu watu wanafanya ku-hack whatsapp zetu lakini simu zetu, message za kitapeli. Kuna watu wanaweza wakawa wanapiga simu tu kusumbua watu, wanatukana, wanadhalilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ifikie hatua sasa ni muda muafaka Mheshimiwa Waziri kama ulivyoeleza kwenye hotuba yako kwamba mtakapohuisha, nashauri muweze kuwaweka pamoja, pawepo na single source ya kuhudumia tatizo hili la makosa ya kimtandao. Kwa sasa hivi tuko na Jeshi letu la Polisi liko Wizara ya Mambo ya Ndani, pia TCRA iko kwenu nimpongeze sana DG Dkt. Jabiri amekuwa akipambana sana. Jeshi la Polisi ni Wizara nyingine, lakini TCRA iko Wizara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa kuwa Mheshimiwa Waziri katika bajeti yake ameeleza pia jinsi ambavyo wana mpango wa kuwezesha Jeshi la Polisi Makao Makuu kwa kuwanunulia vifaa vya kisasa. Ushauri wangu wasiishie pia Makao Makuu tu, waende mpaka kwenye mikoa, waende mpaka kwenye Wilaya hivyo vifaa viwezeshwe kwenye maeneo hayo ili Jeshi la Polisi wakishirikiana na TCRA na Ofisi ya Mashtaka wawe kwenye sehemu moja, washughulike na jambo hilo tu, wataalamu wachukuliwe kutoka maeneo hayo kama ni Jeshi letu la Polisi, wachukuliwe hao wataalamu wanaohusika na masuala ya cyber crime wachukuliwe na wenzetu wa TCRA wakiwa na mitambo yao wasimamiwe na sehemu moja ili wafanye kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mwananchi akipitia kwenye matatizo hayo, ataenda polisi, lakini polisi wataenda TCRA mpaka waje kwa pamoja waweze kulitatua makosa mengine yanakuwa yameshajitokeza na muda unakuwa umeenda, anakuwa hajashughulikiwa kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wewe una nia njema kununua hivi vifaa kwa Jeshi la Polisi, lakini sasa wangekaa sehemu moja ingekuwa rahisi zaidi ili waweze ku-solve mapema makosa ya kimtandao. Kwa kweli yanadhalilisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta wana-hack simu ya mtu, wanaanza kuomba fedha, wanasema mimi fulani nimepata matatizo watu wanaanza kutuma pesa mpaka waje wachukuliwe hatua muda unakuwa umeenda. Kwa hiyo, mkiwaweka kwenye single source ya kuwahudumia inaweza ikasaidia sana, hili mlifanyie kazi, lakini ikiwapendeza kama Serikali muone jinsi ya kuwaweka pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka kushauri siku ya leo ni suala la vipimo vya bundle. Kwa hali ilivyo sasa hivi mitandao ya simu iwe ni Airtel, iwe Vodacom na mitandao mingine yote wanaoamua na kusema kwamba umetumia hilo bundle ni mtandao husika. Mimi ushauri wangu Mheshimiwa Waziri pawepo na center ya kupima, pawepo na taasisi ya kupima matumizi na haya malalamiko ya wananchi dhidi ya mitandao na matumizi ya bundle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mimi natumia kampuni ya Airtel nitaweka bundle la shilingi 5,000 sijatumia vizuri utasikia ni matumizi yako tu lakini naenda kulalamika kwa nani? Nani anakwenda kuona kwamba kati ya mtandao wa simu na mimi customer wao ni nani ambaye amedhulumiwa?

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninadhani kupitia mitandao ya simu mkae chini na TCRA muone ni vifaa gani vitatumika kupima matumizi hayo badala ya kuwaachia mtandao husika ndio useme kwamba huyu mtumiaji alitumia hili bundle kwa matumizi yake, wakati mwingine mtu anaweka bundle hata hajawasha simu tayari bundle limeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mnafanya kazi nzuri hebu mliangalie hili limekuwa likizua malalamiko mengi na matumizi ya bundle na mawasiliano kwa Taifa letu tumeona tuna laini zaidi ya line ambazo zimesajiliwa. Laini za bundle ni kama milioni 49 za simu kama milioni 90 sisi tuko milioni 60 watumiaji ni wengi. Ninadhani tunahitaji control mechanism ya kuhakikisha hawa customers hawaonewi na mtandao wa simu usiwe ni hakimu mwenyewe akajijaji mwenyewe wakati kuna malalamiko mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya bundle hizi na mawasiliano kwa nchi yetu ilipofika na kwa maendeleo tuliyonayo hayaepukiki. Kuna mtu kila siku lazima aingie internet, kuna mtu kila siku lazima awasiliane. Kwa hiyo, mkiweka control mechanism ya matumizi haya mtakuwa mmefuta kilio cha Watanzania wengi ambao wamekuwa wakionewa katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)