Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Kwanza kabisa, nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ndani ya Wizara hii na nikipata reflection ya kazi nzuri ni ongezeko la bajeti ndani ya Wizara yetu hii tunaona mwaka 2024/2025 Wizara hii ilitengewa shilingi bilioni 180.9 lakini leo Wizara inaomba shilingi bilioni 291.5 tunaamini maono na malengo ya Mheshimiwa Rais yanaenda kutimia kupitia Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri Jerry Silaa ambaye ndiyo nahodha wa Wizara hii akimwakilisha Mheshimiwa Rais vizuri, lakini tunaona akisaidiwa na Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi na Katibu Mkuu, kaka yetu Mohammed Abdulla na Naibu Katibu Mkuu - Nicholaus Mkapa pamoja na wakurugenzi wote na watendaji wote ndani ya Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii kwa miaka hii ambapo imebadilishwa na kutengenezwa vizuri imefanya kazi kubwa katika maeneo yetu na Taifa kwa ujumla na baadhi ya maeneo ambayo tutashauri ili kuweza kuendelea kuboresha katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza mimi niombe kwanza niishauri Wizara, tumefanya kazi kubwa ya kuweka postcode katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu na kwa kweli zimewekwa alama mbalimbali katika maeneo yetu, lakini sasa hivi ukipita maeneo mengi hizo postcode zote ziliondolewa na ziliibiwa nafikiri kupitia vyuma chakavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tungeitaka Wizara kwa kazi nzuri ambayo ilifanyika kwa weledi mkubwa kuweza kuonesha mitaa yetu na kui-locate ili iweze kutambulika kirahisi, ni mkakati gani sasa mpya ambao Wizara yetu hii inakuja nao kuhakikisha sasa inarudisha uhalisia kama ambavyo kampeni kubwa na kazi kubwa imeweza kufanyika katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika mitaa mbalimbali utakuta kwa kweli vibao havipo. Sasa tungalie nchi nyingine mbona vibao vinakuwepo. Ukienda hapa Rwanda unakuta mitaa yote imekuwa addressed vizuri kwa postcode ambazo zipo. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri ninaamini kwa kazi nzuri unayoifanya utakuja na jibu la suluhisho hili ili sasa lengo la kitaifa ambalo lilikuwepo liweze kwenda vizuri na mitaa yetu iendelee kutambulika kwa postcode ambazo zimewekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili mimi ninaomba nipite katika falsafa ya Mheshimiwa Rais ya 4R, Mheshimiwa Rais alikuja na 4R na mimi nitaongelea “R” mbili tu; ya reform na rebuild. Hiyo falsafa ya Mheshimiwa Rais ameileta ili kurekebisha pale ambapo tutakuwa tunaona tunaenda vizuri na ambapo hatuendi vizuri tuweze kuparekebisha na pale ambapo pana mapungufu tuwe kujazia ili tuweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaona kwa nini Wabunge wengi wamechangia katia Sheria hii ya Electronic and Postal Communication ya mwaka 2010 mpaka 2022 ni kwa sababu tunaona kwamba, kuna eneo ambalo halikai vizuri. Mheshimiwa Rais ameshatupa room ya kupitia kwenye “R” hizi mbili to reform na rebuild ili kuweza kuweka pale kwenye mapungufu, kufanya masahihisho na kuweza kurudi kwenye mstari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wengi wamechangia katika mabadiliko ya sheria hii, lakini kwa sababu hii sheria ilitungwa kwa nia njema lakini matokeo yake yamekuwa ni tofauti. Sasa chombo chako hiki Bunge hili Tukufu kazi yake ni kurekebisha sheria pale ambapo inakuwa inaonekana haifanyi kazi vizuri. Sasa hatuna budi na tusiwe na kigugumizi kuhakikisha kwamba hii Sheria ya Electronics and Postal Communication ya mwaka 2022 inarekebishwa ili kuweza kuendana na hali ya kidunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia makampuni yote ambayo yalitakiwa yawe listed hayajawa listed lakini kampuni moja imekuwa listed, lakini imeweza kuleta hasara kwa wananchi wetu. Wananchi wakiuza hisa Taifa na lenyewe linapata pato la Taifa. Sasa tusione kwamba hapa ni wananchi wanaoumia peke yake, lakini hata Taifa letu linaumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana na Waziri akija hapa atuambie walivyojipanga kuhakikisha kwamba inaleta marejeo ya sheria hii iweze kurekebishwa ili wananchi wetu ambao sasa wamenunua hisa katika kampuni ambazo zimetajwa Vodacom na maeneo mengine ili waweze kurekebishiwa na waweze kuona jinsi gani wataweza kufidia hasara ambayo wameipata pia na Taifa letu liweze kupata pato kutokana na hizo hisa zikiuzwa au gharama yake ikiongezeka ili iwe faida kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine katika eneo hili nataka nishauri katika eneo la Mkongo wa Taifa. Tunaona kazi kubwa ambayo Taifa imefanya, tukirejea miaka ya nyuma hapo tulikuwa hatuwezi kuongelea hata Mkongo wa Taifa, lakini leo tunaweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuongelea Mkongo wa Taifa. Ni kwa sababu kazi kubwa na nzuri ambayo Mheshimiwa Rais wetu na Serikali yake na wasaidizi wake kupitia Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Naibu Waziri na wengine wamesaidia kuhakikisha kwamba hilo suala linatimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika matumizi ambayo ndani ya nchi yetu, Mheshimiwa Mabula pale alishauri, tunahitaji kuona consumption ya mkongo huu ndani ya nchi yetu unawafikia hata wananchi wangu wa kule Kitobo, wananchi wa huku Nkerenge na wenyewe waweze kutumia huo Mkongo wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, tunataka kuona ni jinsi gani Taifa letu sasa kwa kutumia hii fursa tulionayo imeweza kutanua na kuweza kuuza hii huduma nje ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kuwa na amani na utulivu inatupa nafasi ya kuwa soko zuri katika nchi zote zinazotuzunguka ziwe za East Africa au SADC ili kuweza kufanya biashara. Nilikuwa naangalia takwimu hapa nchi ya Uganda karibu 95% ya internet inapokea kutoka Kenya, lakini tunajua mahusiano mazuri ya Tanzania na Uganda, lakini tunaona kukua kwa mahitaji ya internet ndani ya nchi ya Uganda ni almost 25% kila mwaka. Kwa hiyo, bado nafasi ipo. Sasa tunatumia njia gani ya kuweza kushawishi wenzetu ambao tuna ujirani mwema nao iwe ni Uganda au nchi zingine kuweza kupeleka huduma hii na Taifa letu likapata pato?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe pia Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kuhitimisha atupe mpango mkakati ambao Wizara inayo ili kuweza kuhakikisha kwamba sasa huu mkongo wetu wa kitaifa unaweza kuingiza pato la Taifa letu na nchi yetu iweze kupata fedha na sisi tunahitaji vituo vya afya, tunahitaji zahanati, tunahitaji shule mpya na barabara ziendelee kuboreshwa kutokana na hilo pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine nilitaka kusimama hapa kushukuru kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Missenyi kwa kazi nzuri ambayo Wizara ya Mawasiliano imefanya, imejenga minara katika maeneo yetu katika vijiji tofauti. Niombe Mheshimiwa Waziri bado maeneo ya Kata ya Kashenya unajua sisi tunapakana na Uganda mara nyingi tunapata mtandao wa Uganda, lakini Kanyigo bado mtandao wa shida, Kata ya Bugandika bado ni shida, Kata ya Kitobo, Kilimile Mabaale bado ni shida na Minziro na Nsunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo tumeweza kufunga minara Kakindo tunakushukuru sana, Nkerenge tunashukuru, lakini Bwenko, Makule, Kakunyu na Buchurago hiyo minara wananchi wameipokea pamoja na Kakunyu eneo hilo kwa kweli sasa hivi kuna usikivu mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nikushukuru kwa nafasi na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)