Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye Wizara hii muhimu sana ya Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kujaribu kumshauri Mheshimiwa Waziri, nianze na hili suala la hisa na Sheria ya Kielektroniki na Mawasiliano ya Posta (The Electronic and Postal Communications).
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchokisema Wabunge wenzangu, sisi hatuombi hisani ya Serikali, wananchi warudishiwe pesa zao. Tunaitaka Serikali iingilie kati changamoto ambayo wao wenyewe kama Serikali wameisababisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivyo kwa sababu moja; sheria hii imefanyiwa marekebisho kuanzia 2010, 2017 na 2022. Ukisoma kifungu cha 26 cha sheria kinasema watoa huduma wote wa mawasiliano ni lazima wahakikishe wanauza 25% ya share zao kwa umma na ikaenda mbele zaidi ikatoa mpaka deadline, ikasema ndani ya miaka miwili baada ya sheria hii kusainiwa ni lazima wawe wameuza share zao kwa umma. Wakatoka hapo wakatoa mpaka na adhabu kwa wale ambao hawatafanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mashirika yanaweza yakashindana na Serikali? Walifuata kile ambacho Serikali ilitaka. Vodacom akaenda kuuza share kwa umma na wananchi kwa sababu hawakulindwa na hawakupewa elimu, walienda kununua zile share na wamenunua share wamepata hasara. Tatizo hili kalisababisha nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi wa Shinyanga hajui hata ofisi za Vodacom zinazouza hisa ziko wapi, mwananchi wa Katavi hajui ofisi za share za Vodacom zinakouzwa. Yeye alienda benki, akakopa hela akanunua kwa sababu alijua Serikali ipo inamlinda na itamsimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea billions of moneys. Tunawaongelea Watanzania maskini ambao wameathiriwa na sheria hii. Kukiri kosa siyo udhaifu. Tulitunga sheria ambayo leo imesababisha hasara kubwa na hata Serikali yenyewe inakiri. Walisema kampuni zote za mawasiliano, watoa huduma siyo Vodacom na Tigo peke yake. Wale wanaouza fiber, sijui data na nini, wote wanatakiwa wahakikishe wanauza shares zao 25% kwa umma. Wamefanya Vodacom peke yao. Serikali imefanya nini kwenye hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sheria haitekelezeki, kurudi nyuma siyo kukiri udhaifu. Tunataka Serikali iingilie kati na leo hii mimi ninawajua wengi na wengine ni Wabunge wako humu ndani wamenunua hisa za shilingi milioni 20, lakini leo wakienda kule hisa haziuziki wanalipwa shilingi milioni nane; shilingi milioni 12 ni hasara. Hilo ndilo lilikuwa lengo la Serikali kufilisi watu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ni lazima iingilie kati kama mtu wa katikati kati ya mwananchi na hii kampuni ya Vodacom ambayo imeuza shares zake ambazo leo zimedorora na wananchi wamepata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema kwamba suala hili tuwaachie Vodacom na wananchi ndiyo hivyo hisa za shilingi milioni 20 mtu analipwa shilingi milioni nane. Amewekeza kwa miaka, ana madeni, ana riba na ana marejesho. Hela hizo za kuongezea atazitoa wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaishauri Serikali na siyo kwa mara ya kwanza, tukubaliane tu, makosa yalifanyika. Siku zote kwenye maeneo ya biashara market force ndiyo inaamua mtu akauze shares. Mimi nimefungua kampuni yangu ya private, ninafanya biashara, ninataka niongeze mtaji, zipo njia nyingi. Ninaweza nikaenda kuchukua mkopo lakini pia ninaweza nikaigeuza kampuni yangu kutokana na sheria za kampuni ikawa kampuni ya umma nikauza shares kwa watu na nikapata mtaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kampuni zilishinikizwa na Serikali ikwenda kuuza share kwa public kwa sheria ya mwaka 2022. Ni lazima Serikali i-take responsibility kwa kuingilia kati hizi billions of moneys za Watanzania. Walipwe na tena walipwe siyo tu, wanasema ni lazima wafanyiwe indemnification. Walipwe na walipwe na pale ambapo wamepoteza ili kusudi next time kosa kama hili lisijirudie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulifafanua vizuri suala hilo ningeomba niongelee suala la wizi wa mitandaoni na huduma za hzi kampuni za simu. Hata wewe mwenyewe na Mheshimiwa Spika ni mashahidi. Sisi ambao tuko kwenye mitandao tunaona kila siku namna ambavyo majina yetu yanatumika vibaya. Watu wanatapeliwa tuna kwenye namba hii na watu wanatapeliwa fanya hiki. Sasa hivi tumekwenda mbali na hii akili mnemba, yaani mtu anaweza akajiita Salome na akafanya jambo ni ikaonekana nimefanya mimi. Tunayo Wizara, tumetunga sheria hapa za mitandao, kwa nini jambo hili halifiki mwisho na kwa nini halisimamiwi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwenye uchaguzi, unaweza ukashangaa wewe mwenyewe Mheshimiwa Jerry mtu anatuma message kupitia akili mnemba anasema mimi Jerry Silaa sigombei na hiyo ni a night before voting. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yametokea kwenye nchi za wenzetu, ni lazima tudhibiti immediately haya mambo ya wizi na utapeli wa mitandaoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, short of that tunaliingiza Taifa kwenye mazingira ambayo kila mtu hayuko salama na mimi ni champion wa kuhakikisha kwamba tunapata mwongozo, sheria na taratibu nzuri inayodhibiti matumizi mabaya ya akili mnemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto kubwa na hili ningeomba tu Mheshimiwa Waziri atoe mwongozo, unapokuwa umetuma pesa kupitia mtandao ikatokea fedha zile hazijaenda zile fedha zitarudishwa, lakini ile ada iliyotumika kutuma ule muamala haitokaa irudishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni fedha kidogo, shilingi 500, shilingi 1,000 au shilingi 1,200 lakini hizo fedha kidogo ndizo zinakuwa nyingi. Sisi tunaitaka Serikali itulinde sisi walaji. Ninatamani sana tulisimamie hilo na fedha za watu ziweze kurejeshwa pale ambapo inatokea muamala haujafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nichangie kuhusu Mkongo wa Taifa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamesema vizuri sana. Mkongo wa Taifa ni uwekezaji mkubwa na kwa East Africa pengine sisi ndiyo tumefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye Mkongo wa Taifa. Ni kwa vile jambo hili halionekani kwa macho, lakini kwa uwekezaji huu, nimeisoma vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri, haelezi mahitaji ya zinazoizunguka Tanzania kwenye Mkongo huu wa Taifa ni kiasi gani, hajatueleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama haitoshi sisi tumeuza kwa kiasi gani bishaa hii, kwa sababu hizi fedha ni za Watanzania. Mwisho wa siku hii ni biashara ni lazima iuzwe na ni lazima tupate return n ani lazima sisi kama nchi tunufaike kwa sababu mwisho wa siku ni suala la biashara. Usipokwenda ndani ya muda utajikuta unapata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)