Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, sauti yangi sio nzuri lakini mtanivumilia na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaunga mkono hoja, lakini naomba nitumie jukwaa hili kuwapa pole wananchi wa Kata ya Lukalasi katika Kijiji kile cha Maliba wananchi watatu waliingia kwenye mgodi bahati mbaya wakabomokewa na gema, kwa hiyo, wamekaa ndani siku tisa na wawili wamepatikana usiku wa kuamkia leo wakiwa tayari wamefariki, bado wanamtafuta mmoja.
Kwa hiyo, ninawapa pole sana wananchi wa Kata ya Lukalasi. Tunajua wananchi hawa walikuwa wanaenda kujitafutia kipato, lakini limewakuta hilo janga. Mwenyezi Mungu azipokee roho za marehemu mahala pema peponi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niishukuru sana Wziara hii, Nimshukuru Mheshimiwa Jerry Silaa lakini nimshukuru Naibu Waziri na wataalamu wote katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mimi ninaingia jimboni kwangu tulikuwa na shida sana ya mawasiliano, kata 16 zote zilikuwa hatupati mawasiliano. Ukipata mawasiliano basi ni yale ya kubahatisha bahatisha ama ukae kwenye mti au ujiegemeze sehemu fulani, lakini nikushukuru sana Mheshimiwa Jerry umefika hapa kupitia ile miradi ya ujenzi wa minara, leo hii kata zote tunapata mawasiliano vizuri, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru pale Sala ujenzi wa mnara umekamilika, pale Kihangimauka ni kilometa 15 tu ulikuwa unatoka Mbinga Mjini tulikuwa hatupati mawasiliano; kilometa 15 tu. Leo hii tayari mnara umekamilika wananchi wanapiga simu wanafurahia mawasiliano, lakini ukienda katani kwangu mwenyewe nilikuwa ninapata shida leo hii Tigo, Vodacom, Airtel, na Halotel wapo, mitandao minne, kwa kweli tunakushukuru sana. Ukienda Kata ya Kitura ni hivyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua jimbo lile lina milima, kwa hiyo, ilikuwa shida sana kufanya connection, lakini kazi kubwa imefanyika. Nikupongeze sana wewe na nimpongeze Naibu Waziri, lakini pia niwapongeze wataalamu wako, wataalamu wale wa kanda ni wasikivu sana, ukiwaambia wanakwenda mara moja wanachukua hatua. Sasa hivi tulikuwa na shida ya internet wameenda wameongeza uwezo wa internet baadhi ya maeneo tunapata ile 4G na bado 2 na E, lakini ninajua mko mbioni kuongeza kasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili linalosemwa hapa la mkongo ninajua umefika Mbinga, sasa haujasambaa. Ninaomba sana sasa uende kwa kasi. Sisi Wana-Mbinga tunapenda ku-google. Tunapenda kutafuta bei ya mazao na unajua sisi ni wakulima sana. Kwa hiyo, ninaomba sana kupitia hiyo endeleeni kupeleka huko, lakini kiujumla ninashukuru sana. Sasa hivi zile kata ambazo zilikuwa na shida kama utakosa mtandao fulani basi wa pili lazima uupate, sasa hivi hatuna shida kiasi kile. Kwa hiyo, ni kazi kubwa na nzuri imefanyika. Hongera sana Waziri na timu yako kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine na mimi nimepatwa na butwaa hapa kidogo kwenye hili jambo ambalo linasemwa la suala la uwekezaji wa Vodacom. Ni kweli na Mheshimiwa Kiswaga ametoa taarifa hapa kwa Mheshimiwa Mabula, biashara ya hisa ina kupanda na kushuka. Ni kweli kabisa Mheshimiwa Mabula alisema mimi ninaongea kienyeji na ni kweli kabisa, Watanzania wengi hawako kwenye hizi biashara, ni mambo ambayo watu wanajifunza baada ya kusikia huko duniani watu wamefanya biashara ya hisa wakatajirika na Watanzania sasa wanataka kujiingiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachosema hapa ni kuona hasara waliyopata Watanzania hawa tuwasaidie. Ni ukweli kabisa kwamba ukiwekeza kwenye hisa kuna kupata faida na kuna kuporomoka. Kwa hiyo, Wtanzania hawa hata tulipoanzisha mfumo huu wa kununua vipande vya Umoja, kuna Watanzania walienda wakakopa kwenye benki. Bahati nzuri Serikali ilifanya jambo moja zuri sana, vipande hivi vya Umoja vilikuwa vinauzwa kwa shilingi 70 na Serikali ilikuwa ina-top up shilingi 30 kujaribu kuwahamasisha Watanzania hawa waweze kuingia kwenye hii biashara. Unaona kitu kama hicho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo inafanya vizuri, hii biashara ni nzuri sana na pale ambapo inafanya vibaya ndio yanatokea mambo kama haya.
Kwa hiyo, ombi langu mimi hapa na ombi la hawa Watazania walioingia kwenye hii biashara kuomba huruma ya Serikali. Nini kifanyike ili hii hela iliyowekezwa pale ikalala iweze kuwakomboa. Kama mfano alioutoa Mheshimiwa Mabula pale, mtu kaenda kukopa shilingi milioni 60, akaenda kuwekeza kwa nia kwamba angepata faida. Bahati mbaya ile hela iko kule imezama na ikizama haimsaidii yule Vodacom na haimsaidii huyu aliyewekeza. Sasa ina maana gani? Hela imekaa tu pale imelala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni bora Mheshimiwa Waziri haya mambo yanawezekana. Kama kuna loophole ya kukaa chini na initial owners mkafanya resolution ya aina yoyote ile ili kuwasaidia hawa watu lingekuwa jambo bora sana kwa nchi yetu. Mimi ninajua nia njema ya Serikali ni kutaka kuwafanya Watanzanua waone huu uchumi na ni kitu kizuri sana, lakini sasa tumefika sehemu tumekwama. Tuendelee kukaa tu hivi hivi tukwame? Hapana, ni lazima tuwasaidie Watanzania hawa mwisho wa siku nchi iende.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kile hii Vodacom ilikuwa iko juu sana, yaani siyo uongo ilikuwa inafanya vizuri sana na ndiyo maana unaona hisa moja iliuzwa shilingi 850. Katika bei hizi za hisa ukiona kampuni inauza hisa kwa shilingi 800 naa ujue iko kwenye nanihii kubwa sana. Kwa hiyo, kwa kadiri inavyokwenda tulitarajia baada ya mwaka au baada ya nini, hisa ipande ifike hata shilingi 1,000 au 2,000 lakini sasa imeenda inashuka, maana yake ni kitu ambacho siyo cha kawaida. Kwa nini? Kwa sababu kampuni haijafanya vizuri. Sasa kama haijafanya vizuri kuna namna ya kuifanya kampuni iweze kuongeza, halafu ifanye vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, njia moja ya kufanya ni kufanya resolution, wafanye resolution na Waziri yuko kwenye nafasi ya kuwasaidia hawa waliokuja wakanunua na wale initial owners ili kufanya hiyo resolution na mwisho wa siku Vodacom iweze kusimama kama kampuni nyingine. Mbona Tigo hawajaingia na mbona wale wengine hawajaingia? Ili sasa wote wawe kwenye nanihii moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nzuri ni lazima i-practise kwa wote, sheria inayo-practise upande mmoja haifai, yaani kwa nini muibane Vodacom tu, kwa nini isiwabane na wale wengine kule? Sheria ili iwe nzuri, wote wawe sawa kwa sababu wote hawa ni competitors, Wote wawe kwenye level moja.
Mimi ombo langu, wewe Mheshimiwa Waziri ni wakili msomi, unayajua haya mambo, ni kweli kabisa his ani biashara ipo lakini inawezekana ikauzwa na inawezekana tukafanya resolution mkakubaliana nini kifanyike kati ya wawekezaji hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niombe sana, tafuta huo mwanya muweze kuwasaidia Watanzania hawa. Watanzania hawa ni maskini mno, wameambiwa tu ukiwekeza unapata faida. Sasa bahati mbaya wamewekeza wamepata hasara. Tuwasaidie waokoe hata kidogo kilichobaki huko wafanye mambo mengine.
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umeisha?
MWENYEKITI: Kengele imelia.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja.