Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipa muda mchache huu kuchangia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri kwa namna ambavyo kwa muda mfupi toka amekwenda kwenye Wizara hii lakini tumeona namna ambavyo amekuwa na juhudi za juu kabisa kuhakikisha kwamba yeye na wasaidizi wake Wizara inazidi kuwa imara kwa sababu kwa wakati tulionao ni wakati wa kiteknolojia, ni wakati wa kidigitali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaamini kwamba Wizara yako ikifanya vizuri sana ndivyo Taifa letu litakavyoendelea kuboreka zaidi na kama unavyofahamu hata kukusanya mapato hivi sasa nchi nzima kwa kweli kuna wakati tunakoelekea matumizi hata ya fedha za mfukoni yanaendelea kupungua sana. (Makofi)
Kwa hiyo, nikupongeze sana Mheshimiwa Jerry na kabla sijaendelea nikutakie kila la kheri, sijui ni Ukonga sijui ni Kivule, lakini tunaaamini wewe ni mtu muhimu sana na bado tunakuhitaji kwenye jengo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze pia Naibu Waziri Maryprisca kwa kuendelea kukusaidia, Katibu Mkuu na menejimenti nzima ya Wizara yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba nianzie pale ambapo ameishia Mheshimiwa Ulenge na sisi tunatoka kwenye mikoa na majimbo ya wafanyabishara wengi tumepata changamoto sana kwenye hili jambo ambalo limezungumzwa na karibia kila mmoja hapa juu ya makampuni ya simu kuji-register kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niongee kienyeji kabisa kama vile ambavyo wapiga kura wetu wanatupigia simu na kuongea kienyeji kabisa. Ukiruhusu kwenye jumba hili kila Mbunge aseme wako Wabunge wa kutosha sana humu ambao wananung’unika kama mmojawapo Mheshimiwa Kanyasu na hawawezi kusema kwa wingi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ilifanya kwa nia njema sana mwaka 2017 kuhakikisha kwamba tunaangalia namna bora ya kuendelea kuboresha maisha ya Watanzania wenzetu kwa kutunga sheria ambayo ilielekeza na ikatoa mwanya kwa makampuni kuji-register kwenye soko la hisa na wenzetu wa kampuni mojawapo ya simu ya Vodacom wao wakawa sharp zaidi na huu u-sharp walioutumia haukuwa ni mbaya ulikuwa ni u-sharp wa kibiashara kutokana na sheria tuliyopitisha ingewezekana ikawapa ahueni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu walifuatwa mpaka kwenye makazi yao, walifuatwa mpaka kwenye maofisi kule nje, wakashawishika kwamba inawezekana ukinunua hisa leo za shilingi kadhaa kwa kipande cha shilingi 850 inawezekana baada ya miezi sita ukauza hisa hizo kwa shilingi 4,000 na kadhalika na watu wakaenda mpaka mabenki wakakopa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninao ushahidi wa wananchi kutoka Ukerewe, kutoka Ilemela, kutoka Nyamagana, mmoja tu alikuwa ananiambia kila siku ananipigia simu na Mheshimiwa Waziri nilituma hizi message kwako mara kadhaa kwamba mimi nimeenda kukopa benki shilingi milioni 60 mwaka 2017, fedha hii nikaenda kuwekeza, nikanunua vipande vyangu 70,600. Nikawekeza nikitegemea kila baada ya mwaka au kila baada ya miezi kadhaa nitapata gawio langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha sana na ndiyo maana nimesema niongee kienyeji kabisa, toka amewekeza ile fedha shilingi milioni 60 gawio lake la kwanza amelipata mwaka 2024 kwa shilingi 11 kwa share kiasi cha shilingi 700,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtu kama huyu ameuziwa nyumba leo anaishi kwenye nyumba ya kupanga. Nataka tulichukue hili kama sisi tuone Mheshimiwa Waziri likuingie ili uone namna ambavyo tunaweza tukafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wengi wa namna hii, sasa tuamue jambo moja, sisi ndiyo tunatunga sheria Mheshimiwa Waziri turudi humu ndani tutakaporudi, sheria hii tuiangalie na tuifanyie marekebisho na tutakapoifanyia marekebisho tuamue mambo yafuatayo; aidha, tuamue kurejesha fedha za watu na faida au tuamue vinginevyo iliwatu wetu hawa wanaoteseka na nia yao njema ya kuwekeza waweze kupata unafuu wa maisha. Leo ukimuuliza Mheshimiwa Kanyasu hapa… (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa ya Mheshimiwa Kiswaga.
TAARIFA
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana mchangiaji anachangia vizuri, lakini hapa tusimwingize matatizoni Waziri; moja, kwamba unajua hisa huwa inapanda na kushuka, inawezekana umeweka hapa laki mbili baada ya miaka miwili hela yako ikawa 40,000 inategemeana na hisa inavyopanda. Sasa unapomwambia Waziri aende akaiambie Vodacom au kampuni fulani siyo kwamba naitetea Vodacom lakini naelezea biashara ya hisa ilivyo.
Kwa hiyo, tusimwingize Waziri matatizoni hapa, kama ni suala la kubadilisha sheria tutabadilisha, lakini siyo suala la kusema alipwe na faida, atalipwa na faida kutoka wapi? Kwa sababu hisa kama imeshuka utalipwaje na faida, ahsante sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Stanslaus Mabula unaipokea hiyo taarifa?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana Mheshimiwa Kiswaga, mimi ninafahamu huyu amekuwa... any way nisiende huko hoja yake siipokei. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachojaribu kusema Mheshimiwa Kingu alieleza vizuri sana kwa details kwa nini tulifikia hapa na mimi nimetaka kusema niongee kienyeji sana ili nieleweka na walionituma. Ningeweza kwenda kwa utaratibu mwingine kabisa, lakini ninachotaka kusema Mheshimiwa Waziri ndiyo amebeba Wizara hii. Wizara ya Mawasiliano ndiyo mama mlezi wa makampuni yote ya simu Tanzania, sasa anataka mimi niondoke hapa nikalalamikie kampuni la simu nyumbani kwake, haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaeleza changamoto wanazozipata wananchi na sisi Wabunge miongoni mwetu tumeingia kwenye hili jambo, tumenunua hisa mwaka 2017 leo miaka minane, utaratibu gani unafanyika. Ninachotaka Serikali iingilie kati kujaribu kusaidia wananchi, it’s over, nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili Mheshimiwa Waziri tunao mradi wa Mkongo wa Taifa; Mkongo wa Taifa wengi tunapenda kuuita ni SGR nyingine na Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana umeeleza vizuri kwenye mafanikio tuliyonayo. Sasa hivi tuko takribani wilaya 109 ambazo zimeshafikiwa na Mkongo wa Taifa, lakini malengo yetu ni kufikia wilaya zote nchini. Sasa Mheshimiwa Waziri tunazifikia wilaya kwa kiwango gani? Je, tunafika tu makao makuu ya wilaya tunaacha tunaondoka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitamani Mheshimiwa Waziri kuna maeneo bado hatujafanya vizuri sana kwenye matumizi mazima ya usambazaji wa Mkongo wa Taifa na Mheshimiwa Waziri hapa tu kwa kuokoa muda labda tufahamu kwanza uwezo wetu tulionao wa ndani na tunasambaza mkongo huu tumeshauzambaza asilimia ulizozitaja Mheshimiwa Waziri karibia 40% nadhani bado ni kidogo sana kulinganisha na uhitaji tulionao. Kwa mafano umesema maeneo ya wazi 50 peke yake. Je, ni kweli ukiona maeneo ya Waziri nchi hii kwenye miji mikubwa tu ukichukua Dar es Salaam peke yake unaweza kumaliza hayo maeneo 50, hujaja Mwanza, hujaenda Tanga, hujaenda Mbeya, hujaja Dodoma na sehemu zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninachotaka kusema nikuombe Mheshimiwa Waziri kupitia wewe mwenyewe na timu yako nzima unao wataalamu wa kutosha, hebu tujikite kwa nguvu zote tulizonazo hii biashara wamesema hapa wenzangu. Kwa nini tunakwama? Kwa nini mpaka leo usafiri na SGR kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma hapa kuna maeneo katikati unapoteza kabisa mawasiliano, lakini unaenda kwenye kituo cha stesheni kimoja nimekaa juzi nisikitaje jina nimekaa karibia masaa mawili nasubiri treni hata pale penyewe tumeshindwa kufunga mkongo wa mawasiliano ili angalau tunapata internet muda wote. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu suala la kibiashara hebu tulitazame kiukweli kabisa tuone hapa nchini kwetu uwezo wetu wa usambazaji na uzalishaji wetu unafanana na huko tunakopeleka nje? Huko tunakowapelekea nje wako tayari au hawako tayari na kama hawapo tayari sisi tumechukua initiatives gani au ndiyo easy tu leo tunataka tukifika pale border tumemaliza, lakini ukienda Congo wanatuhitaji sana, ukienda Rwanda wanatuhitaji sana, ukienda Burundi wanatuhitaji sana, Kenya wenyewe wanatuhitaji sana kuliko chochote kile kupitia mkongo huu. Kwa hiyo, ninakuomba leo tulitamani sana, hata Dar es Salaam yenyewe tunayoizungumza ingekua imejaa Mkongo wa Taifa kila sehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo viko vikampuni vya simu vimekuja vinaanza kuteka baadhi ya maeneo. Mheshimiwa Waziri utajikuta wewe kwa sababu hii ni biashara tena unaanza kutoa bure na hii sio biashara ya bure tulitegemea...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: ... kila sehemu mimi nikisimama hata pale Nyerere Square ninaweza kukaa nikaangalia kwenye internet nikakutana na internet ya Mkongo wa Taifa nikajaza pale nikachati kwa muda mrefu na gharama nafuu kabisa ambayo nitakayoifanya.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri na nikutakie kila la heri na ninaamini kwamba utakapokuja ku-wind up utatupa majibu ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninakutakia kila la heri Mheshimiwa Waziri Mwenyezi Mungu akutangulie. (Makofi)