Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambayo kimsingi ni Wizara muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani na pongezi nyingi tumezitoa, lakini tuna mpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo alikuwa na maono makubwa katika Wizara hii na ndiyo maana aliipunguzia mzigo akaitoa Wizara ya Habari akaiweka sehemu nyingine akaiacha Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa sababu ni kitu ambacho Waziri ata-focus kuhakikisha kwamba anaisaidia nchi katika sekta hii muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii inachochoea shughuli zingine za uchumi katika nchi yetu. Kwa mfano watu wa fedha kwenye mambo ya transaction wanategemea sana Wizara hii, kama nilivyosema mawasiliano ya simu yanategemea sana Wizara hii, lakini kama haitoshi tumeona hata ajira nyingi zikisimamiwa vizuri zitatokana na Wizara hii ambayo inawagusa zaidi vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia maeneo machache sana, kwanza nitachangia Mradi wa Tanzania Kidigitali. Mradi huu tulivyojulishwa kwenye Kamati pamoja na taarifa iliyosomwa hapa ni kwamba tuliambiwa umefikia 78% kwa maana ya utekelezaji wake na fedha zimetoka hazina matatizo yoyote, mradi unakwenda vizuri na tunaendelea kusema tu kwamba mradi huu uendelee kusimamiwa na Wizara na tuendelee kuhakikisha kwamba lengo la kuunganisha taasisi zote zisomane ndiyo lilikuwa lengo la Mheshimiwa Rais kwamba kupitia mfumo huu au mradi huu itasaidia taasisi zetu kusomana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia zaidi ya taasisi 100 kwa maana ya Bara pamoja na Visiwani, wote kwa maana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tayari taasisi 100 zimeshafikiwa na mradi huu na zimeanza kusomana. Hii ni kazi kubwa sana, nikupongeze Waziri, Mheshimiwa Jerry Silaa kwa kusimamia kazi hii nzuri ambayo inaenda kutupa heshima kama nchi na haya yalikuwa maagizo ya Mheshimiwa Rais mwenyewe kuhakikisha kwamba mifumo inasomana na huu ndiyo mwelekeo wa kwenda kwenye e-card kwamba sasa tuachane na mtu kuwa na kadi nyingi mpaka zinavimbisha suruali kumbe ni kadi huna fedha, una kadi nyingi mara NHIF, sijui una leseni, mara sijui una kitambulisho cha mpiga kura, mara wale wapenzi wa mpira una kadi ya kwenda kuchanja kwenye mpira, yaani unakuwa na lidude kubwa kumbe hata fedha hamna, umejaza kadi nyingi ambazo kimsingi ikipatikana e-card itasaidia sana kuondokana na changamoto ambayo tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nikuombe sana, endelea na kazi hii kuhakikisha kwamba mradi huu mkubwa wa Serikali wa Tanzania Kidigitali unaenda kukamilika na kuhakikisha kwamba Tanzania inaendelea kuwa mfano wa nchi zingine katika Afrika pamoja na dunia, lakini itasaidia sana kupunguza watu kulipa kwa cash, itakuwa cashless, sasa watu watakuwa hawatumii fedha cash katika kununua maeneo mbalimbali, lakini zaidi ya hapo itasaidia ukusanyaji wa kodi, kwa sababu kila transaction itapita kwenye mfumo wa ki-electronic itasaidia kujua nani amepata mapato gani na mwisho wa siku ni rahisi hata TRA na watu wanaohusika na kodi kuweza kukusanya kirahisi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sekta hii au Wizara hii ni muhimu sana. Mheshimiwa Waziri, nikuombe nenda ukasimamie na tuhakikishe kwamba tunafikia malengo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni eneo hili la vituo vya umahiri vya kuwajengea vijana wetu uwezo ambavyo tumesikia hapa kwamba vijana wetu kwa maana ya hizi kampuni ndogo ndogo za startups ambazo tunaamini zikijengewa uwezo zitawafanya vijana wengi waingie kwenye ajira na nikupongeze sana mwaka huu tulipokuwa pale Arusha mliweza kutoa hata tuzo kwa vijana wabunifu wa Tanzania ambao kwa kweli wengine walikuwa hawaamini mpaka walilia wakati wanapewa na kutambuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lile endelea nalo kwenye mikoa yote, isiwe eneo moja Dar es Salaam na Arusha, nenda mikoa yote Tanzania, vijana wabunifu wapo, tuwajengee uwezo na tuweze kuwatia moyo na nimefurahi sana kuna baadhi ya maeneo mliwapa hadi mtaji, yaani kwamba kijana ameanzisha bunifu yake, hana uwezo wa fedha mnampa fedha ili aweze kukuza bunifu yake na mwisho wa siku anaenda kuajiri vijana wengine. Pia hii itapunguza vijana kubaki kwenye mambo ya betting na mambo kama hayo kwa sababu watakuwa na kazi kamili ya kufanya na vijana wetu wengi wana uwezo mkubwa kwenye sekta hii ya ICT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana uendelee kuwalea kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata fursa hii ambayo kimsingi Rais amesema Wizara yako ikisimamiwa vizuri itasaidia sana kuleta ajira nyingi kama ambavyo tumesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema vile vituo viongezewe kasi viweze kukamilika ili vijana wetu waweze kupelekwa kule kwa ajili ya training, lakini siyo vijana tu hata watu wazima ambao wana shughuli zao zingine wanaweza kwenda kujifunza pale na kuweza kupata uwezo mzuri zaidi wa kutumia ICT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni suala la kupongeza, minara 758 kazi inaenda vizuri, tumepata taarifa kwenye Kamati na mimi binafsi katika Jimbo la Singida Mashariki nimepata minara miwili imeshakamilika kule Misughaa pamoja na pale Lighwa, wananchi sasa hivi wana-beep hata wakiwa chumbani ndani, wanaweza kuwasiliana kokote walipo, zamani ilikuwa mpaka mtu aende juu ya mti, anaenda anatafuta mawasiliano, hii ilikuwa ni hatari sana wengine wanagonjwa na nyoka katika maeneo yale, lakini leo wanapata mawasiliano ya moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupongeze sana, nani kushukuru kwa kumleta Mheshimiwa Naibu Waziri pale kwenye jimbo langu, pale Matare ule mnara umefikia karibu 80% unaenda kukamilika, watu wangu wa Jimbo la Singida Mashariki ambayo ni Ikungi Mashariki wanaenda kupata mawasiliano yale ambayo yalikuwa hayapatikani kwa sababu hata kuna vijana walikuwa wanachelewa kuoa kwa sababu hawawezi hata kuwapigia simu wapenzi wao. (Makofi)

Kwa hiyo, ninaamini kupitia hili litasaidia sana na Mheshimiwa Naibu Waziri rudi mlete Waziri muje mzindue ile minara kuonesha kwamba kazi kubwa ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanyika vizuri katika Jimbo la Ikungi Mashariki katika sekta ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kule Mang’onyi ule mnara ambao ulikuwa unaendelea msukumeni mkandarsi aweze kumaliza na kule Mang’onyi kuna mambo ya uchumi mkubwa wa madini, niombe sana mkaboreshe mawasiliano ili kuondokana na tatizo la kiusalama katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye eneo hili la hii sheria ambayo tulikuwa tunaambiwa hapa, ni Sheria ya Electronic and Postal Communication Act ya mwaka 2010. Sheria hii ni vizuri mkaingalia, imefanyiwa marekebisho mwaka 2010 lakini baadaye ilifanyiwa marekebisho mengine mwaka 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachojiuliza ni kwamba kama tulikubaliana mashirika au watoa huduma wote waingie kwenye soko la hisa, kwa nini awe ni mtuy mmoja Vodacom aliingia na yeye akatii maagizo ya sheria hii? Wengine bado wanatoa sababu ndogo ndogo ambazo zingine hazina mashiko, lakini kama ninavyosema tunaangalia hawa wahanga waliopata shida na Mheshimiwa Kanyasu ameeleza yeye ni mmojawapo wa wahanga ameweza kupeleka pale hisa zake na bado akitaka kuomba hizo kwa maana aende akauze, anasema haziuziki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu hatuwezi kuuita kama ni utapeli, hatuwezi kuita ni jambo gani, lakini ni jambo lina ukakasi. Mimi niombe sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais ana nia njema na nchi hii Watanzania wake hawa wamewekeza mle hamna sababu tuwaangalia kwa jicho la huruma. Mheshimiwa Sanga nilikaa kule kwa akina Mapembelo ni watu wazuri wa uwekezaji kama wanalia namna ile nani atawekeza kwenye nchi yetu?

Kwa hiyo niombe sana mliangalie siyo vibaya sheria ikitoka ikawa haitekelezeki basi turudi tena tuiangalie, si udhaifu ni kuendelea kujiimarisha na kuifanya Tanzania iwe salama kwa ajili ya wananchi kuishi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema nimalizie kidogo kwamba Mheshimiwa Kanyasu ananiambia kwamba hata wale watoa huduma kwa maana ya wakala wanaeza kuwa barabarani tu wanapata zaidi ya faida milioni tano mpaka kumi kwa mwaka, lakini kama huyu ambaye ametoa hela nyingi kwenye soko la hisa ambayo linauzwa kila siku mpaka huko duniani leo hii anashindwa kupanda anapata shilingi 200 kweli kwa mwaka kwa miaka nane? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sasa kama wanasema wenyewe wataalamu wa biashara wanasema inakuwa ni biashara hasara wakina Meku wanasema hivyo. Hatuna sababu ya kuendelea na biashara hasara, tuwasaidie Watanzania hawa wenye nia njema ya kusaidiana kukuza Uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya naunga mkono hoja ndugu yangu Mbunge wa Ukonga ambaye sasa ndiyo kuna kingine pale sijajua, nikutakie kila lakheri kwenye bajeti hii ukatekeleze vizuri pamoja na watendaji wote wa Wizara, ahsante sana. (Makofi)