Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri na niipongeze Serikali kwa jinsi ambavyo inaendelea kuimarisha mawasiliano hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita kwenye mambo machache ambapo ni mambo kama mawili au matatu. Jambo la kwanza; kwanza tuwapongeze kwa ujenzi wa minara kwenye maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha kwamba Serikali na nchi yetu ina kuwa na mawasiliano vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuomba kwamba kuna maeneo ambayo bado yana mikwamo ya minara hususan Makete kuna minara ambayo haijajengwa mpaka sasa hivi Kijiji cha Usalimwani, kumekuwa na changamoto kati ya watu wa UCSAF pamoja na watu wa hifadhi ambapo mnara unatakiwa ujengwe. Tunaomba watu wa Wizara hii muingilie kati ili muweze kusaidia ujenzi wa mnara ule ili wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia aliyozungumza Mheshimiwa Kingu kwamba fiber ipo na tunatamani itumike kibiashara kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma hii, lakini pesa inazokusanya kwenye shirika hili hatuwezi kukubaliana na kile ambacho Mheshimiwa Rais kila mwaka akisimama wakati wa kugawa magawio anakuwa anaizungumzia TTCL.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati Mheshimiwa Nape ni Waziri, Rais alisema kwamba kwa nini mnahangaika na mambo ya line za simu wakati mna fiber ambayo pekee inaweza ikaendesha shirika la TTCL. Fiber peke yake tu inatosha kuwapa ninyi utajiri na kuhakikisha kwamba Shirika linasimama na kuwa imara. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwamba ukaliangalia Shirika la TTCL kwa jicho la karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye suala la cashless economy. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Gavana wa BOT, lakini na watu wa BOT kwa sababu wao wameshaanza kuonesha mwenendo kwamba kuna umuhimu kwenye Taifa letu kutoka kwenye mifumo ya cash kwenda kwenye cashless economy na tayari BOT imeshatoa tangazo lao wakiziomba benki, lakini pia wakitoa maelekezo kwamba kutakuwepo na kupungua kwa kodi au kuweka incentives kuhakikisha kwamba watu wengi wanahamia kwenye matumizi ya cashless economy, na nitumie nafasi hii ninyi kama Wizara ya Mawasiliano mna ufunguo mkubwa kuhakikisha Taifa linahama kutoka kwenye matumizi ya cash na kwenda kwenye cashless economy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ndiye utakayeweza kumsaidia Waziri wa Fedha ili kuongoza tax base, wewe ndiye utakayemsaidia Waziri wa Fedha kuhakikisha kwamba walipa kodi wanakuwa wawazi na wanakuwa wengi kwa kuhakikisha kwamba Watanzania wengi wanahamia kwenye cashless economy. Wanahamiaje? Kwa kuongea na mitandao ya simu, kuwasiliana na Wizara ya Fedha na TRA kuhakikisha kwamba kama kuna makato na nini ziweze kupunguzwa kama ni incentives kuhakikisha kwamba Watanzania wengi wanahamia kwenye sekta ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Taifa la Rwanda, wenzetu kutoa pesa mfukoni na kulipa ni kitu ambacho hakiwezekani, kila kitu ni kwenye simu, hii inasaidia kupunguza mambo ya rushwa, lakini pia inapunguza mambo ya money laundering, ni vitu ambavyo vinakwepeka. (Makofi)
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninatamani uwe champion kwenye nchi hii kuhakikisha Taifa linahamia kwenye cashless economy. Watu waone kutumia pesa kwenye mfumo ni rahisi zaidi kuliko kutembea na maburungutu ya fedha mfukoni kwa sababu ni hatari kwa usalama wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la usalama wa mawasiliano; bado kumekuwa na kesi nyingi za watu kutapeliwa, bado kumekuwa na kesi nyingi za mambo ya AI kwa maana ya artificial itelligence. Wewe ndiye unayesimamia eneo hili, tunatamani, tunaelekea kwenye uchaguzi uhamasishe matumizi sahihi ya teknolojia kwa maana ya akili mnemba ili Watanzania wengi wawe na awareness, wekeni elimu kwenye vipindi vya television na redio ili kuhakikisha watu wengi wanakuwa na elimu kuhusu athari na madhara ya matumizi ya akili mnemba kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu akiamua kwamba aweke sura ya Mheshimiwa Jerry Silaa sehemu ambayo Mheshimiwa Bashungwa yupo anafanya hivyo na anatokea. Kitu ambacho siyo sahihi kwenye Taifa letu na kinaweza kutuletea madhara makubwa kwa sababu watu wamekuwa wepesi kuamini vitu ambavyo muda mwingine havipo, lakini wanaamini kwa sababu hawana elimu kwamba artificial intelligence inaweza ikamfanya nini mtu katika mazingira gani na ikaonekana mtu amefanya hilo tendo kumbe siyo yeye na hususan kipindi hiki cha uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni hili ambalo Mheshimiwa Kingu amezungumza. Mheshimiwa Waziri kwa kweli ni lazima utoe tamko leo kwa sababu hata mimi nina wahanga, Wana-Makete ambao walinunua hisa Vodacom baada ya Serikali kutangaza kwamba Vodacom iwe listed kwenye Dar es Salaam Stock Exchange wakajiingiza huko, walivyoingiza hiza zao hadi leo mitaji hiyo imelala, yaani mtu ameenda kununua hisa za shilingi milioni 200, shilingi milioni 100, milioni 300 badala ya mtaji kukua, mtaji sasa umekufa na bahati mbaya hata hizo hisa alizonazo hazihusiki popote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wewe ndiye una dhamana ya kutuambia leo kwamba hao Watanzania hatima yao ni nini, kama tunaenda ku-review sheria, tu-review sheria ili tuweze kunusuru, lakini leo wewe mwenyewe kama Waziri ukitaka kujiuliza, je, yale mashirika yote ya mawasiliano ambayo mlikuwa mmeomba yawe listed kwenye stock exchange, yote yaliji-list, kama mmoja ameji-list na ameingia mhanga na hisa hazikui maana yake ni kwamba kuna changamoto kwa Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ilikuwa njema kwamba Watanzania wengi waweze ku-own uchumi, waweze ku-own kuingia kwenye mifumo hii ya mawasiliano kwa sababu biashara ya hisa ni biashara kubwa duniani lakini hiki kilichoweza kutokea kwa watu ambao walinunua hisa za Vodacom imekuwa msiba badala ya kuwa mtaji. Kwa hiyo, muda mwingi sisi Wabunge tunapigiwa simu kwamba bwana tusaidie tufanye hiki, leo tunatamani kwamba Serikali itoe kauli, mitaji iliyolala, mitaji iliyo-freeze, mitaji ambayo imegota kwenye Vodacom kwenye soko la hisa mnaenda kufanya nini ili kunusuru Watanzania hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mfahamu kwamba hii ni sekta binafsi, sekta binafsi ni lazima ilelewe na kama hatuwezi kulea sekta binafsi Watanzania watakuwa waoga kwenda kwenye hilo eneo kuwekeza kwa sababu hao wengine wameshapata maumivu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, na Jerry Silaa ni kijana smart, tunaamini kabisa kwamba huwezi kuruhusu fedha hizi za Watanzania ambazo kwa takribani miaka saba, miaka nane zimelala hazikui ziko pale, zitaenda kunusuriwa kwenye maisha ya watanzania wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wengi wamepata shida kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nikuombe suala la hisa za Watanzania ambazo ziko kwenye shirika la Vodacom, leo Serikali itoe kauli na msipotoa kauli kwa kweli tutakuwa tayari kushika shilingi kuhakikisha kwamba tunanusuru. Nia ilikuwa njema, lakini wema wa nia hii umeenda kuleta matatizo kwa hiyo ni lazima tutokea katika huo mtego ambao kwa kweli umeshikilia fedha nyingi za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niendelee kumtakia kila la kheri Mheshimiwa Waziri anavyoendelea kuandaa majibu kuhakikisha kwamba anatupa majibu kwenye huu uwekezaji kwenye Shirika la Vodacom, nini kitaenda kutokea leo kwa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)