Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kabisa kwa dhati ya moyo wangu kwa kunifanya kuwa mchangiaji wa kwanza katika hotuba ya Wizara hii muhimu kwa nchi yetu, lakini nikushukuru wewe na Kiti chako kwa niaba ya Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Spika, pamoja na Wenyeviti kwa namna ambavyo mmetupa fursa Waheshimiwa Wabunge kutoa mivhango kwa maslahi ya nchi yetu tunapoenda kumaliza bajeti ambayo itatufanya Wabunge twende kwenye election na turudi tukiwa na nguvu tele ya kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mimi nitajikita kwenye mambo makubwa mawili na kwa kweli mchango wangu utakuwa katika mambo ya kitaifa, nina imani mambo ya jimboni, mambo ya minara na sisi pia tunahitaji fiber nina imani kabisa Waziri na timu yake wamejipanga watayafikisha, lakini leo mchango wangu utakuwa kutoa ushauri katika masuala mazima ya kitaifa kwa lengo la kuisaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi yatakayoleta tija katika kuleta investment katika Taifa letu katika masuala mazima ya sekta ambayo Mheshimiwa Jerry anaiongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu lilitunga Sera ya Mawasiliano mwaka 1997 na Sera ya Mawasiliano ya mwaka 1997 ilijikita katika kuhakikisha Taifa letu linavutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya telecommunication na mambo yanayohusiana na mawasiliano katika Taifa letu. Naomba nilipe Bunge lako Tukufu taarifa kuwa mwaka 2010 Serikali yetu walileta Bungeni Electronic and Postal Communications Act, ikatungwa ambayo iliweka vipengele ambavyo hivyo vitakuwa mwongozo wa hoja ninayotaka kuijenga siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ambayo sasa inaongozwa na Mheshimiwa Rais mwanamama shupavu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inapaswa kupongezwa kwa kiwango kikubwa Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takribani katika kipindi cha miongo 20, tumeona leo tumepewa statistics Taifa letu limeweza kuwa na line zilizosajiliwa zinazowafanya watu waweze kuwasiliana kwa kufika line milioni 97, hongera Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, hongera Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Electronic and Postal Communications Act iliyotungwa mwaka 2010 na kuja kusisitizwa kwa Finance Act ya mwaka 2016 na kufanyiwa marekebisho revision ya Sheria ya Electronic and Postal Communications Act ya mwaka 2022 section 26(1) na (4) ninaomba Mheshimiwa Waziri ukae kwa kutulia na Mheshimiwa Naibu wako mnisikilize ushauri ninaokwenda kuwapa kwa maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria hii tulipoitunga mwaka 2010 na tukafanya mabadiliko yake mwaka 2022 katika masuala ya kampuni za mawasiliano, tulitunga article ambayo iliyalazimisha makampuni yote ya simu Tanzania kuji-list katika stock of exchange kwa kuyataka kuachilia 25% ya stake zinunuliwe na Watanzania na lengo la sheria lilikuwa jema kabisa kuwafanya Watanzania waweze kumiliki uchumi wa Taifa lao ili tunaposema tunakuza uchumi raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wawe sehemu ya kumiliki uchumi wa Taifa letu kwa lengo ya kuwafanya sehemu ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa bahati mbaya sana niseme initial wakati sheria hii inatungwa tulipokuja kuifanyia revision mwaka 2022 tukatoa kipindi cha miezi sita kuhakikisha makampuni yote ya telecommunication, M&O zote za nchi yetu zinakwenda kuji-list ndani ya miezi sita katika DSE ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo hisa ambazo zilifanyiwa evaluation na owner wa kampuni, kampuni ya kwanza ilikuwa ni Vodacom Tanzania. Walipokwenda kuji-list kwenye stock of exchange hisa ziliuzwa kwa shilingi 850 kwa hisa moja, Watanzania wanaofanya biashara, viongozi wa Serikali, sisi Wabunge na wananchi wa kawaida wakavutiwa kwenda kununua hisa, wakawekeza katika stock ya 25% na kwa bahati mbaya sana sheria ile ilitaka 25% ya watakaonunua hisa wawe Watanzania tukawa tumewa-exclude foreign investors katika kununua zile hisa 25%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jerry, kaka yangu, naomba unisikilize sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza hapa, baada ya Watanzania kutoa mitaji yao wakanunua hisa kwenye kampuni ambayo ilikuwa ya kwanza ku-list kwenye stock of exchange, kwa bahati mbaya sana nataka nikwambie as today tunavyozungumza kwa kipindi cha miaka nane watu wamechukua fedha zao na mitaji wamewekeza kwenye Vodacom, kwa miaka nane leo tunazungumza, ukiangalia dividend ya fedha za Watanzania walizowekeza kwenye sekta hii ya mawasiliano katika kununua hisa kwenyeKampuni ya Vodacom, nataka nikuambie, leo tunavyozungumza kwa miaka nane mtu mmoja kwa hisa moja amelipwa shilingi 245, amelipwa shilingi 245 sawa na wastani wa shilingi 35 kwa mwaka kwa hisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayasema haya kujenga hoja, kama mtu huyo amenunua hisa za shilingi milioni 100 angechukua fedha hizi akaamua kuziweka hata katika treasury bond au kwenye fixed bond bei…

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi? Mheshimiwa Kanyasu.

TAARIFA

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa mchangiaji, anachangia jambo muhimu sana. Mimi ni sehemu ya watu walionunua hisa lakini hatujawahi kuona hilo gawio, lakini hata ukitaka kuziuza hakuna mtu wa kumuuzia.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Elibariki Kingu, unaipokea hiyo Taarifa ya Mheshimiwa Kanyasu?

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hii ya DC mstaafu mwenzangu na Naibu Waziri mstaafu. Lengo langu ninakwenda kujenga hoja na hayo nitafika huko tunakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie katika kipindi cha miaka nane Watanzania kwa kuwekeza pesa katika DSE kwa kununua hisa za Vodacom, wastani wa shilingi 35 kwa mwaka fedha ambazo hata mtu angezichukua akaamua kumkopesha Mzee Lukuvi bado angeweza kulipwa fedha ambazo zingeweza kuwasaidia Watanzania maskini hawa waliowekeza katika mtaji huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni nini? Kama Taifa, Mheshimiwa Waziri ninakusihi, mnapopewa nafasi na madaraka kuwashauri wakubwa na Serikali, washaurini viongozi wetu kwa maslahi ya Taifa ambayo yataweza kuvutia investment, siyo ku-deter investment katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninapozungumza hisa hizi ambazo wananchi initially walizinunua katika DSE kwa shilingi 850 leo nakwambia hisa hizi zime-drop kutoka shilingi 850 mpaka shilingi 720 na hata ukizitangaza hakuna mtu wa kuzinunua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najenga hoja hii, je, ni mitaji ya watanzania wanyonge wangapi waliyochanga fedha zao wakazipeleka DSE kununua hisa za Vodacom...

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wake umemalizika anamalizia sentensi ya mwisho.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wake umemalizika malizia sentensi ya mwisho Mheshimiwa Elibariki.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hoja hiyo, ninakuomba Waziri utakapokuja kuhitimisha utusaidie kutupa majibu, nini msimamo wa Serikali, kama hamtakuja na majibu ya kutosha tutakwenda kushika shilingi. Utuambie mnakwenda kufanya nini ku-revise hii sheria, muache soko liamue watu kwenda kuji-list kwenye DSE na watu wakifanya hivyo tutakuwa tumeokoa mitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nakuomba radhi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri, ninyi nataka niwashauri. Mwaka jana mwezi wa nane Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwenu muweze kuhakikisha kwamba TTCL inajiendesha kibiashara. Nakuomba dakika moja tu.

Mheshimiwa Waziri nataka niwasaidie, tumemuona Kadogosa ana SGR, Serikali kupitia kodi za Watanzania tumejenga SGR ya telecommunication ambapo fiber tumeizungusha nchi nzima. Mheshimiwa Jerry, kwa nini fiber hii hamuitumii kibiashara, kwa nini tuendelee kutoa fedha za Watanzania kuipa TTCL wakati kodi za Watanzania zimetumika kujenga fiber?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupa analysis ndogo ya Uganda pekee yake ningekuwa nina muda ningekupa analysis ya Mataifa 12, kwa upande wa Uganda. (Makofi)