Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Hotuba ya Waziri Mkuu, ambayo ni Hotuba nzuri inayoenda kutekeleza Dira ya Mwaka 2025/2050.

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kuwapongeza Watumishi wa Wizara zote mbili kwa kazi kubwa na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Ni namna gani unavyoisimamia na sisi Waheshimiwa Wabunge kuwepo humu ndani ya Bunge lako Tukufu kuhakikisha kwamba, tunasimamia yale ambayo tumeelekezwa na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kusema kwamba, Hotuba ya Waziri Mkuu pamoja na TAMISEMI inalenga maisha ya wananchi ambako tunatoka. Ushauri Wangu ni kwamba, ipo miundombinu mingi ambayo tumeifanya katika majimbo yetu na tunapopitisha bajeti hapa, mapato, maoteo na matarajio; tunapokuja Waheshimiwa Wabunge tumejenga maboma, zahanati, maabara, na nyumba za watumishi, ninaiomba Serikali iweze kuongezea fedha za miradi kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uzoefu wetu unatuelekeza sisi Wabunge, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vitongoji, Madiwani na kada zote kufanya uchaguzi wa kila baada ya miaka mitano. Tunakuwa na ahadi tunazozitoa kwa wananchi. Moja ya ahadi ni kuhakikisha kwamba, mimi nikichaguliwa nitafanya hiki, nitafanya hiki na wananchi wetu kwenye majimbo yetu wamekuwa wakifanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa inakuja kwenye Serikali Kuu. Fedha zinapopatikana katika miradi ya wafadhili na maeneo mengine, badala ya kwamba, tuje kumalizia miradi ambayo wananchi wameshajenga na miradi hiyo inasimamiwa na halmashauri, kinachotokea ni kuanzisha miradi mipya. Kama kuna madarasa matano pale, madarasa sita mapya yanaanzishwa kwenye eneo husika. Kwa utaratibu huu tutapiga kelele sana katika Bunge lako Tukufu, maendeleo hatutayafikia kwa kadiri tunavyoona kwenye mazungumzo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, narejea Hotuba ya Mheshimiwa Rais, alipokuwa anahutubia Bunge, alisema, sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha, sisi Watanzania, kile ambacho tunakipata tushirikiane kukitumia vizuri ili tuweze kufikia malengo ambayo tunayakusudia. Tukifanya hivyo, ninaamini kwamba, katika maeneo na majimbo mbalimbali tunaweza tukafanya kazi kubwa, nzuri, tukapata maendeleo na kutibu mahitaji ya wananchi kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kada za watumishi. Watumishi wengi wapo mjini. Vijijini tunazo changamoto kubwa sana. Mimi naomba kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, waangalie ni namna gani watumishi waliopo vijijini angalau pawe na utofauti na watu waliopo mijini. Maana sasa tunashuhudia mtumishi akiletwa kijijini atakaa siku tatu, anatengeneza matatizo kibao, anarudi mjini. Hili nalo walitazame kwa mapana zaidi. Kama Serikali tuone ni namna gani tutatibu, ili uwiano wa watumishi uweze kuwepo katika maeneo mbalimbali husika?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye wilaya yangu tumehamasisha, tukajenga maboma 75 ya shule za msingi. Mheshimiwa Waziri Shemdoe, alikuwa Mtendaji wa TAMISEMI, anajua, na taarifa anazo. Ninaiomba sana Serikali iweze kufalinyia kazi, ili tusiwakatishe wananchi kwa jitihada ambazo wanazifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejenga maboma ya nyumba za waalimu 45. Wananchi hawa tumewasukuma ili watumishi wao waweze kufundisha na kutibu watoto wao, lakini Serikali inapokuja na ramani ambazo wamezifanya Dar es Salaam na maeneo mengine, ni tofauti na kule tunapotoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba sana TAMISEMI hata mipango ya ramani wanazozileta kwenye halmashauri zetu ziendane na uhalisia. Ukweli usiopingika ni kwamba, miradi mingi inayofanywa na wananchi kijijini ndiyo iliyowasomesha wote waliopo pale mbele, lakini sasa tunapokuja huku, tunakuwa na utaalam zaidi kuliko wenyewe kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejenga zahanati 16, tunashukuru zahanati nane Serikali ya Awamu ya Sita imetuletea fedha na inaendelea kutoa huduma. Bado tuna zahanati nane. Ninaiomba Wizara ya TAMISEMI iangalie ni namna gani ya kutusaidia kwenye bajeti hii wananchi wapate huduma, kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotuelekeza na inavyotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tupo kwenye utawala, tupo kwenye kipindi ambacho ni cha kitaalam zaidi, tunanunua ndege, tunajenga SGR, tunahitaji sayansi na maabara. Wilaya yangu tumejenga maabara 27, tunaomba fedha tupate kumalizia miradi hiyo. Tukifanya hivyo, tutakuwa tunajenga dhana ambayo sasa tunajumuisha viongozi na wanafanyakazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwenye Serikali yetu. Tumekuwa na vitu vingi vinavyofanyika kwa wakati mmoja. Tumekuwa na taasisi nyingi ambazo zinaanzishwa, lakini tunaotoka kwenye halmashauri zetu, tunaamini Mkurugenzi wa Halmashauri, Mwenyekiti wa council, Baraza la Madiwani, Mkuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na viongozi wote kwenye eneo hilo ni viongozi kabisa. Vetting ilifanyika vya kutosha, wakapewa dhamana ya kusimamia maeneo hayo, na sisi Wabunge tupo humu ndani kwa ajili ya kuishauri Serikali na kutoa mawazo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizopo kwenye maeneo yetu ni kwamba, unakuta mradi umejengwa katika eneo X, lakini Ofisi ya TAMISEMI inapokuja na mawazo yake na mtazamo wake hata mamlaka iliyopo huko inavyoshauri, hakuna kusikilizwa kwamba, tumeelekeza kama ilivyo. Sasa unakaa unawaza, wewe ni kiongozi kwenye lile eneo, siku nyingine utaenda kuhamasisha wananchi ili kufanya shughuli za maendeleo?

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, nalo hilo lifanyiwe kazi, lifanywe vizuri kuondokana na changamoto zilizopo kwenye maeneo haya husika na kwenye wilaya yangu, makao makuu kwa sababu, hizi Wizara zote ni mtambuka na ndiyo wasimamizi wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mji ule unakua kwa kasi. Tunao mradi mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria, bado una changamoto, lakini tunao mradi mdogo ambao ulitengewa fedha zitoke kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji katika eneo la Lagangabilili.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ni kubwa, na pale ndiyo makao makuu. Naiomba sana Serikali, kimeshachimbwa kisima kirefu kupitia Wizara ya Maji, kwa sababu, wasimamizi wapo hapo mbele, na ndiyo Wizara ya kimtambuka hii inayosimamia yote tunayoyazungumza. Waziri Mkuu ndio msimamizi wa yote na TAMISEMI ndiyo mwenye watu wake. Naomba sana mipango hii ifanyiwe kazi, fedha zipatikane, ili wananchi wa Lagangabilili waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninaungana na wachangiaji wenzangu, wamezungumza suala la barabara. TARURA imefanya kazi kubwa na nzuri sana, na tukiwa humu Bungeni tunasifia kwa mipango mikubwa waliyoifanya, lakini Mungu naye anakuwa na mipango yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi tunaenda kwenye msimu, barabara zetu hazipitiki. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri, atutengee fedha kwenye maeneo yetu. Tusije tukawa tunaona tu Dar es Salaam na maeneo mengine, wakati tunatakiwa tuchukue mazao yetu, tuyapeleke mjini kwenda kupunguza makali ya bei. Ninaomba barabara zetu zitengenezwe, fedha za dharura ziende zikajenge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya kutoka Luguru kwenda Migato, haipitiki. Kuna barabara ya kutoka Nanga kwenda Laini – Mwaswalwe – Rugwa, haipitiki na kuna barabara ya kutoka Luguru – Mahembe – Kinamweli – Magu haipitiki. Kwa hiyo, tunapokwenda kufungua msimu, hatutaweza kufanikisha changamoto zilizopo kwenye maeneo haya. Naomba sana jambo hili liweze kufanyiwa kazi, ili kusudi wananchi waweze kufanya kazi iliyotarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, sisi kazi yetu ni kuishauri Serikali. Kati ya TARURA, RUWASA na kada nyingine, kwa mtazamo wangu ninavyoona, wale wote walitakiwa wakutane na Mkurugenzi wa Halmashauri na Baraza la Madiwani, ili kupanga uhitaji wa maendeleo kwenye eneo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa ninaweza nikasema ni Wabunge wachache sana tunaoijua hiyo miradi, lakini anayehusika ni Mkurugenzi. Ndiyo maana tunatumia nguvu kubwa sana kuhakikisha tunasimamia. Kila siku tunalalamika na unaweza ukaona fedha ya kutoka Serikali Kuu, shilingi milioni 80 au 100 ikawa imesimama tu, Mkurugenzi hajui, lakini Mkurugenzi wa RUWASA anajua na TARURA anajua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali, hawa wote wanafanya kazi moja ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, kuisaidia Serikali kusonga mbele, wawe na mwingiliano wa pamoja kwenye bajeti na taratibu zao zote, kama hivi tulivyokuja kujadili kwenye Bunge lako Tukufu. Tukifanya hivyo, tutapiga hatua, minong’ongo itapungua na kazi za kimaendeleo zitaenda kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni mgawanyo wa fedha unapotoka kwenye ujenzi wa zahanati au ujenzi wa madarasa usilingane na watu wa Dar es Salaam. Watu wa kwenye mikoa bei ya simenti ni tofauti na maeneo mengine; ni tofauti na mtu ambaye anatoka kijijini kwenye wilaya zaidi ya kilometa 800 au 1,000 na kitu unalingana na mtu ambaye yupo mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendelea hivyo, tutakuwa tunawaumiza wengine, miradi haitaisha kwa wakati, na wengine watakuwa wanapata sifa kila siku. Naomba katika Bunge lako Tukufu, waangalie ni namna gani ya kufanya mabadiliko kwenye maeneo hayo, ili kusudi kumalizia hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)