Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOHANNES L. LUKUMAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kuniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa na Umoja wa Nchi za Afrika kuwa Bingwa wa Afya ya Mama na Mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka msisitizo kwenye Bima ya Afya kwa Wote na kuhakikisha kwamba wale wananchi wote ambao wana magonjwa sugu ikiwemo ugonjwa wa moyo, figo, sukari na hawana uwezo kabisa, wanaenda kupata tiba ambayo Serikali imegharamia. Hiyo yote imeenda sambamba na watoto chini ya miaka mitano akina mama wajawazito, wazee na wale wote wanaotoka katika jamii ambayo ni maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitoe hizo shukrani kwa Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninampongeza pia kumteua Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Waziri Mkuu wetu. Ningependa nimwone nimweleze moja kwa moja, lakini atapata habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu amekuwa kimbilio la wananchi. Watu wamejenga matumaini makubwa kwa kazi anayoifanya. Amekuja kwenye jimbo langu, ametatua mambo mengi. Ameenda moja kwa moja akatatua matatizo makubwa sana yaliyokuwa yanakabili wananchi wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kubwa ni maji. Nilimweleza kuhusu matatizo ya maji katika Jimbo la Arumeru Magharibi na shilingi bilioni 520 ambayo ilikuwa inaenda Jiji la Arusha nikamwomba mwezi Novemba tarehe 30, mwaka 2025 kwamba kata zilizoko karibu na mradi huo zipate hayo maji sasa, na amefanyia kazi, akaenda akamweleza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tukapewa shilingi bilioni 2.7, na sasa wananchi wanapata maji. Ninamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa ninagawa mipira kwenye moja kati ya hizo Kata inaitwa Kiranyi ambazo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha wale wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi, akatoa mipira ya maji mingi sana. Bado Kata nyingine zilizobaki kama Kata ya Kimnyaki, Kata ya Sambasha, Kata ya Olorieni, Kata ya Tarakwa, Kata ya Oldonyosambu, Kata ya Oldonyowass, nao wategemea kupata mipira, tayari kupata maji na kuondokana na kero ya maji katika Jimbo la Arumeru Magharibi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupongeze sana kwa kunipa nafasi ya kuongea kuhusu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi anayoifanya. Kwa upande wa barabara amefanya kazi kubwa alitembelea Hospitali yangu ya Wilaya ya Olturumet, akatoa agizo sehemu kidogo tu ya kilometa mbili ya barabara itengenezwe, ikatengenezwa mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaomba pamoja na hayo yote, Jimbo la Arumeru Magharibi lina tatizo kubwa sana la barabara pamoja na matatizo mengine. Kuna barabara mbalimbali katika hili jimbo ambazo tunazo. Kuna Barabara ya Lolino – Selian, kuna Barabara ya Olturoto - Mringa, kuna Barabara ya TPRI kwenda Likamba, Barabara ya Kilimamoto -Mwandeti, Sanawari - Oldonyosambu, Sokoni II - Bangata, Mbauda - Osunyai, kuna nyingine inaitwa Malula mpaka Nduruma.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hizi zitatengenezwa kwa sababu watu hawa wanafanya kazi chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini kutokana na bajeti aliyoongeza ya TARURA, ninaomba jimbo langu liongeze bajeti kutoka shilingi bilioni 2.3 ya sasa, zifike angalau shilingi bilioni sita ili hizi barabara zilizobaki ziende kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninaongelea suala la maji. Nilisema Mheshimiwa ametatua hilo tatizo, lakini ninaomba sasa pamoja na kwamba ametatua, ninaomba miradi tisa ya maji ambayo inaendelea ya Olmolog, ilibaki shilingi milioni 700, kuna ya Oldonyosambu, Mungushi, Engalaoni, kuna Mradi wa Ilkerin, Mradi wa Engorora, kuna Mradi wa Themi ya Simba Oljoro Lengare, ninaomba Waziri wangu wa Afya atekeleze kama alivyoahidi ili hawa wananchi wa Arumeru Magharibi waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la UKIMWI. Katika ziara ya Kamati yangu, tulitembela konga ya UKIMWI kule Dar es Salaam, mambo yanaenda vizuri, lakini wananchi wale wanafanya kazi vizuri hasa yule Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, anawasaidia lakini kwa ujumla kwa Watanzania bado kuna elimu ya UKIMWI inahitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kutokana na suala lililoko sasa hivi la dawa za UKIMWI kukosekana kutoka nje za nchi, kuna kiwanda cha dawa kiko pale Arusha, ninaomba sasa zipelekwe zile shilingi bilioni 23 zilizobaki ili kiwanda kianze kufanya kazi mwezi wa sita watu wapate dawa, na pia tuweze kuuza nchi nyingine za nje hasa hizi za East Africa, tuweze kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali yangu kuhakikisha kwamba tunaenda kuweka viwanda vya kutengeneza dawa za katika nchi hii tuondokane na suala la utegemezi wa dawa kutoka nchi za nje. Hilo nilikuwa ninaomba liwekwe maanani zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa ni suala la afya ya msingi watalaamu, tunaita primary healthcare. Katika nchi hii, huduma za afya ya msingi ni muhimu. Kwa nini? Zaidi ya 75% ya Watanzania wanapata huduma katika afya ya msingi. Afya ya msingi inaanzia hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti inavyoandaliwa ya Wizara ya Afya na TAMISEMI, japokuwa baadaye nitaongelea suala la Wizara ya Afya, ninaomba sasa iwekeze zaidi, na iweke kipaumbele kwenye afya ya msingi ili wananchi waweze kupata kinga, magonjwa yale sugu yagunduliwe mapema. Wakifanyiwa screen, kwa mfano ya haraka haraka, mtu akapatikana na saratani, anaweza akatibika kwa urahisi zaidi. Magonjwa mengine kama ya kisukari, magonjwa ya moyo yanajulikana, tupate chanjo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninasisitiza zaidi kwamba afya ya msingi ipewe kipaumbele katika bajeti yetu. Hasa ukizingatia na ukiangalia kwa haraka haraka, ukienda kwenye vituo vya afya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza vifaa vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa ninavyoongea, Waheshimiwa wataniunga mkono, upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito unafanyika katika vituo vya afya. Tuimarishe hivyo vituo vya afya kwa hivi sasa ambavyo viko katika ngazi ya afya ya msingi ili wananchi walio wengi kule vijijini waweze kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwekeze zaidi kwenye hivi vituo vya afya wapatikane watumishi, vipatikane vifaa na tutangaze kazi nzuri iliyowekezwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye hivi vituo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamalizia kurasa. Nimesikia watu wanaongelea bima ya afya. Bima ya afya ni ukombozi mkubwa katika nchi hii. Ninaomba watu waelezwe umuhimu wa bima ya afya. Ninasikia watu wanasema wanadaiwa hela kwa watoto chini ya miaka mitano. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, TAMISEMI sasa ilekeze nguvu kubwa kwa vituo vya afya kuanzia hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati, wananchi wapate taarifa sahihi. Juzi nilimwona Mheshimiwa Waziri Mkuu akimwuliza Mganga Mkuu mmoja wa wilaya sipendi kumtaja. Akasema dawa zinapatikana kwa 95%, akambana, akajichanganya, akasema mtu mwingine ameenda kufanya prescription.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa watu waseme ukweli kuhusu nchi yao, waeleze ukweli, wachukue muda mdogo kuzunguza na wagonjwa. Semeni! Sera ni nzuri sana na Serikali inafanya kila jitihada, dawa zinapatikana katika vituo vya afya, wananchi hawana habari. Kwa hiyo, ninaomba ifike wakati sasa TAMISEMI ihakikishe watu wanapewa taarifa sahihi. Watu wapate tiba kama ilivyokusudiwa, na kama ilivyowekwa katika Bima ya Afya kwa Wote katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)