Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ukisoma maandiko yanasema, mshukuruni Mungu kwa kila jambo, maana moyo usiokuwa na shukurani hukausha mema yote, lakini ukisoma Quran Surat Sabayi aya ya 13 inasema, "Wa Qalilun Min 'Ibadiya sh-Shakuru" (na wachache ni miongoni mwa wale wenye shukrani).
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya, na ndani ya siku 100 za uongozi wake ahadi ambazo ameziahidi ameweza kuzitekeleza ikiwemo ahadi ya uzinduzi wa bima ya afya kwa wote ambapo tayari imeshaanza kwa awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ameahidi shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo. Fedha hizo tayari zimekwishatolewa, lakini ameahidi mpango wa pamoja wa mafunzo kati ya waajiri, VETA pamoja na vyuo vikuu. Jambo hili tayari limeshafanyika pamoja na gridi ya Taifa ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunasema tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na juzi tumeshuhudia Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano ikisaini mikataba mitano mikubwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata ajira nje ya nchi. Hili ni jambo kubwa sana, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, sisi wote ni mashuhuda, amekuwa akifanya ziara mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya, jimbo kwa jimbo, na kote alipopita ametekeleza majukumu yake ipasavyo, na amejenga matumaini makubwa sana kwa Watanzania. Kwa hiyo, sisi tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee tunawapongeza Wizara ambazo zipo ndani ya ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu: Wizara ya TAMISEMI; Kazi, Ajira na Mahusiano; Sera, Bunge na Uratibu, wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana, hongereni sana viongozi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu, sasa hivi tunatekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, na kwa sasa tunatekeleza Dira ya 2025/2026 kwenda 2030/2031 na msingi wa miaka hii mitano ni ujengaji wa uchumi shindani pamoja na kuzalisha ajira kwa maana ya tunaenda kufanya transformation, economic growth and job creation.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tunaenda kwenye uchumi shindani, imani yangu kubwa ni kwamba TAMISEMI ni moyo wa Serikali. TAMISEMI iki-paralyse, Serikali ina-paralyse; TAMISEMI ikifanya vizuri, Serikali inafanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongea hivyo kwa uzoefu. Alhamdulillah nilipata heshima ya kuhudumu kama Mkuu wa Wilaya kwa miaka tisa na nusu. Ninajua kwamba Wizara ya TAMISEMI ni Wizara ambayo inashughulika na sekta zote za maendeleo. Ukienda kwenye mikoa na wilaya, niwapongeze sana Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Ma-RAS, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Ma-DAS, na Maafisa Tarafa, wanafanya kazi kubwa na nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya, maji ya kwake, umeme wa kwake, barabara za kwake, afya ya kwake, na elimu ya kwake. Ndiyo maana nikasema TAMISEMI ni moyo wa Serikali. Kwa hiyo, ninapongeza kazi kubwa na nzuri ambayo imefanyika, lakini yapo maeneo ambayo ninatamani nishauri yaweze kuboreshwa na kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni eneo la uwajibikaji. Hayati Mzee Benjamini William Mkapa alisema uwajibikaji ndiyo msingi wa maendeleo. Wengi waliozungumza, wameelezea ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na yapo mambo ambayo yalipaswa kushughulikiwa chini, lakini yameenda kwake. Tuna haja ya kufanya reforms kwenye halmashauri zetu. Kama ambavyo tunataka economic reforms katika nchi, ipo haja ya kufanya reforms kwenye halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametuhakikishia kwamba hakutakuwa na business as usual, kutakuwa na business unusual; ili twende kwenye business unusual ni lazima watu waache kufanya kazi kwa mazoea. Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata, na Maafisa Tarafa, hawa watu chini huku wakitimiza wajibu wao vizuri Mkuu wa Wilaya, DAS, Mkurugenzi, Mkuu wa Mkoa, na RAS watakuwa na kazi nyepesi sana ya kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima TAMISEMI sasa ishuke chini kule kwa watendaji kuhakikisha wanawabana kama ni kwa mujibu wa sheria, haiwezekani mtu aharibu hapa apelekwe pale. Watu wanafanya kazi kwa urasimu, jambo la kufanyika kwa siku moja linaweza likachukua miezi mitatu. Haya mambo ni lazima tukubali kuyabadilisha ili tuweze kupiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni eneo la ukusanyaji wa mapato. Ninadhani ndiyo focus kubwa ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba halmashauri zetu zinakusanya mapato. Kwa bahati mbaya sana, ukiangalia ile Idara ya Mapato kwanza watumishi ni wachache, lakini professionalism ni changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta unazungumza na Afisa Mapato wa Halmashauri, hata vipaumbele vyake vitano vya mapato havifahamu. Unamwambia nioneshe Ledger Book, nioneshe Cash Book hana. Unamwuliza, vyanzo hivi vya mapato mara ya mwisho vimekusanywa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wafanyabiashara wamekaa miaka mpaka 10 hawajawahi kutozwa baadhi ya tozo ambazo ziko kwa mujibu wa sheria za halmashauri. Kwa hiyo, tunaona kabisa hii Idara ya Mapato ifanye reforms, tufanye mageuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaweza kufanya mabadiliko zaidi kuhakikisha kwamba aidha tunaunda kampuni ambayo itakuwa specific kwa ajili ya kubeba ajenda za kiuchumi, kwa sababu leo hii tunasema tunataka uchumi shindani lakini hatuna blue print ya uwekezaji kwenye wilaya zetu. Ukienda kwa Mkurugenzi, ukimwambia nioneshe maeneo ya uwekezaji, atakutajia kwa mdomo, lakini hatuna blueprint ya uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kongani za viwanda, maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kujenga hoteli, maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kilimo kikubwa cha kisasa, hayo mambo digitalized hayapo. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuangalia jinsi gani tunaweza kuimarisha Idara ya Fedha ili tubebe ile ajenda ya Mheshimiwa Rais ya kusema kila wilaya tuwe na viwanda vya kimkakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini huku chini tukiweka vizuri, tutakuwa na viwanda kwenye kila wilaya, na bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa ndani, tutazizalisha sisi wenyewe. Hatuna sababu ya kuagiza vitu nje ya nchi ilhali sisi kama Watanzania ndani ya nchi tuna uwezo wa kuvizalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameahidi ajira 8,000,000 kama tukiwa na business mind tukawa strategically located. Ninawahakikishieni, tuna uwezo wa kukusanya fedha nyingi sana kupitia Serikali za Mitaa. Shilingi trilioni moja hii ni ndogo kulingana na uhalisia wa vyanzo vilivyopo, mipango miji wakifanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna issue ya (PPP) Public Private Partnership. Tukishirikisha wadau wa sekta binafsi kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kimkakati ndani ya halmshauri zetu, tuna uwezo wa kukusanya mapato makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, John F. Kennedy aliwahi kusema: “Don’t ask what America has done for you? Ask how much you have done for the Americans?” Nami ninairudisha kwetu Watanzania, tusiulize Tanzania imetufanyia nini? Hebu sisi tujiulize tumeifanyia nini Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono, ahsante sana. (Makofi)