Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mwanahamis Athumani Munkunda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nami nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutujaalia afya njema Wabunge wote na Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Haikuwa hotuba tu, bali ilikuwa kama lecture ya darasani kabisa. Kila mmoja alishika kalamu kuhakikisha anafuatilia hoja zake sekta kwa sekta, hata kama wakati mwingine ilikuwa unapitiliza. Wakati tunasoma, tulikuwa tukisema kuwa Mwalimu anapopitiliza lazima urudi na umsikilize tena. Ameonesha uwezo mkubwa katika kuitendea haki hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa. Alituahidi ndani ya siku 100 atakwenda kutekeleza suala la kutoa ajira kwenye sekta ya afya na sekta ya elimu, na sisi Mkoa wa Shinyanga nakiri hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba tumepokea watumishi wapatao 562 katika sekta ya afya na sekta ya elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari hawa tumeshaongeza purchasing power kwenye mkoa. Maana yake wenye nyumba watapangisha; wenye maduka, watauza, natayari wateja zaidi ya 562 wameongezeka, ni raia sasa wa Mkoa wa Shinyanga. Tunamshukuru sana sana kwa kazi hii kubwa ndani ya muda mfupi tumeweza kupokea watumishi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba nijielekeze sasa katika kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nami nielekeze mchango wangu kwenye maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alituonesha namna ambavyo Serikali imejipanga kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha kwamba tunaboresha ukusanyaji wa mapato, na hasa mapato halisi ya ndani kwenye Serikali zetu za Mitaa na Tawala za Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kazi kubwa ya Serikali, na ili iweze kufanya kazi vizuri, ni lazima iwe na mapato. Tumeona kwa kipindi kifupi, hata Mheshimiwa Rais alisema, tunapaswa kufunga mkanda na kukusanya vizuri ipasavyo ili tuweze kutekeleza miradi yetu mikubwa ya ndani kwa fedha zetu wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hapa tuwapongeze sana TRA kwa kazi kubwa, tumeona mwezi Machi wamefika shilingi trilioni tatu. Tunawashukuru sana, kazi kubwa imefanyika kwenye ukusanyaji wa haya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua pia kazi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inachochea na kutengeneza mazingira wezeshi ili tuweze kufanya huo ukusanyaji. Kwa mfano, Serikali ilivyokuja na miradi ya TACTIC. Hii miradi ya mikoa 28 ya kuboresha miundombinu, lakini na miradi mbalimbali kwenye miji hii 28 lengo na dhana ya mradi huu wa TACTIC ilikuwa ni kuboresha na kuchochea ukuaji wa miji, lakini pia na namna ambavyo miji hii itaboresha na kutengeneza maeneo ya kibiashara ili kuweza kukuza wafanyabiashara wadogo ndani ya miji hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii imekuwa ikisuasua kwenye baadhi ya maeneo na hivyo kukwamisha au kuchelewesha dhana ya miradi hii ya TACTIC ambayo ni mkopo wa benki wa dunia. Tukitolea mfano mradi wa TACTIC ambao sisi Mkoa wa Shinyanga tumepata, uboreshaji wa barabara za mji wetu wa Manispaa ya Kahama.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu Manispaa ya Kahama ndiyo eneo pekee kwa Mkoa wa Shinyanga ambalo linakusanya mapato makubwa kwa namna ambavyo lina mwingiliano mkubwa na nchi zetu za jirani. Kwa hiyo, miradi hii ikienda kwa kusuasua inachelewesha ukuaji wa miji na pia inachelewesha ile dhana nzima ya kufanya ile untapped revenue ambazo zinategemewa kwenye miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumpongeze sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kazi kubwa ambayo ilipatikana changamoto kwa yule mkandarasi aliyekuwa anatakeleza mradi ule, na sasa tunatarajia Serikali itasimamia kwa nguvu ili basi lengo na dhana ya miradi ile ya TACTIC, liweze kufikiwa. Natambua kuwa unapofanya vizuri kwenye miradi ya TACTIC ndivyo unavyoongeza pia kupata zile fedha kwa ajili ya kuboresha miji mingine kama miji ya Babati na maeneo mengine ambayo tunategemea. Pia tunapopata hizi fedha, wakaboreshe kwenye maeneo kama ya kwako ili tuweze kuendelea kunufaika na miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalopenda kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukiangalia fedha nyingi au bajeti kubwa ambayo inaombwa imeelekezwa kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Wote tunafahamu na wote ni mashahidi, TAMISEMI (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ndiyo injini, ndio askari wetu wa mwamvuli walioko kule chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa naomba niseme kwa dhati ya moyo wangu, ninawapongeza sana Wakuu wa Mikoa nchi nzima, ninawapongeza sana Wakuu wa Wilaya nchi nzima pamoja na Wakurugenzi na Mabaraza ya Madiwani. Mapato yote haya tunayoyakusanya mwisho wa siku wale ndio wanaokwenda kuyasimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukiangalia bajeti ya Tawala za Mikoa, ukienda kifungu kwa kifungu utakuta umaliziaji wa maboma ambao wanufaika ni wananchi. Umaliziaji wa zahanati, umaliziaji wa vituo vya afya, ununuzi wa magari ya wagonjwa, uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji kazi wa halmashauri, yote hii zaidi ya 80% ya bajeti ya Tawala za Mikoa inakwenda kwenye Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni nini na ushauri wangu ni nini? Ni vyema sasa, kwa kuwa watu hawa ndio wanaobeba mzigo mkubwa na usimamizi mkubwa wa fedha hizi, ninaishauri TAMISEMI, tuwe na mafunzo ya kimkakati kwa hawa Waheshimiwa Madiwani na hasa mabaraza haya ambayo ni mapya. Wakati mwingine ukisikia na ukifuatilia ziara ya Waziri Mkuu, changamoto nyingi anazokumbana nazo ni nyingi ukiziangalia zinaweza kutatulika kule chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakijengewa uwezo watu hawa hasa Waheshimiwa Madiwani, na pia wataalamu wa ngazi ya halmashauri, hatutakuwa na changamoto kubwa hasa kwenye ile dhana kubwa ya ukusanyaji wa mapato, kwa sababu miradi mingi lengo lake ni kwenda kuchochea na kuamsha ari ya wananchi kuweza kufanya biashara kwenye mazingira ambayo ni tulivu ambayo yamewekezwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tukiwajengea uwezo Mabaraza ya Madiwani pamoja na wataalamu wetu, kazi itakuwa rahisi sana kwenye usimamizi wa fedha hizi. Tutaendelea kila siku hapa kushikana uchawi. Niseme, mzigo mkubwa ambao tunaupeleka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, wakati mwingine hatuwapi mafunzo ya kuweza kusimamia maeneo haya. Wengi wanafanya kwa uzoefu. Sisi wenyewe tumefika hapa, tumejengewa uwezo hata namna ya kutumia vifaa vilivyomo humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema sasa TAMISEMI mkaona kuna haja ya kuwa na mafunzo ya kimkakati kwa Waheshimiwa Madiwani pamoja na wataalamu wetu, mafunzo ambayo yatatutoa from oversight thinking kwenda kwenye foresight thinking, waache kuwa kama wanyampala. Waheshimiwa Madiwani waende kwenye kutatua changamoto na kuisaidia Serikali kubuni vyanzo vipya.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zipo kule chini, vyanzo vya mapato vipo kule chini. Ukienda sekta kwa sekta, ukija sekta ya kilimo, kazi kubwa itafanyika kule chini. Kwa hiyo, nilisema hilo kwenye Serikali za Mitaa tukiwajengea uwezo itatusaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nimalizie, naunga mkono hoja, lakini pia tuendelee kuzisimamia halmashauri zetu kutenga 10% ya mapato hasa halmashauri za manispaa, miji na majiji kwa ajili ya kuboresha barabara zetu za ndani ili ziweze kupitika. Hatuwezi kubebesha mzigo wote kwenye Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)