Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Eng. Johnston Johansen Mutasingwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ENG. JOHNSTON J. MUTASINGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mungu aliyetujaalia afya njema na tunaendelea na uchangiaji katika Bunge hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Bukoba Mjini kwa kunichagua kuwa Mbunge wao. Ninawaahidi kwamba nitawatumikia kwa kishindo kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na njema anayoifanya na Mawaziri wote kwa ujumla. Mnafanya kazi nzuri sana na Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, ninapenda kuchangia pale kwenye ziara anazofanya Waziri Mkuu. Kweli zimetukuka na zinaonyesha jinsi ya uwajibikaji unaopaswa kuongezeka katika watumishi wa Umma. Haya yote anayoyafanya ilitakiwa yawe yameshafanywa na watumishi kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba, kila mtumishi awe mzalendo kwa nchi yetu. Tukiwa wazalendo haya yote anayoyaona Waziri Mkuu kwa sasa hayatakuwepo, kwa sababu tutakuwa tunaiwaza Tanzania, na siyo mimi kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu akifanya kazi kwenye diameter yake akatimiza majukumu yake kwa 100%, changamoto za Watanzania zote zitaisha, maana hizi nafasi tunapewa na Mungu tuzitumie kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya katika Taifa letu ya kuwatumikia Watanzania. Mama nia yake na dhamira inaonekana wazi, kwamba sasa anapenda wananchi wapate maisha bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuchangia pale kwenye hotuba ya Waziri Mkuu aliposema kipaumbele namba nne cha kulipa wadau na wakandarasi. Hapa ninapenda kusema jambo moja. Tunapoelekea, bajeti ya mwaka wa fedha huu, tukienda kwenye bajeti ile tukiwa na madeni, hasa kwenye miundombinu na mvua hizi zinazonyesha, tunakwenda kuwa na changamoto kubwa sana ya utekelezaji wa miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaiomba Serikali kwa sasa iangalie kipaumbele hasa kwenye miundombinu maana mvua zimenyesha. Bajeti mliyoletewa kwa sasa ni tofauti kabisa na kipindi cha sasa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba Serikali ijitahidi kabla ya bajeti kutekelezwa tuangalie kwenye miundombinu, tusiwe na madeni ya wakandarasi au wazabuni. Hii itasaidia pesa yote iliyotengwa kwenda kujenga barabara, na tutakuwa tumeondoa changamoto ya barabara katika maeneo yetu nchini, maana mvua zimenyesha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata katika Jimbo letu la Bukoba Mjini, sisi terrain yetu ni mteremko, kuna makorongo na tunapata mvua kwa muda mrefu. Kwa hiyo, uharibifu wa barabara umeongezeka sana sana sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, ninashauri TARURA kuwa na kipaumbele katika manispaa zetu na majiji yetu. Sasa, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefungua barabara sana. Kwa kweli mbarikiwe sana TARURA na Rais abarikiwe sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu la Bukoba Mjini, kuna baadhi ya barabara ambazo sasa inabidi zipewe kipaumbele pamoja na kwamba zimepata matengenezo na TARURA. Kuna barabara ya Nyamukazi - Pepsi. Hii barabara inaelekea kiwanda cha Samaki, lakini baada ya mvua kunyesha mchanga wote wa ziwani umeziba, ile barabara sasa haipitiki. Kwa hiyo, ninaiomba TARURA waipe kipaumbele sana hii barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara inaitwa Kahororo – Makongo – Ntoro, na hii barabara inaelekea ziwani. Kule kuna wavuvi, lakini kuna watu wanachimba mchanga na kokoto. Hii tukiimarisha, tutakuwa tumeondoa changamoto ya ajira kwa vijana ambao wanafanya zile kazi katika ile barabara, ili waweze kwenda kuchimba mchanga na kokoto pamoja na kufanya uvuvi. Kwanza itapunguza hata gharama ya usafirishaji na wale watu watapata kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Barabara ya Kashai – Kahororo, na yenyewe inafanana vilevile. Kuna Barabara ya Chemba – Rugambwa, na hii barabara kuna wawekezaji kule wameweka shule na hoteli. Sasa, tukiijenga na wale wa sekta binafsi wataajiri vijana ambao wako mjini. Sasa, Serikali iboreshe ile miundombinu ili watu wanaoenda kujenga maeneo yale waweze kujenga na vijana waweze kupata ajira, sawasawa na barabara ya Amani ambayo inaenda Kata ya Karabaga inaunganisha Jimbo la Bukoba Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miundombinu, ninaomba Serikali ijitahidi kuangalia hayo maeneo. Pamoja na kazi nzuri inayofanyika, lakini lazima tuangalie katika hilo eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa elimu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana. Hapa mnaposema kuna upungufu wa vyoo, kuna upungufu wa madawati, siyo upungufu. Uhitaji umeongezeka. Maana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira bora kwa Watanzania na wanafunzi kwenda shuleni. Kwa hiyo, kinachotakiwa hapa ni kuongeza na kuimarisha maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa matundu ya vyoo, mimi ninaishauri Serikali, tukisema tuwape halmashauri au manispaa kufanya hii kazi itachukua muda mrefu. Lazima mje na mkakati maalum wa kwenda kumaliza hiyo changamoto kwa wakati mmoja. Niwashauri na TAMISEMI, sasa hivi kiukweli tuna maeneo madogo ya shule. Tunapoendelea kuongeza madarasa kama tunabana yale maeneo. Tujaribu kufikiria na kuja na wazo sasa la kuanza kujenga madarasa kwa mtindo wa ghorofa ili tutumie na eneo la juu kuliko kuendelea kutumia maeneo ya chini ambayo yanazidi kuwa madogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itasaidia sana kubakiza maeneo ya shule, lakini na kuja na kitu kingine tofauti kabisa. Kwa hiyo, tunaweza tukajenga basement chini tukaja juu tukaongeza madarasa kwenda juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana, hotuba ya Waziri Mkuu alisema anakwenda kuboresha na kukarabati shule za zamani. Hili ni wazo zuri sana. Sisi katika Jimbo letu la Bukoba Mjini kuna kipindi tulipata tetemeko na tuna shule za zamani. Unaweza ukaona zile shule hazikuathirika, lakini kiinjinia unaweza kukuta zimeathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nina Shule ya Bunena, hii shule ilianzishwa mwaka 1912, Shule ya Kibeta ilianzishwa mwaka 1954, Shule ya Ihungo mwaka 1947, na Mafumbo mwaka 1973, Bilele mwaka 1970. Sasa, Serikali izipe kipaumbele hizi shule kwenda kuzikarabati na kuziwekea mazingira bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina shule moja ya Nyamukazi, hii shule iko ziwani. Pia tuna Kisiwa cha Musira, na wanafunzi wengi wanatoka Musira na boti asubuhi na mchana kurudi kuja katika shule hii. Ninaiomba Serikali ione sasa katika Shule ya Musira tunaweza kujenga bweni ili wale watoto wanaoishi kwenye kisiwa kile waweze kuja kuishi shuleni na waweze kupata ile elimu ambayo ni bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru sana Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya katika sekta zote, elimu, miundombinu, na afya. Pale Bukoba Mjini tunazungukwa na ziwa. Tuna visiwa, tuna maeneo ya kuvua, kuna Nyamukazi, kuna Musira yenyewe, kuna Kifunga. Sasa, ninaiomba Serikali katika Ziwa Victoria, ili tuweze kulinda samaki wetu lazima tufanye mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, lazima tufuate sheria. Kwa sababu sisi tunaoishi ziwani tunategemea sana samaki na dagaa, wengine ndio waliotukuza sisi mpaka hapa. Uvuvi haramu imekuwa changamoto kubwa sana ya kusababisha mpaka Ziwa lifungwe. Sasa, ninaomba wasimamizi kwenye Ziwa Victoria waangalie hili suala.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kuainisha maeneo ya mazalia ya samaki na kuyawekea alama ili wavuvi wasiende kuvua maeneo yale. Hii itasaidia sana. Wakati unavua huku, huku kuna sehemu inaendelea kuzalisha samaki. Hii itasaidia sana kutofunga Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tuweze kuweka mipaka kati ya Tanzania na Uganda, kwa sababu tuna wavuvi wengi wanaovuka mpaka kwenda sehemu nyingine wanapata changamoto. Sasa, tutumie gharama kidogo tuweze ku-identify, katika Ziwa Victoria mpaka wetu sisi unaishia wapi? Maana hii imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa wavuvi na kwa watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vijana ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwanza ameanzisha Wizara ya Vijana lakini ametoa fedha kwa ajili ya vijana. Je, tuna uhakika gani kwamba hizi fedha zinakwenda kwa vijana walengwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi sana kwenda kwenye Wizara, na kwenye idara tofauti tofauti. Tuna uhakika gani kwamba hizi fedha zitawafikia vijana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninaunga mkono hoja na Mungu ambariki sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Mungu akubariki sana wewe, Amen! (Makofi)