Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe Mosi Aprili, Bunge lako Tukufu lilipokea hotuba ya Waziri Mkuu akiomba fedha shilingi trilioni 12.5 ili kuweza kuwaletea Watanzania maendeleo. Katika hotuba hiyo, Waziri Mkuu alifafanua kwa kina kabisa mambo ambayo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeyatekeleza katika mwaka huu tunaoendelea nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mambo hayo, Waziri Mkuu alieleza wazi kabisa namna ambavyo uchumi wa nchi yetu unakua. Katika mwaka 2025 tumeelezwa uchumi umekua kwa asilimia 3.3, lakini katika robo ya mwisho, umekua kwa asilimia sita, hayo ni maendeleo mazuri yenye matumaini kwa Watanzania, pia mfumuko wa bei uko ndani ya uwigo unaotakiwa. Katika Nchi za SADC, uwigo ni kati ya asilimia tatu mpaka tano, sisi tuko asilimia 3.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili, maana yake mfumuko wa bei usipodhibitiwa, maisha ya mwananchi wa kawaida yanakuwa mabaya sana. Tunaishukuru sana Serikali kwa kudhibiti mfumuko wa bei, lakini Waziri Mkuu alijifafanua kwa kina kabisa, moja ya jambo ambalo Serikali iliahidi ndani ya siku 100 baada ya uchaguzi mkuu, ni pamoja na kutoa ajira. Ajira zimetolewa kwa walimu na sekta ya afya na wengine. Tunaishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tusonge mbele na ili bajeti hii ya shilingi trilioni 12.5 pamoja na bajeti nyingine ziweze kutekelezwa vizuri, ni lazima turudi kwenye Dira 2050. Dira ambayo Rais aliizindua Julai, 2025. Dira hiyo imesema wazi kwamba takribani 70% ya matarajio yote ya kiuchumi yatatokana na sekta binafsi. Maana yake ni kwamba, tunapokwenda kutekeleza bajeti hii ambayo Waziri Mkuu ameiweka mezani na bajeti za Wizara nyingine zote lazima tutoe kipaumbele katika utekelezaji wa Dira 2050, ndiyo inatuonesha tunakwenda wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongelea moja kati ya maeneo ambayo dira imetuonesha tunapaswa twende wapi, nayo ni kukuza uwekezaji na kukuza viwanda. Katika kukuza uwekezaji na viwanda, ninashawishika sana kuyaangalia maeneo maalum ya kiuchumi. Serikali imetenga jumla ya maeneo 34 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na uwekezaji mwingine. Nami katika Jimbo langu kule Songea, ambako wananchi wa Songea Mjini wamenituma kuja kuwasemea hapa, tuna eneo la uwekezaji maalum wa kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la ekari 5,000 ambalo tayari Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeshalipa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni tano, tunamwomba Waziri Mkuu, tunaiomba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ituletee sasa wawekezaji wa viwanda pale Songea katika eneo la Mwengemshindo ili tuweze kuweka viwanda na uwekezaji na hatimaye tutekeleze Dira 2050 kwa vitendo kabisa. Kwa sababu dira hiyo siyo tu inakwenda kukuza uchumi, pia inakwenda kuzalisha ajira katika sekta binafsi, ajira ambazo tunazihitaji zaidi kuliko kitu chochote kwa hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Waziri Mkuu imeongelea suala la kilimo na katika suala la kilimo hakuna eneo ambalo wanalima sana kama Mkoa wa Ruvuma, hakuna eneo wanalima sana kama Songea ambako mimi ninatoka. Sisi ni wakulima wazuri sana hususan wa zao la mahindi na mazao mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea kilimo, lazima tujue kwamba tutahitaji kuendelea kutegemea pembejeo hususan mbolea. Serikali imefanya vizuri sana kuweka ruzuku kwenye mbolea. Tunaomba, kwa niaba ya wananchi wa Songea, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, kwa niaba ya Watanzania wote, hili suala la ruzuku kwenye mbolea liweze kuendelea, hivyo tunavyokwenda katika hotuba hasa ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo huko anakosikia, atakapokuja na bajeti yake hapa, tunataka tusikie habari ya ruzuku katika mbolea iendelee ili mwananchi na mkulima aliyeko pale Songea Lizaboni, aliyeko pale Songea Bombambili, aliyeko Songea Mjimwema, aliyeko Songea Ndilimalitembo, aweze kufaidika na ruzuku ya mbolea. Sambamba na hilo tunaomba masoko ya mazao yetu, pia viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ambayo tunalima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la barabara, Songea ni wanufaika wa utekelezaji mzuri wa mipango ya ujenzi wa barabara. Waziri wa TAMISEMI, Profesa, mpigakura wangu namba mbili, kwenye hili yeye na timu yake wapokee maua yao, Mji wa Songea sasa unang’aa kwa barabara, barabara ambazo zimejengwa kwenye miradi mbalimbali kutoka kwenye Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu kwa Waziri wa Ujenzi, ndugu yangu Ulega, mimi hupenda kumwita Shekhe na tunamjua katika Bunge hili kwamba Ulega ni Shekhe kweli kweli, akiomba dua, dua inakua dua hasa. Nimwombe sasa, tunahitaji Ujenzi wa barabara ya mchepuko kilometa 16 ndani ya Manispaa ya Songea, ili kuwaondolea wananchi adha ya msongamano wa malori 1,600 ambayo yanapita ndani ya masaa 24. Hili ni ombi letu, Wanasongea tunaomba barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Barabara pia ya Makambako – Songea, ukarabati wake ambao tumeambiwa mkandarasi amepatikana, akabidhiwe site na kuanza kazi hiyo. Tunaomba Barabara ya kutuunganisha na Msumbiji kutoka Likuyufusi kwenda Mkenda, kilometa 124 iweze kupatikana na Mkandarasi huyu aweze kufanya kazi. Tunaomba Barabara ya kutoka Lumecha kuunganisha mpaka Malinyi ili Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma iweze kuunganika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 69 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameongelea utekelezaji wa Miradi ya Maji ya Miji 28. Moja kati ya miji ambayo imetajwa katika ukurasa huo wa 69 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni Mji wa Songea. Kwenye hili tunatoa pongezi za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ya Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na Waziri wake Jumaa Aweso kwa kazi wanayotufanyia kutujengea Mradi wa Maji pale Songea wenye thamani ya shilingi 145,700,000,000. Mkandarasi yuko site kazi inaendelea. Wanasongea wanachosubiria ni kukamilika kwa mradi huo ili wanasongea waweze kupata maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu Hotuba yake; alivyotoa maelezo ya utekelezaji na kazi nzuri ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kusimamia vizuri Uchaguzi Mkuu wa 2025, uchaguzi uliotuleta sisi wote humu ndani. Kwenye hili Waheshimiwa Wabunge wote ninaomba tuipigie makofi mengi sana Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana…

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)