Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza, ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuwa sehemu ya kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Pili, ninawashukuru sana wananchi wa Monduli kwa kunichagua kuwa mwakilishi wao kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa Hotuba yake nzuri ambayo kimsingi inatoa dira na mwelekeo, hususan kwenye Wizara yetu hii nyeti ya TAMISEMI. Ninawapongeza Mawaziri na viongozi wote wanaoshiriki kwenye Wizara hii ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachangia kwenye maeneo machache. Kwanza, ninafurahi sana kuchangia kwenye eneo hili la utawala bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anawasilisha hotuba yake walikuwepo hapa Wakuu wa Mikoa wakisikiliza kwa umakini. Mimi ninajikita kwenye eneo moja hapo kwenye utawala bora kwa sababu, tunaona fika kwamba, maelekezo mengi yametolewa kwenda kusimamia na kutekeleza, lakini ninatamani sana haya maelekezo yanapotolewa, basi yafanyiwe kazi na iwe na chain ya moja kwa moja. Inapotoka kwa Mkuu wa Mkoa, inashuka Wilayani kwa Wakuu wa Wilaya, inashuka kwa Wakurugenzi, kwa chain hiyo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja hapa limezungumzwa sana juu ya ujenzi wa vyoo, limeelezwa sana na limetolewa maelekezo mengi. Sasa, jambo moja ambalo linanipa wasiwasi ni ile chain ya muunganiko wa uwasilishwaji kati ya pande zote hizi kwa sababu, unakuta wenzetu halmashauri wanaweza wakazungumza kwamba, haziko kwenye bajeti na tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa maelekezo hapa, tuhakikishe tunamaliza ujenzi wa choo. Ninaomba sana jambo hili lifanyiwe kazi na kuwe na muunganiko kati ya ofisi zote hizi tatu; Wilaya kwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini ninayasema haya? Tumekuwa na maelekezo mengi yanatolewa hapa, kama tunavyokumbuka na ninaona kwamba, utekelezaji wake unakuwa haupo. Kwa mfano, ninasema hapa, Waziri Mkuu kuna wakati akitoa maelekezo kwamba, Wakurugenzi wilayani huko wanapofanya vikao vya Kamati ya Fedha walielekezwa wafanye Siku za Jumamosi, ili Waheshimiwa Wabunge waweze kuhudhuria, lakini sijaona hata wilaya moja ambayo imeshatekeleza hilo jambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaona hapo kuna chain ndogo ambayo haina mawasiliano. Ninatamani haya maelekezo yanapotolewa kuwe na chain nzuri ya kufika kule kwenye wilaya zetu, ili angalau basi kazi hiyo ifanyike na kuwe na muunganiko mzuri. Kwa hiyo, nilisema hapo nilizungumzie.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni lazima sasa tuhakikishe kwamba, maelekezo yote yanayotolewa yawe kwenye chain ofisi, kama ni TAMISEMI, kama ni Waziri au Katibu Mkuu, watekeleze, unapokwenda huko wilayani unakuta jambo hilo halipo. Kwa mfano, kwenye jimbo langu, hapa tunavyozungumza walisema kwamba, vikao hivyo vya Kamati za Fedha vifanyike Jumamosi, nimeletewa hapa ratiba sasa hivi vipo Jumatano, sijui siku gani! Sasa, kuna haja gani ya kutoa maelekezo ambayo hayafanyiki? Ninadhani hilo linakuwa siyo utawala bora. Nimesema nizungumzie hapo, ili angalau basi wajue tunapopewa maelekezo yatimizwe, siyo tunapewa tu inakuwa kama ipo kwenye documentation peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, unapopita huko hata vile vikao vya kisheria kwenye vijiji vifanyike, ili wananchi wapewe uelewa wa kutosha, wajue sheria na taratibu zile, ndiyo maana ya utawala bora. Waende wajifunze kwamba, sheria inasema hivi, sheria inaelekeza hivi, itapunguza mkusanyiko wa kero kwenye maeneo yetu huko vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ninataka nichangie kwenye eneo hili la TARURA. Kipekee ninawapongeza TARURA kwa sababu, wameendelea kufanya kazi nzuri nchini kwetu. Wameendelea kutengeneza barabara, lakini mwaka jana Bajeti ya TARURA, yaani fedha za ndani, siweki na zile za nje kwa sababu, tunataka tujifunze, hata hotuba ya Mheshimiwa Rais alisema kabisa tujikite kuhakikisha kwamba, tunafanya kazi kwenye bajeti yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, walipitisha bajeti ya shilingi bilioni 710, sijui imefanya kazi kwa kiasi gani au imepelekwa kwa kiasi gani, hilo sijui, lakini mwaka huu wakati Mheshimiwa Rais hapa anahutubia Bunge, Wabunge wengi walitoa ya moyoni kwamba, basi TARURA iongezewe fedha. Ninashukuru na ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu, bajeti ya mwaka huu inakwenda shilingi bilioni 871, hizo ni za ndani, sijataka hizi za nje kwa sababu sina uhakika nazo, ninazungumzia za kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema wakati tunatekeleza hii bajeti kwenye mwaka wa fedha unaokuja ni vyema sasa hivi tuone ni jinsi gani tutapeleka fedha za dharura. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu tuone ni jinsi gani tutapeleka fedha za dharura kwenye majimbo yetu haya angalau barabara zirudi. Yale maeneo yaliyokatika angalau barabara zitengenezwe, ili tutakapokwenda kupitisha bajeti iende ikafanye angalau kazi ambayo tayari iko kwenye maeneo yetu kwa sababu, bajeti hii inaakisi bajeti ambayo tumefikiria kwenda kuifanyia kazi. Kwa hiyo, ninaomba TARURA ipelekewe fedha za dharura, ili zirudishe mtandao wa barabara, hali ni mbaya kwenye majimbo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ninashauri kidogo; Wenzetu wa TARURA tumekuwa na desturi ya kujenga mitaro yetu ya kukusanya maji. Tumekuwa na desturi ya kujenga ile mitaro labda kwa kusimama hivi sentimeta 70, pale chini kuna sentimeta 60 na hapa juu kuna sentimeta 120 au 130. Sasa, mwaka huu tumeona fika kwamba, maji yamekuwa mengi kwa hiyo, mitaro ile imeshindwa kuyabeba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema wenzetu wa TARURA wakabadilisha mfumo ule hapa chini wakaweka sentimeta 100, pembeni wakaweka sentimeta 80 au 90 na hapa juu wakaweka sentimeta 200 ili angalau ile slope iweze kubeba yale maji na kuya-compile, ili kupunguza uharibifu wa barabara. Kwa sababu, sasa hivi ukienda kwenye wilaya nyingi mitaro ile iliyojengwa kwa kiasi hicho mingi imetoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuangalie hizi pipe culvert. Tumekuwa na desturi ya kuweka dimension ya 90, tubadilishe mfumo tuweke ya 120 angalau iweze ku-compile yale maji na kuondoa zile changamoto ambazo zimekuwa kwenye mitaro yetu kule kwenye wilaya zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, TARURA wanafanya kazi, ni vyema tukaangalia jinsi ya kupeleka fedha. Mimi leo siulizi mwaka jana kiasi gani kilifanyika, tutakuja kuuliza baadaye kwenye hii bajeti ambayo tunakwenda kuitekeleza, lakini ni vyema tukapeleka fedha kwa wakati, ili kuwaokoa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninarudi tena hapo TAMISEMI, wengi wanajua na napeda ku-declare interest kwamba nilikuwa Diwani kwa miaka 15, hakuna Mbunge atakayesimama hapa asieleze kazi kubwa inayofanywa na Madiwani kwenye nchi hii. Rais alileta tabasamu kwa Madiwani nchi nzima, akatoa posho zao zilipwe na Hazina, tunamshukuru sana Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, zamani ulikuwa unamyenyekea Mkurugenzi ili ulipwe ile posho, lakini sasa hivi Rais amepeleka Hazina inalipwa. Ukweli uliopo ni kwamba makusanyo yetu kwenye halmashauri yamekuwa bora kiasi fulani. Ninaomba tuangalie pamoja na kwamba kwenye bajeti hii haipo au hamjaelekeza kwamba tunaboresha posho ya Madiwani, ninashauri jambo dogo, kwenye mpango huu wa makusanyo yetu ya ndani kwa sababu Madiwani ndiyo wanasimamia kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tayari Rais huku ameshatupelekea anatulipa Hazina, Halmashauri zitenge kwenye fedha zake ku-top up kiasi fulani kwenye ile posho inayotoka Hazina ili angalau ipande, kwa sababu wengine tulianza Udiwani tukilipwa shilingi 60,000, tukaenda shilingi 120,000 mpaka tukafika shilingi 350,000. Halmashauri na yenyewe iki-top up hata shilingi 150,000 ikawa shilingi 500,000 tutakuwa tumesogea hatua moja tuwasaidie wenzetu hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba sana wenzetu wa TAMISEMI, waone kwenye bajeti kule halmashauri zitengwe fedha zi-top up kwenye zile fedha ambazo Rais analipa kule kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Tutawapa motisha wenzetu Madiwani waweze kusimamia miradi, kwa sababu Mwenyekiti wa Halmashauri anasimamia zaidi ya shilingi bilioni hamsini kwenye miradi hii ya Serikali, lakini akifika hiyo posho ya shilingi 400,000 na unajua fika anaingia Jumanne ofisini, Alhamisi, anapata zile kero ambazo Mbunge anapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanatoka Wilaya nzima kumfuata, leo nina msiba, leo sijui nina nini, kwa hiyo tuboreshe maslahi ya Wenyeviti wa Halmashauri. Namwomba sana Waziri wa TAMISEMI, aangalie sana namna ya kuwaboreshea.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata zile posho za simu zisiwe zinatoka kwa baadhi ya halmashauri, wapeleke waraka unaoelekeza wilaya zote kama ni shilingi 120,000, wale Wenyeviti wa Halmashauri wapate, kama ni shilingi 50,000 wote wapate kwa uwiano, siyo wilaya hii inapata na wilaya hii haipati. Hili nilisema nilizungumzie kwa sababu kwa kweli hiyo ni kero ambayo inawasumbua sana Madiwani nchi hii. Sawa tunajua keki yetu ni ndogo, lakini ni vema tukagawana keki hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina jambo moja ninataka kuiomba Wizara ya Utumishi na ninaomba kusikilizwa kidogo. Hii keki ni yetu sote, hakuna kitu kinauma kama unakuta Wilaya B wanaajiriwa Watanzania zaidi ya 20, Wilaya C haajiriwi hata mmoja na wote sisi ni Watanzania!
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, malizia mchango wako.
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamalizia mchango wangu kwamba, ni vyema tukagawa keki hii Waziri wa Utumishi angalau kila Wilaya, ukipeleka kwenye Mkoa, angalau tutapata watumishi hata kama ni mmoja mmoja, watatu watatu, kila Wilaya ionje keki hii tupate watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ninashukuru. (Makofi)