Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niwe wa kwanza kuchangia jioni hii ya leo. Kwanza, ninatoa shukrani kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninatoa shukrani kwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Pia, ninatoa shukrani kwa wananchi wa Jimbo langu la Karatu ambao wameniamini kwa kipindi cha pili niwe mwakilishi wao katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataja mafanikio ya takribani miaka mitano iliyopita katika Jimbo langu la Karatu. Wilaya ya Karatu ilikuwa haina hospitali ya wilaya, kwa sasa Serikali imetujengea hospitali mpya katika Wilaya yetu ya Karatu, ambayo imekwishawekewa jiwe la msingi na Makamu wetu wa Rais wa wakati ule. Kwa sasa hospitali yetu ya wilaya inafanya kazi katika Jimbo letu la Karatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la vituo vya afya, Serikali imetujengea vituo vipya viwili, lakini pia, imekarabati vituo vinne vilivyokuwa vimejengwa kipindi cha mbele kwa sasa tuna huduma za vituo vya afya katika Jimbo letu la Karatu. Kuna vituo sita vya afya ambavyo vinawasaidia wananchi wetu kupewa huduma; hivi ni vituo vya Serikali na vya watu binafsi. Kwa ujumla huduma ya afya imeimarika katika jimbo letu la Karatu. Katika eneo la afya, kupitia zahanati zilizojengwa ndani ya jimbo, tulikuwa na zahanati 34 na kwa sasa tumeongeza nane na tunaelekea kuwa na zahanati 42 katika Jimbo letu la Karatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la elimu; kwa miaka mitano iliyopita Serikali imejenga sekondari saba na zote zimefunguliwa katika Jimbo la Karatu. Kwa sasa tuna zaidi ya sekondari 40 katika jimbo letu. Kwa ujumla katika eneo la elimu ya sekondari tumepiga hatua kwa kujengwa sekondari saba na zilizokuwepo awali zaidi ya 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika elimu kuna mapungufu. Katika eneo la sekondari mapungufu siyo makubwa sana, lakini katika elimu msingi kuna upungufu wa watumishi katika jimbo lile wa zaidi ya walimu 265. Pamoja na wale wapya walioletwa Serikali ilipoajiri mwaka huu 2026, lakini bado kuna upungufu wa walimu 265. Katika sekondari upungufu siyo mkubwa ni walimu 75, lakini katika elimu msingi upungufu ndiyo mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika afya; idadi ya vituo tulivyonavyo, zahanati na hospitali ya wilaya, tunatakiwa kuwa na wahudumu wa eneo la afya zaidi ya 1,500 kwa sasa tuna zaidi ya 400. Ukiangalia katika afya, pamoja na juhudi kubwa ya Serikali kujenga vituo vya afya, zahanati na hospitali ya wilaya kwa sasa tuna upungufu wa wahudumu 1,097 kutoka 1,500 katika jimbo lile. Utaona eneo la afya wahudumu ni wachache mno ukilinganisha na maeneo mengine katika eneo la watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la barabara, TARURA tulikuwa na kilomita 600. Baada ya Serikali kuongeza fedha tumeenda kuongeza kilomita 763, ninaamini baada ya kuongezewa fedha katika eneo hili la TARURA katika kilomita 763, sasa tutakwenda zaidi na wananchi wale watakuwa wanapata huduma kwa kipindi chote cha mvua na kiangazi. Jimbo letu katika eneo la TARURA lilikuwa halina hata kilomita moja ya lami. Tunaishukuru Serikali, kwa miaka hii mitano tumeweza kujengewa kilomita 4.5. Ninaamini Serikali itakuwa sikivu kujenga katika jimbo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo pia ninaishauri Wizara ya TAMISEMI; viongozi wetu wakuu kipindi kile cha kampeni huwa wanawaahidi wananchi katika eneo hili la lami katika miji midogo inayokua, kama Mji wa Karatu. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati ametembelea jimboni kwangu mwaka 2025 aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Karatu kwamba, katika kipindi hiki cha miaka mitano mingine ya kwake ataweza kuwapatia kilometa 10 za lami katika Mji wa Karatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Karatu ni mji unaokua kwa utalii na ambao huduma iko kwenye centre ambapo watalii wanaokwenda katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mbuga yetu ya Serengeti na wanaokwenda Mbuga ya Manyara, centre yao kubwa ni katika eneo la Karatu. Kwa wakati ule tulimlilia Mheshimiwa Rais kwamba, katika mji ule wa kitalii angalau aweze kutupatia kilomita 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Wizara ya TAMISEMI ni, waweze kuainisha ahadi za viongozi wetu wakuu, ili hata kama hawatafanya kwa 100%, basi angalau waweze kufanya hata kwa 50% au 60%, ili viongozi wakuu wanapotoa ahadi katika majimbo yetu wananchi wale waweze kuwa na matumaini makubwa. Ombi langu kwa TAMISEMI ni ninaomba sana ahadi hizo waziainishe, ili kuona kwamba, ni kwa kiwango gani wanaweza kwenda kutekeleza katika eneo la TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuongea katika eneo la kilimo. Serikali ilitupa sisi katika Skimu ya eneo la Bonde la Eyasi zaidi ya shilingi bilioni 38.5 na juzi juzi tu Mheshimiwa Waziri Mkuu alipoanza kufanya ziara kwenye majimbo alifika katika Jimbo la Karatu na akajionea kazi nzuri inayoendelea katika shilingi bilioni 38.5. Kulikuwa na changamoto kidogo kwenye eneo la bwawa ambapo Serikali imetoa shilingi bilioni 21, mkandarasi ana changamoto kidogo. Ombi langu kwa Serikali ni waone ni namna ipi watasukuma ile changamoto iliyokuwepo ya shilingi bilioni 21, kwa sasa haiwezi kuanza kufanya kazi japo mkandarasi yupo site.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili la kilimo, katika jimbo langu nilipata bahati ya kutembelewa na Kamishna wa TRA na tulihudhuria kikao katika Hoteli ya Acacia. Hata hivyo, kwa taarifa aliyotupa, maelekezo na mtazamo aliotuambia sisi wafanyabiashara na wakulima katika Jimbo la Karatu ni kwamba, kwa sasa wakulima wa Karatu na maeneo mengine wasiende kulima bila kutengeneza hesabu. Kwa sasa mkulima ambaye anakwenda kulima kwa shilingi milioni nne na zaidi anatakiwa atengeneze hesabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakulima wetu tunajua changamoto wanayoipata katika kazi hii ya kilimo. Mkulima wa Tanzania anakwenda kulima siyo kwamba anakwenda kupata faida; asubuhi akiamka kwa sababu, mvua ikinyesha ndiyo kazi yake anakwenda kulima. Sasa kama ndiyo mpango wa Serikali na kama ndiyo Serikali imekuja kwa kusema kwamba, mkulima anayepata zaidi ya shilingi milioni nne achangie kodi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali iko hapa na ninawaambia, ndugu zangu tunakoelekea kutakuwa siyo kuzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama maelekezo ya Kamishna wa TRA niliyekutana naye katika Jimbo la Karatu na kwa mwelekeo alioutoa siku ile na nilivyomsikiliza ni kwamba, sasa wakulima wa Tanzania ambao wanakwenda kupata shilingi milioni 4.1 wanakwenda kuwa walipa kodi. Sasa kama wanakwenda kuwa walipa kodi na wakati huo Watanzania wanalima bila kuwa na faida yoyote wanayopata. Hii hesabu wanapokwenda kutengeneza, wanatengeneza kwa fedha ipi wakati hata hajaenda kulima kile kilimo ambacho, mimi katika jimbo langu mkulima anapata gunia tano mpaka 10. Sasa kama Serikali italeta mpango wa kusema kwamba, mkulima kupata shilingi milioni 4.1, achangie kodi itakuwa ni jambo gumu sana katika Jimbo langu la Karatu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)