Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya mapato na maendeleo kwa kazi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inatuonesha kwamba pato la dunia limepanda kwa mwaka 2025 3.3% na pato letu la Taifa Tanzania 6.0%. Hii ni ishara kwamba bado nchi yetu tuko vizuri na mwenendo wa ukuaji wa pato la Taifa unakwenda vizuri. Kwa sababu hiyo nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na nimhakikishie, tuko pamoja na yeye aendelee kusonga mbele Taifa letu lisonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye ni mtoa hoja pamoja na wasaidizi wake, tumeona ziara zako ambazo zimekuwa na tija, zimegusa wananchi wa kawaida kule chini. Tunaomba sasa kuwe na mwendelezo, yale malalamiko ya wananchi ambayo waliyawasilisha kwako waweze kupata mrejesho na tija ya ziara ile iweze kuwa nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuwapongeza Watendaji wote wa Serikali Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, lakini na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu na watendaji wote kwa kazi nzuri. Sisi Wanahai tuendelee kumhakikishia Mheshimiwa Rais tuko pamoja naye. Tumemwona kila mahali, ukipita kwenye kata zetu 17 tunamwona Mheshimiwa Dkt. Samia miradi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna miradi mikubwa inaendelea pale Soko la Kwa Sadala. Sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shemeji yetu, asukume lile soko liende kwa speed inayofanana naye na asukume lile Soko la Mula liende kwa speed inayofanana naye. Tunaona jengo la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai linakwenda kwa speed ya kuridhisha pamoja na nyumba. Hiyo ndiyo Hai mpya ya Mama Samia na Saashisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme jambo hapa. Waswahili wana msemo ‘kimfaacho mtu chake.’ Tumeingia kwenye shida ya mafuta ambayo siyo ya kwetu ni ya kidunia. Sisi Watanzania tumekuwa wahanga, lakini na sisi tuna cha kwetu tulijiandaa na hayo ni maono mazuri ya Mheshimiwa Rais alipoanza kusema tuwe na reserve yetu ya dhahabu ili itusaidie wakati wa shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani ni wakati sahihi sasa ile reserve ya dhahabu iuzwe tupate fedha, fedha iingizwe kwenye ruzuku ili bei ya mafuta irudi pale ilipokuwa awali kwa sababu hiki ndiyo cha kwetu. Kimfaacho mtu chake, dhahabu ya kwetu na mama alioona mapema kwamba kuna shida itatokea, shida imetokea tufanye maamuzi ya haraka fedha ipatikane, tutoe ruzuku, mafuta yarudi kwenye bei ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuweke mipango endelevu ya kuhakikisha tunakuwa na ruzuku, lakini pia tunakuwa na reserve ya kutosha ya mafuta kwa sababu dunia hatuwezi kui-control sisi wenyewe. Mambo kama haya yanayotokea sasa hivi yanaweza kutokea wakati wowote. Kwa hiyo, Waziri wa Nishati uumize kichwa uone namna ambavyo tutakuwa na reserve ya kutosha ya mafuta ili tunapopata majanga tusiweze kuathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 47 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza kuhusiana na suala la usafiri na usafirishaji na akasema ili kupunguza msongamano wa vyombo vya moto na kuimarisha usafiri pamoja na miundombinu kujengwa iko mikakati ameeleza pale. Ninataka kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake, liko eneo muhimu sana la usafirishaji nalo ninalotaka nilizungumzie leo, vijana wetu wa bodaboda na bajaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili kama hatutalitazama vizuri ni eneo ambalo litakuja kutuletea shida huko mbele. Leo hii kila wilaya imejaa vijana wa bodaboda na vijana wa bajaji. Ninaomba tutazame kundi hili, nianze cha kwanza kuishauri Serikali tupate takwimu za vijana hawa kila wilaya na hali zao za kiuchumi na hali zao za kielimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya ya Dodoma hapa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma atusaidie bahati nzuri they are well organized hawa vijana, tayari wameshajiunda kila ukienda utakuta bodaboda, kituo fulani wana mwenyekiti wao, wana kiongozi wao na wameanzisha vi-SACCOSS vyao vizuri ili tuweze kuwafahamu ni akina nani. Ninajua lakini ninataka kwa takwimu, ninajua kuna vijana wana masters wanafanya biashara hii, kuna vijana wetu wana degree moja, wanafanya biashara hii, wapo vijana wa diploma, wapo wa certificate na wapo wengine wenye elimu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatutawatambua na kuwapa elimu biashara hii itakuwa ni mzigo na usumbufu barabarani, lakini tungeweza kuibadilisha kwa haraka na ikawa na manufaa kama wenzetu wa Rwanda walivyofanikiwa. Sisi ni mashahidi ukienda Rwanda utakuta bodaboda akifika kwanza amevaa reflector yenye namba yake inayomtambulisha na namba yake ya simu. Mbili, amevaa helmet. Kwa hiyo, cha kwanza kwa faida ya vijana wa bodaboda na bajaji ili usafiri huu uweze kutumiwa na makundi ya watu wote ni lazima wakubali kupata elimu na kufuata utaratibu ili biashara yao iweze kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Rwanda unaweza ukavaa suti yako ukapanda bodaboda na ukafika salama. Akifika kwenye zebra anasimama anasubiri taa zimwongoze na sisi tunaweza kufika hapo. Tunafikaje hapo? Tuwatambue kwanza. Tukishawatambua tuwaweke kwa makundi yao na elimu zao ili tuweze kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani, ninazungumza tunaweza tukatoa hata ajira hizi tunazotoa hapa. Mheshimiwa Rais alitoa ajira 12,000, hapa tunaweza tukasema kama kuna kijana wa Kitanzania ana degree mbili amethubutu kwenda kukodisha bodaboda kwa mkataba mgumu na akawasha bodaboda akaingia mtaani huyu ana commitment ya kazi, huyu ana utayari wa kufanya kazi. Ukimchukua ukampeleka ofisini atakuwa mwaminifu, atakuwa mchapakazi mzuri ili kwamba tukishajua Dodoma hapa au Wilaya ya Hai tuna vijana kadhaa wana degree ya elimu, tuna vijana kadhaa wana degree ya uhasibu, tunapotangaza kazi zetu tuwape kipaumbele kule kwenye vijiwe vyao kwa kuangalia taaluma zao na washindanishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani, tunapata vibali vya ajira 1,000 tutenge ajira labda 2,000 kwa ajili ya kuwa-motivate vijana wa bodaboda na wenyewe twende tukawashindanishe huko kwenye makundi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tutakuwa tumewatambua vijana hawa na kuwafanya wawe na uzalendo na kuona wao ni sehemu ya Tanzania linapotokea tatizo lolote wataitazama nchi yao kama ni nchi yao na wanahusika nayo. Pili, kwa kuwa wameshajipanga na tumeona changamoto kubwa wanapata ajali, wakati mwingine badala ya kuingiza familia kwenye kuinua pato wanarudi nyuma kwa sababu pesa zinaenda kwenye matibabu, nikaomba tuwe na kifurushi maalum kwa ajili ya vijana hawa bodaboda. Ninaamini wana uwezo kupitia vikundi vyao wakajiunga wakaweza kupata matibabu kupitia vifurushi maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 22 amezungumza kuhusu sekta ya uzalishaji na akam-quote Baba wa Taifa kwenye kitabu chake cha mtu na maendeleo, ninaomba kunukuu, alisema: “Maendeleo ya kweli huanza pale wananchi wanapoweza kuzalisha chakula cha kuwatosha wenyewe.” Pamoja na bajeti hii ya Waziri Mkuu ninajua ni mwendelezo tutakuja kupata bajeti ya kilimo lazima mipango yetu ijielekeze kwenye kuongeza uzalishaji kwa sababu ukiongeza uzalishaji ndiyo unaongoza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja hapa ambalo linatusumbua kwenye Wilaya yetu ya Hai, sisi ni wachapakazi wazuri sana, lakini sasa hivi tuna crisis kubwa ya mbolea. Sasa hivi nimezungumza na mawakala wawili wa mbolea, mbolea Wilaya Hai hakuna na kipindi hiki muda huu ndiyo muda wa kwenda kuweka mahindi na nafaka zetu mbolea. Niombe Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo waende kwa dharura kuangalia namna gani mbolea inaweza kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa mbolea hii tunajua kwa ruzuku inauzwa kulingana na makundi yake shilingi 73,600 kulingana na aina ya mbolea. Wilaya Hai mbolea imefika mpaka shilingi 170,000, hii siyo sawa. Niiombe Wizara ya Kilimo iweke mechanism ya kuweza ku-control bei ya soko la mbolea ili wananchi wakutane na kile ambacho ndicho kilichopangwa na Serikali na ruzuku yao ambayo imewekwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka kuhusu TAMISEMI, tunapanga bajeti ya TARURA ya barabara zetu na Serikali inafahamu ndilo eneo ambalo linatugusa sana sisi wananchi na sisi Wabunge. Niombe fedha inayopangwa kwenye bajeti ya TARURA iende na iende kwa wakati. Tumepata mafuriko hapa sasa hivi ni kilio barabara nyingi zimeharibika zikiwemo za Wilaya ya Hai. Nimekuwa nikisema hapa na ninaendelea kurudia, karne hii siyo jambo la kufurahisha wananchi wa mjini kama wa Hai watumie boti kuvuka, hii siyo sawa na Mkuu wa Mkoa yuko pale siyo sawa. Haifanani na sisi, niwaombe sana tafadhali wapeleke fedha hasa lile fungu la dharura ili likaweza kuhudumia barabara zetu ambazo zimeharibika na wananchi waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwa kuwa ni TAMISEMI, sisi kama Mkoa wa Kilimanjaro kwa sababu ya historia yetu ni kweli wazee wetu walijitahidi wakajenga shule nyingi wakati wa mwaka 1952 na kuendelea. Sasa mipango ya Serikali inapokuja kujenga shule mpya sisi wa Kilimanjaro tunabaki nyuma kwa sababu shule zetu ni chakavu tumeleta maombi maalum ya kuomba fedha kwa ajili ya kutengeneza shule chakavu. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie fedha hizi zitoke kwa wakati ili tuweze kwenda kufanya matengenezo shule zetu na vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa asubuhi nimeuliza tena kuhusiana na uchakavu wa vituo vya afya ili na sisi Kilimanjaro na Wilaya ya Hai tuweze kufanana na wale ambao wanajenga shule mpya kuliko hivi wanavyotuacha nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, Serikali imejenga miundombinu ya kutosha. Nimekuwa nikisema hapa na ninarudia tena, sijaona humu kwenye bajeti ya TAMISEMI wakiwa wanaweka fungu linaloenda kufanya matengenezo. Tumejenga miundombinu mingi sana. Hapa Chuo Kikuu cha Dodoma mtaona Serikali imeweka fedha nyingi ukienda Chuo cha UDOM sasa hivi vyoo vimefurika, vigae vinabanduka na majengo yanashuka, siyo sawa. Nilitamani Serikali tunapojenga miundombinu tuweke na fungu maalum kwa ajili ya ukarabati ili miundombinu yetu iweze kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia la mwisho, nimeona umewasha mic hapa. Tangu ninasoma shule ya msingi ninasikia Liganga na Mchuchuma, Liganga na Mchuchuma. Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, sasa kabla sijastaafu amalizane nayo hii biashara. Kwa sababu tunategemea makaa ya mawe na chuma yaletwe pale Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools tutengeneze chuma. Msemaji niliyemfuata hapa ametoa takwimu chuma ambacho tunanunua kwa fedha nyingi nje ya nchi kumbe tungeweza kutengeneza hapa. Nimwombe sana Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo asimamie hili ambalo nimeanza kulisikia tangu nikiwa shule ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)