Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie bajeti hii muhimu kabisa ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote nianze kwa kuishukuru sana Serikali kwa kupanga maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa yaweze kufanyika Mkoani Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Njombe na Wabunge wenzangu nao watasema. Tunaona kwamba Serikali imetupa kipaumbele kikubwa sana na imetuthamini sana wananchi wa Njombe. Ni fursa kubwa pia kwa wananchi kutokana na ujio wa viongozi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niwaombe sasa Waheshimiwa Mawaziri, alikuwepo Mheshimiwa Waziri Mkuu naona bahati mbaya ametoka niweze kuwaalika kutembelea Jimbo la Ludewa, kutembelea ile Barabara ya Itoni – Ludewa – Manda na ile Barabara ya Mkiu – Liganga – Madaba kwa sababu sasa hivi ninatambua kwamba Serikali imefanya jitihada kubwa sasa kukwamua Mradi wa Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunavyozungumzia Mradi wa Liganga na Mchuchuma, wananchi wanajiuliza sasa kwamba, tunasema mradi uko hatua nzuri, mbona barabara bado ni changamoto sana? Kwa hiyo, ninaamini kupitia ugeni huu wa Mheshimiwa Rais, Mkoa wa Njombe tutapata wageni Ludewa, ambao watakwenda kutembelea Barabara ya Itoni-Ludewa-Manda lakini vilevile hii Barabara ya Mkiu – Liganga – Madaba kwa Mheshimiwa Super Feo kule, ni muhimu sana kwa sababu miradi hii kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ndiyo inabeba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokisema Mheshimiwa Kitila Mkumbo anajua maana yake nini. Kwa kuwa sasa hivi nimeona Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye taarifa yake amezungumzia Mradi huu wa Liganga na kuonyesha kwamba Serikali iko serious sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninatafuta takwimu chache nimeona kwamba kwa kitendo cha Serikali kuagiza chuma nje ya nchi, tunapoteza fedha nyingi sana za kigeni kati ya dola bilioni 1.22 hadi dola bilioni 1.5 ambazo ni sawasawa na shilingi za Kitanzania trilioni 3.2 hadi trilioni 3.5. Kwa hiyo, hii ni fedha nyingi sana ambayo tunaipoteza kwa kuagiza chuma nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi tunapoteza vilevile ajira nyingi. Mradi unaweza ukaajiri Watanzania wengi sana na katika hili tuombe Serikali isielekeze viwanda vyote eneo moja. Ni lazima tuweze kutawanya hii miradi ili wananchi wasijae sehemu moja. Jiji la Dar es Salaam tunahangaika leo foleni pale, lakini sasa viwanda vyote tunataka vikae kule. Makambako kulikuwa na Kiwanda pale cha Dawa na hicho ndiyo tunataka tukipeleke Dar es Salaam. Kumbe tukivitawanya hivi viwanda hata wananchi tuna-control mtawanyiko wa watu wetu. Wengine watakwenda uelekeo huu wengine watakwenda uelekeo huu. Kwa hiyo, wananchi wanaona pale pana fursa ya ajira nyingi sana ambazo Serikali inazikosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha ajira hata kodi mbalimbali, zile kodi ambazo mwekezaji angelipa Liganga zinakosekana. Kwa hiyo, kuna kila sababu ya kuanza huu mradi na kabla ya kuanza mradi tuanze kuboresha ile miundombinu. Barabara ile kutoka Itoni – Ludewa – Manda na Mkiu – Liganga -Madaba. Vilevile, ninashukuru kwenye taarifa zote za fedha nimeona kwenye bajeti imo. Tumeona pale kuna ile Barabara inayoanzia kule Liganga kuunganisha na Mchuchuma kupitia Ibumi. Tumeona imetengewa fedha pale, ninaishukuru sana Serikali kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia hata Barabara kutoka Mawengi kwenda Manda ambacho ni kilio kikubwa sana cha wananchi na ndiyo maana ninaomba ikiwezekana kabla ya Mei Mosi kama Mheshimiwa Waziri Mkuu atapata nafasi aweze kwenda kuikagua ili aone jinsi gani wananchi wa Ludewa wanavyokutana na changamoto za usafiri kwa muda mrefu. Tunatambua kwamba kuna mkandarasi na tunatambua kwamba Serikali imemlipa. Kwa hiyo, tunaona jitihada, lakini sasa tunaomba twende kwenye matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua sasa kwa kule inakwenda mwisho. Tunaomba Wizara ya Ujenzi itusaidie mkandarasi aweze kurudi site, aanze kurudisha vifaa site na afanye maandalizi kwa ajili ya kuendelea na ujenzi ile sehemu ya Lusitu mpaka Njombe. Hii nyingine tukipitisha bajeti nami ninaunga mkono hoja kwa sababu ninaona kuna fedha kwa ajili ya Barabara kipande cha kutoka Mawengi hadi Manda kilometa 211, lakini vilevile hizo kilometa 70. Kwa hiyo, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja ili hayo yaweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo wananchi wa Ludewa wanapenda kulifahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ni jambo kama la kisera ndiyo maana ninalisemea hapa, lakini lilifaa sana kule kwa Mheshimiwa Aweso kwenye Wizara ya Maji. Kulikuwa na miradi ya maji ambayo ilikuwa ifadhiliwe na USAID. Kwa Ludewa tulikuwa na miradi tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na ukarabati wa Mradi wa Maji Ibungulu – Lifua – Manda. Kulikuwa na ujenzi wa Mradi wa Maji Masimbwe - Lupanga na Mlangali. Kulikuwa na Mradi wa Utilili; kulikuwa na Mradi wa Kitewele; kulikuwa na Mradi wa Mkiu; kulikuwa na Mradi wa Liughai lakini vilevile, kulikuwa na Mradi wa Maji wa Kiwe. Kulikuwa na ukarabati Mradi wa Ludewa Mjini na Ludewa Vijijini (Mapeto na kwa Magego), lakini sasa kwa bahati mbaya miradi hii yule mfadhili alijiondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka kuona kwa sababu jambo limekaa kama sera, je, Serikali ina mpango gani? Ninatamani sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati wa kuhitimisha atoe maelekezo kwamba ile miradi yote ambayo ilikwama kutokana na mfadhili kujiondoa ambaye ni USAID iweze kuingizwa kwenye bajeti za Serikali kupitia Mfuko wa Maji ili wananchi hawa waweze kuondokana na changamoto za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile eneo lingine ambalo nilipenda kulizungumzia ni eneo la elimu. Kule Ludewa tuna shule za msingi za Serikali 114, vilevile tuna shule nne binafsi. Tunaishukuru Serikali miaka mitano iliyopita imefanya kazi kubwa sana kuboresha miundombinu ya elimu ya shule za sekondari, lakini kwenye eneo la shule ya msingi bado kidogo kwa Ludewa tuko nyuma. Katika hizi shule 114, shule nyingi zina miundombinu ambayo ni chakavu sana, lakini vilevile zina uhaba wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa pia nimeomba takwimu kwa shule hizi 118 tuna wanafunzi 34,705 kati ya hao watoto wa kiume wako 17,093 na watoto wa kike 17,612. Hata hivyo, tuna upungufu wa Walimu 565 kwa sababu walimu ambao tunao kwa sasa ni 685. Kwa hiyo, Walimu 685 ukiwagawa kwenye hizi shule 118, unaona jinsi gani kuna shule nyingine kwa mfano Shule ya Msingi Mbongo ninavyozungumza ina walimu wawili. Shule ya Msingi Kipingo na Shule ya Msingi Nkwimbili. Kwa hiyo, wastani kwa shule tunakuwa na walimu wanne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali iweze kutuongezea walimu, kwa sababu ninatambua walimu tuliletewa na kila mwaka Serikali imekuwa ikiajiri walimu, ila changamoto ya kasi ya kuhamisha walimu ni kubwa sana. Ninajua hatuwezi kuzuia uhamisho wa Serikali, lakini tunaomba sasa kwenye mgawo huu wa sasa Ludewa iweze kupewa walimu mbadala ili tuweze kuondoka kwenye kuwa na walimu wawili mpaka kuwa walimu nane angalau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wenyewe ukiongea nao inaonesha kwamba ili mwalimu aweze kutimiza wajibu wake ipasavyo inabidi shule angalau iwe na walimu nane. Hapo ndipo mwalimu anaweza akaandaa lesson plan kwa utulivu, akaandaa hiyo subject logbook akaandaa na teaching aids na vitu vingine vyote vinavyohitajika na watoto watapata taaluma ambayo ni bora sana. Sasa shule ikiwa na walimu wawili, mmoja akipata dharura inakuwa ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona umewasha kipaza sauti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)