Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon Zacharia Paulo Issaay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia mada iliyopo mezani. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa rehema zake mbalimbali katika Taifa letu na sisi kwa ujumla, kwa kweli kuna mambo mengi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu hadi tulipofika hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa inayofanyika hasa katika Jimbo langu la Mbulu Mjini na Tanzania kwa ujumla kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI. Kamati yetu inakwenda maeneo mengi nchini na kwa hivyo kazi kubwa imefanyika katika nchi hii, ni vile tu mahitaji yetu hayatakwisha na kwa namna ya pekee tuna kazi nyingi ambazo zimefanyika na imeonesha dhamira ya Rais kwa Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimpongeze sana kwanza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia kwa kazi kubwa anayofanya katika Taifa letu na hasa kwa ziara zake. Kwa kweli ziara yake imeibua mambo mengi na imeonyesha hali halisi ya Watanzania na changamoto walizonazo, lakini pia na mambo ambayo wangeyahitaji. Tunamwombea kila la heri, lakini pia kwa namna ya pekee aendelee na moyo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa Watanzania ameibua mambo mengi na ninadhani kwa upande wa Serikali kuna uratibu unafanyika ili yale yote yaliyoibuliwa kwenye ziara yake yaweze kufanyiwa kazi na Serikali iweze kuonekana mbeleni kwa Watanzania kama kazi ambayo inafanyika kwake na wasimamizi wote, nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nipongeze Wizara zote zilizowasilisha mada zake mezani leo kupitia kwake yeye Mheshimiwa Waziri Mkuu, Wizara ya TAMISEMI na Wizara zingine zote kwa namna ya pekee. Ndugu zangu TAMISEMI ni Wizara kubwa sana, Ni wizara ambayo ipo nchi nzima kuanzia kwa mwananchi wa chini mpaka hapa Serikali Kuu kwa maana ya Waziri Mkuu na hatimaye kwa Rais kwa sababu kazi inayofanywa na TAMISEMI ni kazi kubwa sana. Kwa hiyo, tunaipongeza sana hii Wizara lakini kwake Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini pia na Wizara zote pamoja na Serikali kwa ujumla. Ninaenda awamu ya tatu kwa wale tuliotoka 2015, kazi hii imefanyika sana na imeonesha matokeo chanya kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee tuendelee kuiombea nchi yetu amani, lakini pia na mshikamano ili kupata mafanikio hayo ambayo tunatarajia kuyapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwanza kuona kabisa umuhimu wa kuomba sana Serikali itoe fedha za TAMISEMI au Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na TAMISEMI na wizara zilizo chini yake kwa sababu kazi kubwa inafanyika, lakini miradi hii ambayo inatekelezwa na shughuli zinazotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Wizara zilizo chini yake kwa ujumla tuna kazi nyingi kutoka kwa mwananchi hadi hapo tulipofika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee pia nizungumzie suala hili la Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo tuna Vitengo kuanzia TAMISEMI ambapo kwenyewe, huku tuna masuala ya maji, masuala ya TARURA na masuala mbalimbali ambapo kwa namna ya pekee hatuna namna nyingine zaidi ya kumfikia Mtanzania kama hatuyatimizi yale ambayo tumeyaweka kwenye malengo yetu kwa mwaka ule wa fedha wa Serikali, lakini pia kwa utekelezaji mbalimbali wa mipango ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee pia niwapongeze Viongozi Wakuu wote wa Nchi hii, Marais waliotangulia hadi Rais aliyeko madarakani, lakini tuna ahadi ambazo bado hazijakamilishwa kutoka kwa Viongozi wetu Wakuu. Nadhani Serikali iratibu hizi ahadi na ione namna ambavyo itaweka kwenye mipango yake kila mwaka mfano mmoja uko kwenye jimbo langu la Mbulu Mjini. Kule Mbulu Mjini tuna ahadi ya Mheshimiwa hayati John Pombe Magufuli ya kilomita tano ndani ya Mji wa Mbulu lakini hadi sasa walau bado kilomita 1.2, zingine tunaishukuru sana Serikali imefanyia kazi na ahadi hizo zimetekelezwa lakini kwa sasa wananchi bado wana hamu kubwa ya kusubiri ahadi hiyo itekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi kama hizo ziko kwa nchi nzima. Nadhani ni jambo jema tukaziratibu tukaziweka kwenye mipango na hata kama hatuwezi kutekeleza kwa mara moja, basi tuendelee kuzitekeleza kwa awamu awamu ili kuona kwamba yale yaliyoahidiwa na viongozi wetu yanapata kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuzungumza kwenye ahadi hizi ni kwamba mara nyingi imeahidiwa na viongozi wakubwa kwa sababu lilikuwa hitaji la wananchi, lakini pia uongozi waliona walipotembelea maeneo hayo kuna mahitaji hayo makubwa. Nini kifanyike? Ni katika mipango yetu ambayo hata kama hatuwezi kutekeleza kwa mara moja basi tufanyie kazi ili kuweza kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la vijana taka tusitake tusijifiche nyuma ya pazia. Vijana nchini wamekuwa wengi ambao wamemaliza vyuo, wanasubiri ajira na ajira hazipatikani. Nimpongeze Mheshimiwa Kangi alipochangia, ushauri wangu ni mdogo tu, hebu Serikali iratibu sasa hivi asilimia ngapi ya vijana wanafanya shughuli za bodaboda? Je, hiyo shughuli za bodaboda mbele ya safari ina mwanga? Mimi nikiangalia tunaingiza bodaboda nyingi vijana wengi wananunua na wengine wananunuliwa hizo bodaboda, lakini mbele ya safari ni shughuli ambayo haina dira kwa vijana wetu. Tujielekeze kwenye malengo makubwa ya kuwashawishi wawekezaji katika mazingira ya viwanda na mazingira mengine ili vijana waweze kuajirika na waweze kupata shughuli kuwa na matumaini kwa Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tuna halmashauri kwa mfano Mbulu Mjini, ninakusanya si zaidi ya bilioni mbili na nusu, lakini kuna halmashauri zinakusanya karibu bilioni 40, bilioni 30 Mungu amewajalia, hatuna namna yoyote ya kuwachukia zaidi ya kuwapongeza na zaidi ya kuziombea hizo halmashauri. Ushauri wangu ni nini? Zile halmashauri ziruhusiwe kuajiri hawa vijana kwenye zile nafasi za Serikali ambazo zipo kwa kupitia fedha zao. Kwa sababu tusiporuhusu kuajiri wale tukasubiri kapu la Serikali liwaajiri hawa vijana wote nchini kupitia Serikali Kuu, kwa kweli hatua hiyo hatutaifikia haraka na tutakuwa na genge la vijana ambao baadaye wanaichukia Serikali yao na mazingira yao hayataruhusu hali ambayo itakuwa nzuri. Nadhani kuna haja ya kufanya tathmini na kuona kwa sababu upungufu ni mkubwa sana Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu ni mkubwa kwenye sekta za umma, lakini tukiangalia mazingira ambayo yanaweza kuwasaidia hao vijana wakaingia kwenye ajira kwa baadhi ya sehemu na Serikali itaendelea na zile halmashauri na zile taasisi ambazo hazina uwezo kujaza zile gap ambazo ni muhimu sana kwa vipaumbele itatusaidia kuliko wote tukategemea kapu la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni fedha za TARURA. Tunaipongeza Serikali ilipoanzisha TARURA ilikuwa hapa Bungeni imefanya kazi kubwa sana katika nchi hii, imefungua barabara nyingi katika nchi hii imefanya nchi hii wananchi wafikie huduma kwa urahisi lakini changamoto kubwa wanayo toka tulipofungua zile Barabara, fedha zao hatujaongeza hata kiasi chochote na kwa namna ya pekee sasa ile miradi tuliyoanzisha, barabara mpya tulizofungua kama kwenye jimbo langu hazijapata matengenezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mitatu, minne ninaiomba sana Serikali, bajeti ya TARURA itolewe kwa kiasi kilichopitishwa kwenye Bunge hili ili tuweze kurekebisha zile barabara na kutoa fedha za matengenezo ili zile barabara za kuunganisha mwananchi kutoka kitongojini hadi kwenye Makao Makuu ya Tarafa, kutoka Makao Makuu ya Tarafa kwenda kwenye Makao Makuu ya Halmashauri, barabara zile ziweze kupitika wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hela za Mfuko wa Jimbo zimekosekana kwa miaka miwili, tunaiomba sana Serikali, fedha za Mfuko wa Jimbo zilikuwa ndiyo uti wa mgongo wa kila Mbunge wa jimbo, tulifungua barabara na sasa kwa miaka miwili hatujapata. Tunaiomba sana Serikali iangalie utaratibu wa kurejesha fedha za Mfuko wa Jimbo ili tuweze kufanya kazi zilizokusudiwa na miradi ambayo sasa hivi ni viporo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni changamoto kubwa tuliyonayo ya miradi ya wananchi iliyoanzishwa. Maboma mengi nchini yameanzishwa na wananchi kwa michango yapata miaka mitano, sita, kwingine hadi kumi lakini hayajaendelezwa. Ninashauri kama inawezekana kutolewe maelekezo mahususi kwenye bajeti zetu tusianzishe miradi mipya kwenye halmashauri zetu tuchague ile miradi viporo halafu tuiingize kwenye bajeti kwa sababu wakati wananchi waliaanzisha hiyo miradi walikuwa na nia njema sana ya kuona namna pekee ya kuweza kuiunga mkono Serikali ni wao kuanzisha miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maboma ya afya, maboma ya elimu, maboma ya utawala, Ofisi za Serikali za Mitaa, Ofisi za Kata majengo hayo yamekaa muda mrefu yanasubiri Serikali ikamilishe. Ili Serikali ilikamilishe ni lazima halmashauri iweke kwenye mipango yake. Kwa huku juu tusingeweza tukafikia hiyo hatua. Ushauri wangu ni kwamba pengine maelekezo hayo yatatusaidia ili Mabaraza ya Madiwani na Madiwani kwenye maeneo yao wasianzishe miradi mipya zaidi ya kuunga mkono juhudi za wananchi ili tuweze kufanya mipango ya maendeleo kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Miradi ya TACTIC; Miradi ya Maboresho ya Miji Tanzania. Mbulu ni mnufaika, lakini tumekaa miaka sita tukisubiri hii miradi. Ushauri wangu kwenye hii miradi kuna miradi imeanzishwa na sasa ina wakandarasi, lakini ina muda mrefu. TAMISEMI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, ifanye uratibu wa miradi yote ya TACTIC ambayo iko kwenye miji na majiji ili iweze kukusanya na kujua kwa nini miradi hiyo imekaa muda mrefu na kwa nini haikamiliki na lini itakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ubabaishaji, tulipoenda unakuta mkandarasi amechukua mradi miaka mitatu, minne hajakamilisha. Ushauri wangu ni kwamba hii miradi tusipokamilisha wale wafadhili wa Benki ya Dunia hawatatupa fedha na miradi mingine haitafika kwenye maeneo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee ninapongeza Serikali ya Awamu ya Nne kuweka miradi hii katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ambayo ni halmashauri kongwe, wilaya kongwe, lakini hatuna stendi, hatuna dampo, hatuna machinjio wala hatuna soko. Ninaishukuru sana Serikali, kwa mpango huu tunaomba mradi huu uje kule Mbulu ili uweze kuwahudumia wananchi wa Mbulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ombi kwa Serikali.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia kengele ya pili imeshagonga.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa miradi hii tunaiombea fedha haiwezi kutekelezwa kwa mara moja na kwa kuwa mingine inasubiriwa kwa hatua kubwa, tunataka usimamizi uwepo karibu ili miradi hii kama ya Barabara iliyoko kule Mbulu kwa maana ya Karatu – Mbulu – Haydom imekaa miaka 10 ina kilomita mbili, ya ndani pale Garbabi mkandarasi alishaaacha na miradi kama hiyo inachafua taswira ya Serikali. Ninashauri kama inawezekana Serikali iwalipe hao wakandarasi, iwarudishe site waweze kukamilisha hii miradi kwa wakati ili miradi hii iweze kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine nitaandika kwa maandishi. Ninashukuru kwa kunipa nafasi na ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)