Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nianze na tatizo la ajira hapa nchini. Tunayo Mifuko ya Hifadhi za Jamii katika nchi yetu (PSSSF, NSSF, WCF) wamefanya kazi kubwa kutusaidia kupambana na tatizo la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, NSSF wana Kiwanda cha Sukari pale Mkulazi mpaka sasa wameajiri watu 10,172 wakiwemo indirect na direct employment, lakini matarajio yao itakapofika mwaka wa fedha 2027/2028, watakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 50,000 za sukari na wanatarajiwa kuwa na wafanyakazi 11,315 indirect na direct employees.
Mheshimiwa Mwenyekiti, PSSSF hao hao wana Kiwanda cha Ngozi cha kutengeneza viatu pale Kilimanjaro ambapo wana ubia na WCF wameajiri watu 4,237, lakini ikifika 2027 watakuwa na 7,000 ikijumuisha indirect na direct employment. Vilevile, wana Kiwanda cha Chai pale Mponde, Wilaya ya Lushoto wanaubia na WCF, wana ajira 3,208 lakini ifikapo 2027 watakuwa wameajiri watu 4,708.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii tumeshauri sana Mifuko hii kupanua wigo wa uwekezaji waende mpaka kwenye viwanda vya kuchakata Samaki, lakini pia kwa ajili ya geographical diversity wafikie na mikoa mingine ambako wanaweza wakapata fursa ili Watanzania wengi zaidi waweze kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifuko hii inazo changamoto; changamoto ya kwanza kwenye Mifuko ya NSSF na PSSSF ni madeni wanayoidai Serikali. Serikali iliwakopa matrilioni. Tunashukuru Serikali imeshaanza kulipa madeni, imepunguza lakini bado kuna madeni ambayo Serikali inatakiwa ilipe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninazungumzia ulipaji wa madeni haya? Watakapolipa madeni haya Mifuko hii licha tu ya kuwa na uhimilivu wa kuwalipa wanachama wao watakuwa na ukwasi kwa ajili ya kuongeza vitega uchumi ambavyo vitaongeza ajira hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kiwanda cha Ngozi na Viatu pale pale Moshi Kilimanjaro ambao wana ubia na magereza, PSSSF wana changamoto ya soko. Nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu ajaribu kukaa na majeshi badala ya kuwa na tender za kununua viatu kutoka nchi za nje China na kwingineko wawaelekeze kutengeneza soko la viatu kwenye kiwanda chetu waweze kununua viatu na hapo tutaongeza uzalishaji na hapo Mifuko hii itaongeza uwekezaji na hivyo tunaweza kusaidia ajira hapa nchini. Hata hivyo viatu wanaagiza China vingi huwa ni vibovu tu. Wanatumia siku mbili vinaharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye eneo la mapambano dhidi ya rushwa, dhidi ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma. Ukurasa wa 91 Mheshimiwa Waziri Mkuu ameripoti TAKUKURU wameweza kusaidia kuokoa shilingi 60,331,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, to be sincere Bunge hili la bajeti huwa Wabunge tunakuja hapa kutafuta fedha kwa ajili ya majimboni, kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata maji, wanakuwa na barabara nzuri, wanakuwa na zahanati, vituo vya afya, mahospitali, kunakuwa na ujenzi wa madarasa, shule za sekondari, msingi, lakini pia tunakuwa na uwezo wa kuajiri walimu, uwezo wa kuajiri watu kwenye sekta ya afya na ajira zingine. Yote haya yanategemea Serikali kuwa na fedha. Tunafanya kazi nzuri. TRA wanakusanya mapato mazuri, lakini pia Mheshimiwa Rais kwa ajili ya miundombinu mikubwa anakopa fedha ili tuwe na miradi ya kuwasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili, kila Wizara inaleta hapa bajeti yake ya makadirio ya mapato na matumizi. Kwa hiyo bajeti ina sura mbili. Ina sura ya mapato, ina sura ya matumizi. Ninataka nijikite kwenye eneo la matumizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna eneo ambalo sisi Wabunge ingewezekana tukakaa kutwa nzima hapa ndani tukazungumza na Serikali tukambana Waziri Mkuu ni kwenye eneo la matumizi na hasa matumizi mabaya, wizi, ubadhirifu na ufisadi ambao unasababisha wananchi walipakodi wasiweze kupata huduma za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwakumbushe kidogo tu Waheshimiwa Wabunge waone namna ambavyo hizi fedha zinavyochotwa kwenye masandarusi zingine sijui wanabeba kwenye madiaba na marumbesa, fedha nyingi. Niwapeleke tu kidogo kwenye mwaka wa fedha 2021/2022. CAG alitoa ripoti yake kwenye Mamlaka tu za Serikali za Mitaa, eneo moja tu ambako mafisadi walichota 637,550,000,000. Waheshimiwa Wabunge unajua fedha hizi zikitamkwa tu kwamba CAG amebaini kuna ubadhirifu tusipofanya hesabu kidogo kidogo hatuwezi kujua ni kiwango gani hayo mafisadi yamekuwa na nguvu. Kwa mfano, ukienda kwenye hizo bilioni tungeweza kununua Power Tillers kwa ajili ya wakulima ya horsepower nane yenye majembe yote kwa milioni saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna majimbo 222 na kama Power Tiller moja ingekuwa na wakulima tano kila jimbo hapa nchini lingekuwa na Power Tiller 2,050. Kwa hiyo kila Mbunge hapa ungekuwa na wakulima 2,050 wenye Power Tiller. Kwenye afya, zahanati moja Serikali tunajenga kwa milioni 90 yenye vifaa. Tuna majimbo 222, kwa fedha hizi tu kila jimbo hapa, kila Mbunge angekuwa na zahanati 32. Kwenye elimu kwa fedha hizo, darasa moja tunalijenga kwa milioni 25, tuna majimbo 222, kila Mbunge hapa jimbo kwake angekuwa na madarasa 115 na inawezekana ungekosa hata mahali pa kuyajenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maji, tunakadiria kisima kimoja hata kwenye mambo ya uchimbaji, casing ya miamba na nini ni kati ya milioni 15 mpaka 25. Ukichukua milioni 20 tuna majimbo 222, kila Mbunge hapa jimboni kwake angekuwa na visima 144 vya maji na kutatua tatizo la maji. Kwenye uvuvi, kizimba cha kawaida cha mita nane kwa mita nane na deep mita tatu ni milioni 20 chenye vifaranga 18,000 ambapo tungekuwa na wavuvi kwenye vikundi 25 kila kizimba, nchi nzima tungekuwa na vizimba shilingi 796,875 na hivyo wangepata mkopo wa kuwawezesha kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye bodaboda. Bodaboda moja King Lion inaweza kununuliwa kwa milioni tatu. Tuna majimbo 222. Kila jimbo lingepata pikipiki 957 na kama pikipiki moja ingekuwa na kikundi cha watu wawili kila jimbo lingekuwa na wenye bodaboda 1,914 lakini kwa fedha hizi hizi sikukuu ya mwaka mpya, tuko Watanzania milioni 64, kila Mtanzania tukiwemo na katoto kangepata shilingi elfu kumi kwa ajili ya sikukuu ya mwaka mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu, siku ile anateuliwa hapa alianza vizuri, nilimwona anatoa hotuba yake pale, nitapambana na wazembe, nitapambana na ubadhirifu, nitapambana na mafisadi, nikasema chuma hicho kinaingia. Baadaye ameenda kwenye Tume ya Maadili akasema wajaribu kufanya kila linalowezekana tujue watu wanaotuibia fedha. Nikasema chuma hicho! Songa mbele mtani wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa simsikii humu ndani kwenye hotuba hajajipambanua kupambana na haya majamaa, kama tumeweza kurudisha bilioni 60, hizi fedha zetu wamechukua, kwa nini hizi fedha wasirudishe? Mwibara hatuna maji, Mwibara barabara mbovu, wavuvi hawana vizimba, hakuna vituo vya afya vya kutosha, anashindwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaamini kitu kimoja tu Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi tumefika mahali kweli CAG anakagua na ameandika kwenye ripoti yake kwamba tumekutana na wizi, ubadhirifu halafu tena tunasema waende tena wachunguze, uchunguzi juu ya uchunguzi? Nikasema aaah! Ndiyo maana hata juzi niliona Azam wanacheza na Simba, Manula akishika mpira anampa beki James Akaminko, washambuliaji wanakimbia mbele wanageuka mpira hauji Akaminko anamrudishia Manula dakika 90 zinaisha ni suluhu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, ashambulie kabisa, Bunge tuko pamoja naye ashughulike na hayo majamaa. Inakuwaje mafisadi wanateka nchi hii? Wanaiweka mfukoni? Wakati yeye ana mamlaka? Watanzania fedha zinaibiwa bado wanataka kuchunguza, wanachunguza kitu gani? Mheshimiwa Mchungahela amenifurahisha sana leo hapa jioni anisubiri pale nimpe supu ya kuku."
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha, kengele ya pili tayari.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu choma, fyeka vichaka vyote vya mafisadi na hayo madalali yanayodalalishia makampuni ya mafuta, choma kabisa hayo ndiyo yanatuharibia, mafuta yanakuwa na shida hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)