Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia au kutoa maoni yangu kwenye bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kipekee nimpongeze Waziri Mkuu na Mawaziri wote ndani ya Ofisi yake, Manaibu Waziri na Watendaji wote ambao wanaendelea kufanya kazi ya kuwahudumia Watanzania hasa Ofisi hii kubwa kabisa ya TAMISEMI ambayo tumeipitishia takribani shilingi trilioni 12 walizoziomba hapa kwenye bajeti kwa sababu inagusa karibu kila eneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya, lakini kwa niaba ya Wanabiharamulo, miaka takribani mitatu nimekuwa nikisimama hapa mara nyingi kuongelea habari ya jengo jipya la halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninafurahi kukwambia tayari shilingi bilioni moja imeshaingia kwenye akaunti ya Halmashauri ya Biharamulo sasa na sisi tunajenga jengo jipya la halmashauri kwa sababu niliyataja kwa miaka mitatu mfululizo natakiwa nisimame kushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tarehe 4 Aprili, 2026, nadhani tumeona kwenye vyombo vya habari Biharamulo hatuna chanzo cha uhakika cha maji. Mheshimiwa Rais alipokuja Biharamulo tarehe 8 Juni, 2022, nilimwomba Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria na akamwelekeza Waziri wa Maji rafiki yangu Mheshimiwa Aweso akamwambia hakikisha wanapata maji hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasimama ndani ya Bunge hili kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na kumshukuru sana Waziri wa Maji na watendaji wake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya maana juzi tarehe 4 Aprili umesainiwa mkataba wa kuleta maji ya Ziwa Victoria katika Wilaya ya Biharamulo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 55.1 ambayo ni zaidi ya bilioni 140.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda kupata mradi mkubwa wa maji chini ya mkopo nafuu wa Serikali ya Hungary. Ahsanteni sana; ninaishukuru Serikali na wote waliohusika kwa ajili ya kuleta neema hii kubwa ya Biharamulo ambayo sasa na sisi kama ni ujenzi wa viwanda na vitu vingine vinaenda kufanyika kwa sababu substation ya umeme ipo na mambo mengine ya uhakika yapo pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisimame hapa pia kushukuru kwa bajeti ambazo zimekuwa zinaendelea especially kwenye upande wa TARURA. Tumejenga barabara nyingi sana katika bajeti hii iliyopita na tunaendelea kujenga barabara na tumeona kwamba hata bajeti ya TARURA imeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni heshima kubwa sana ambayo Wabunge hasa Wabunge wengi tunaotoka maeneo ya vijijini, Mheshimiwa Rais kwa mara nyingine ametuongezea tabasamu kwa sababu tunayo sababu ya kwenda kurudi kwa wananchi wale tuliozunguka katika uchaguzi wa mwaka jana tukiwaambia kwamba barabara zilizoahidiwa sasa zinaenda kutengenezwa kwa sababu kutoka shilingi bilioni 944 kwenda shilingi trilioni 1.2 na hela nyingi zimeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini sasa hata marejeo kwa sababu tulishapitisha tayari kwenye RCC zetu kule na Road Board. Kwa hiyo, tunaamini hili ongezeko wilayani kule wanaanza kulifanyia kazi. Kwa hiyo, tungeomba TAMISEMI pia yatakapoletwa huko Wabunge tuhusishwe kwa sababu sasa hivi tuko Dodoma hapa, hili ongezeko lisije likafanyika Mbunge hujui unaenda kule unakuta barabara ambayo hukuiombea wewe uliyeenda kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi kwenye Ilani imepitishwa tu na mtaalam kule. Kwa hiyo, tungeomba watakapomaliza kwa sababu tulisharudi huko hatuko majimboni walau tupate taarifa tujue ni barabara gani zimependekezwa Wabunge tunapokuwa tunaendelea wakati wa kupitisha bajeti ujue unapitisha kitu gani kwenye eneo lako. Hilo nilitaka niliombe namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo lingine kwa sababu hii ni Ofisi ya Waziri Mkuu, yako mambo ambayo ningependa kushauri ninajua Wizara nyingine zinakuja, lakini ninataka kuongelea habari ya umeme. Tumekuwa tunapata shida kidogo kwenye hii miradi ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta umeomba maji. Wizara ya Maji inajitahidi inakupelekea mradi wa maji. Unafika pale miradi hii mingi inatekelezwa vijijini. Ukifika pale wamejenga mradi mkubwa sana na mzuri wa maji. Tunatumia solar lakini vijiji vingine ni vikubwa. Sasa kumekuwa na shida kati ya TANESCO na watu wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mradi mzuri wa maji unaenda pale wananchi wanalalamika mradi hautoi maji kwa sababu umeme hamna. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba coordination pale ambapo Serikali; (hili jambo nilishalichangia kipindi cha nyuma) nikasema kwa mfano miradi yaani taasisi nyingi za Serikali unakuta wana mahitaji specific ya ardhi. Kwa hiyo, zile taasisi haziwezi kukaa pamoja na wananchi unakuta ziko pembeni. Kama ni zahanati au kituo cha afya kinajengwa pembeni, kama ni shule ya sekondari inajengwa pembeni kwa sababu wanahitaji maeneo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa umeme unaoletwa vijijini ule wa nguzo 40 au nguzo 60 ukitaka upeleke kwenye taasisi, wananchi wanabaki bila umeme. Ukitaka upeleke kwa wananchi basi taasisi zitapata umeme. Sasa tungeomba tuje na package maalum ya kupeleka kwenye shule za sekondari, kupeleka kwenye vituo vya afya, kupeleka kwenye vyanzo vya maji hiyo isihusike kabisa na masuala haya ya REA inayoenda kwenye vitongoji au vijiji ili iweze kutusaidia vile vyanzo vipate maji kwa ajili ya kuhudumia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haipendezi Serikali inaweka pesa pale zaidi ya shilingi milioni 400 au 500 halafu mradi hauzalishi wala hautoi maji, ni kama ile pesa imetupwa pale. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba hilo liangaliwe waweze kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo ambalo nilikuwa nalipitia hapa. Wote tunajua kwa sera mpya ya elimu vijana wetu wanaanza kuishia darasa la sita. Kwa hiyo, tunategemea mwakani 2027 kutakuwa na darasa la saba wanaomaliza na la sita wanaomaliza. Sasa ukiangalia la saba na la sita hawa tuna takribani ya average ya watoto 1,500,000 kwa kila darasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakuwa na increment ya watoto takribani 1,545,330 ambao wamefanya mtihani wa darasa la nne mwaka huu na mwaka jana wote wanaenda kumaliza darasa la saba. Sasa wanapomaliza darasa la saba kitakachojitokeza ni nini? Tutakuwa na watoto wengi wanaoingia form one kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba Serikali ilichukue hili. Ukipiga average ambayo sio standard kwamba kila darasa libebe watoto 60. Tunahitaji vyumba 25,756 vya ku-accommodate hawa watoto wapya. Tunajua watoto wengi wamekuwa wanaenda private. Sasa private huwezi kuishtua private sector ikaanza kujenga vyumba vipya na ku-accommodate watoto wengi namna hiyo. Kwa hiyo watoto wengi tutegemee Serikali itawabeba kwa sababu kama private ina limit ya kutaka wafanye comfortability ya watoto walio nao wasi-fail waweze ku-acommodate na huku Waziri Mkuu alishaelekeza ndani ya Bunge hili kwamba elimu ya sekondari ni elimu ya lazima hakuna kuishia la saba tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulione hili tuanze kupanga kadri tunavyoenda haraka kwa sababu kwenye bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2027/2028 kujenga yaani kujenga madarasa haya yote kwenye bajeti moja bado mzigo utakuwa ni mkubwa kwa Serikali. Kwa hiyo, ninachotaka kushauri tunayo maboma ambayo yamekaa muda mrefu, basi tusaidieni kuyamalizia yale maboma ili tuweze kupata idadi ya vyumba vya madarasa vitakavyotakiwa kwa wakati ule itusaidie ili hatimaye watoto hao wanapokuja form one wakute madarasa yapo na hali kadhalika wakute walimu wapo kwa ajili ya kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha kitu kinachoitwa mahusiano kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Tuna Wizara ya Ajira, Kazi na Mahusiano. Sasa kwa sehemu kubwa tumekuwa tunaona matatizo mengi yaliyoko Serikalini. Huyu anatamka cha kwake hiki, huyu anatamka cha kwake hiki, kwa sababu there is no proper communication. Kuna kipindi mtu mwingine anakaa ofisini anasubiri bosi wake aanguke ile apande cheo. Huyu anasubiri ni ajali tu za kawaida na hata humu ajali za siasa si tunazijua, tunapigana ajali humu? Kwa hiyo, hizi ajali zipo. Hii Wizara ya Mahusiano tunaomba ifanye kazi ya kuponya mioyo ya watu walioumia ili utendaji wa Serikali uweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niongelee suala la mafuta ninapomalizia. Bahati nzuri siku ile nilitaka kutoa hoja hapa tukapata taarifa, maelekezo ya Spika tunayaheshimu na tunakubali kabisa, nimeenda mpaka kwenye Kamati kule nimeongea ingawa siyo mjumbe wa Kamati hiyo tuliruhusiwa kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kimoja ninajiuliza, aliyekaa pale akatamka kwamba tuna stock ya mafuta ya miezi mitatu what was his intention? Yaani anatamka, taharuki ikianza wataalamu ndiyo wanakuja kukuelezea…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie. Wataalam ndiyo wanakuja kukuelezea kwamba maana ya hiki ni hivi na maana ya hiki ni hivi. Tunaomba wanaotoa matamko Serikalini watoe matamko kwa kutoa maelezo, mbona baadaye Watanzania wamejaribu kuelezwa na wameelewa kwamba mafuta hayako yote hapa. Yanakuwa yanakuja yote yanahesabika kama yanakuja, lakini aliyetoa tamko mara ya kwanza anaichonganisha Serikali, anatuchonganisha Wabunge na wananchi kwa sababu kila mwananchi alijua mafuta yapo kumbe mafuta yale yanayoelezewa mengine yapo kwenye meli, mengine ndiyo yamewekewa order hayajaja, yote ile ndio combination ninayosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba wanaotoa matamko Serikalini, kama ni mtendaji huna experience ya kuongea, sisi wanasiasa tuna experience, Waziri yupo ana experience ni mwanasiasa, waacheni wanasiasa waongee na wananchi kwa sababu wana uzoefu wa kuongea na wananchi wanawaelewa kuliko mtendaji mmoja anatoa tamko, anatoa taharuki kwa chama, anatoa taharuki kwa Bunge, anatoa taharuki kwa nchi na hatumwoni akirudi tena kutoa maelezo yale kwamba nilikuwa ninamaanisha kitu fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kushukuru sana na naunga mkono hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)