Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa nafasi hii, lakini kipekee kabisa ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na leo kupata nafasi hii ya kuendelea kuchangia kwa lengo la kuishauri Serikali na watu wengine wote kwa maana ya wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajielekeza katika ukaguzi wa hesabu kwa maana ya audit. Ninajielekeza hapa kwa sababu ni eneo muhimu sana katika mipango yetu yote tunayoifanya. Hii mipango tunaifanya kwa sababu tayari tulishatumia huko nyuma na matumizi ya kule nyuma bila shaka tungetamani kujua yametumika vipi, lakini wapi turekebishe, wapi tuweze kuongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kuongelea hapa kwa sababu tumekuwa na jukumu muhimu kama Wabunge kwamba ni jukumu letu kufanya ukaguzi. Ninataka niwakumbushe kwamba jukumu la ukaguzi ni la Bunge na wala siyo jukumu la CAG kama miongoni mwetu tunavyodhania na kufikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa sana au kumekuwa na tabia zikijitokeza mara nyingi za kuona kwamba jukumu hili ni la CAG, lakini pia kumejitokeza tabia ambayo imejengeka ya kuanza kumlaumu na kumshambulia CAG kwa madai kwamba, eti kwamba anaifedhehesha Serikali au kwamba anakifedhehesha chama au anakishambulia chama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme kwamba dhana hii ni potofu, dhana ya ukaguzi kwa maana ya auditing, dhana hii ni dhana ya utawala bora. Kwamba Serikali haiwezi kujiangalia yenyewe baada ya kuwa imetimiza majukumu yake, lazima kuna chombo cha kutazama au kuisimamia, kuishauri na jukumu hilo la kuishauri na kusimamia Serikali ni jukumu la Bunge. Sasa Bunge ndiyo chombo chenye kufanya ukaguzi au chenye kuisimamia Serikali kuangalia mambo gani yamefanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG hapa anakuja kama jicho la Bunge tu, jicho kazi yake ni kwenda kuangalia na kuona nini kimefanyika, linatoa taarifa kwa mwili, kwa maana mwili ni Bunge, kwa namna yoyote ile tukijaribu kuangalia audit procedure sioni sehemu ambapo CAG anapaswa kulaumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kwanza kabisa ambacho kinafanyika ambacho ni cha muhimu kabisa kabla auditor hajaenda kufanya jukumu lake la kaguzi, kuna kitu kinaitwa audit plan, anafanya audit plan. Kwenye audit plan hii sisi kama Bunge ndiyo tunamwambia kwamba tunataka ukakague hapa, pale, pale; na kwa sababu hii, hii, hii. Kwa hiyo auditor yeye atamtaarifu mkaguliwa, kwamba nitakuja kukagua na maeneo ambayo ninatarajia kukagua. Baada ya taarifa hii maana yake kwamba mkaguliwa tayari anajua maeneo ambayo atakaguliwa, nyaraka zipi na vitu gani vitahusika, vitahitajika katika ukaguzi huo; wa hiyo analo jukumu la kujiandaa kwa kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofuatia maana yake kutakuwa na entrance meeting. Auditor ayakavyokwenda pale atakuwa na kikao na management kuhusiana na jukumu hili la ukaguzi. Baada ya kikao hiki bila shaka kutakuwa na uwazi kabisa kwamba nini kitahusika, nani atahusika na kwa sababu ipi na kwamba mkaguzi atakaa muda gani katika eneo hili la ukaguzi, na atataka nini na vyote vitakavyohitajika katika eneo hili. Sasa, baada ya hapo kazi ya ukaguzi itaanza. Akiwa field auditor atahitaji taarifa zote kwa ajili ya kupata ushahidi. Ataanza kutafuta ushahidi aidha kwa kutumia nyaraka zilizokuwepo au atahoji baadhi ya watu wanahusika na ukaguzi huu. Lengo lake ni nini, kuja kufanya conclusion baadaye kule; kwa maana ya kuweka audit opinion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya taratibu hizi baadaye auditor ataandika barua kwa management; management letter. Kwenye barua ile atamwambia maeneo ambayo ameona kama kuna changamoto au kuna kitu chochote kinahitaji clarifications. Haya yote ni kwa sababu ya kumfanya mkaguliwa awe huru na kutoa ushahidi wote unaostahili kuhusiana na ukaguzi ule na yale mambo yaliyoonekana. Baada ya hapo sasa, baada ya kuanza kupata taratibu hizo zote na kuanza kuandika hizi drafts za auditing na kumaliza atakaa na mkaguliwa, kutakuwa na exit meeting. Mkutano huu ni muhimu sana, ni mkutano ambao auditor na mkaguliwa watakaa kujadili mambo yote yaliyoonekana kama ni kinzani, utatuzi wake na kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo mkaguliwa atatoa ushahidi wote, kwamba hili bwana uliloandika hapa kwamba hujaona au hiki ulichoona kwamba ni shida hiki siyo shida ni moja, mbili, tatu, nne, tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sasa, auditor anavyotoka pale akishaandika ripoti, ile ripoti ni conclusive, ripoti ambayo imekamilika, ambayo haina shaka kabisa. Sasa kumekuwa na kauli, akitoka pale baadhi ya watu kwa makusudi kabisa au kwa kutokujua wanakuja kudai kwamba kutakuwa na ripoti, ripoti ambayo ni kinzani, tofauti na ile ambayo auditor ameiandika pale. Kwamba hiki kilichoandikwa kimezungumzwa tu, kuna bado, kuna nafasi, kutakuwa na maelezo ya hivi na vile; kana kwamba kama ile ripoti iliyotolewa pale haijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kutoa uelewa huu kwa lengo gani; kwamba sisi ambao ndiyo tunaouhusika na ukaguzi huu, kwa maana ya Waheshimiwa Wabunge, tuwe tunafahamu kwamba ukaguzi huu maana yake ni nini, lakini wapi role yetu inatakiwa ku-play kwa lengo la kufanya ukaguzi huu uwe wenye tija. Kwa sababu ukaguzi huu ndiyo mwanzo wa safari ya kufanya mipango mingine ya ukaguzi unaokuja mbeleni. Kwa hiyo tunayo sababu ya kufanya kazi na kuhakikisha kwamba ukaguzi huu uliopo unafanyiwa kazi katika kutatua changamoto zilizokuwepo katika kuifanya Serikali kwenda na yale mashauri au ushauri waliopewa na auditor kutokana na yale yaliyoonekana kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lengo hili kusudi liweze kutimia ni kama hivyo nilivyowaambia ndugu zangu, kwamba sisi Waheshimiwa Wabunge tuna nafasi kubwa sana ya kuufanya ukaguzi huu uwe wenye tija. Hakuna mtu mwingine yoyote atakayeufanya huu ukaguzi ukawa wa maana kama siyo sisi kwa sababu ukaguzi huu ni wetu sisi na huyu CAG sisi ndiyo tuliomtuma aende kufanya ukaguzi hu, aje ili tuone kwamba kuna nini na kitu gani turekebishe, tuishauri Serikali na kusimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)