Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti ya Waziri Mkuu. Nimeisoma imegusa maeneo mengi sana ya kimkakati, kama tutaitekeleza na niombe nitamke kwamba imeakisi malengo ya MKUMBI II, 2025 - 2050. Ninaipongeza Serikali kwa kuja na huu mkakati ambao kusema ukweli kama tutautekeleza ipasavyo tutakwenda kuingia kwenye uchumi wa kati wa juu ambayo ndiyo malengo mahsusi ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwa kuendelea na kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inalenga kuchochea, nina hakika miradi hii ndiyo itatusaidia kutekeleza malengo ambayo yamezingatiwa kwenye MKUMBI II. Ninaona SGR, Dar es Salaam - Dodoma na ujenzi unaoendelea kwa hivi vipande vilivyobaki kutoka Dodoma - Tabora, Tabora - Kigoma, Kigoma – Isaka, niiombe Serikali tukamilishe. Tunapokamilisha haya ndiyo tunakwenda kupata tunachokiita uchumi jumuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi na makubwa yamefanyika kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, niishukuru Serikali kwa kuwekeza pesa nyingi kwenye mawasiliano, kwa sababu tunapoongelea uchumi, tunaongelea usafirishaji, miundombinu na mawasiliano. Ninashukuru kwa minara ambayo imejengwa na mingine inakwenda kuzinduliwa na Rais, nimeona tarehe 10 mwezi huu. Ninaiomba Serikali nchi nzima kuhakikisha kwamba tuna mawasiliano ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru dada yangu Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano, pale kwangu Muleba tumejenga minara zaidi ya nane, ninaishukuru Serikali, kuna maeneo ambayo yalikuwa kusema kweli hatuna mawasiliano, mpaka upate mawasiliano upande kwenye kichuguu au upande kwenye mti. Ninamwomba Waziri, pale kwangu Muleba Kata ya Kyebitembe tumejenga mnara, lakini kuna maeneo ambayo yako chini ya bonde hayapati mawasiliano, bado tupo kule ambako Mheshimiwa Rais na Serikali inataka kututoa, ni maeneo madogo ambayo tunahakikisha kwamba ile minara ambayo tumeijenga pale tuiongezee nguvu ili lengo ambalo Serikali imekusudia kwa wananchi wake liweze kutimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, minara imeshajengwa tunashukuru na kazi kubwa imefanyika, ninaishukuru Serikali kwenye suala la mawasiliano hili sina shida ninajua Waziri ni msikivu, hili atakwenda kutufanyia na wananchi wa Kyebitembe wanasikia, Waziri ni mtu wetu wa nguvu, anafanya kazi nzuri, ninaomba na pale Kyebitembe wamwone na awatembelee siku moja wamwimbie ‘akasimbo’ pale lakini wapate na mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya kilimo, wakati tunajadili MKUMBI II, Waziri Mkuu alikuwa mgeni rasmi tuliwaita Wakuu wa Mikoa, ma-RAS, wakaitwa Wenyeviti wa Halmashauri, ilikuwa ni kazi nzuri sana, inakwenda kutusogeza tunapotaka kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya kilimo, pia kwa Mkoa wangu wa Kagera, zao letu kubwa hasa kwenye Wilaya ya Muleba ni zao la kahawa, kahawa inayozalishwa ninaomba niseme, asilimia kubwa inatoka Wilaya ya Muleba, ninakuomba Waziri Mkuu ukipata nafasi ukatutembelee pale Muleba, wananchi wamechangamka wanapanda mibuni kama tumeanza upya. Siku za nyuma tuling’oa mibuni kwa sababu bei ilikuwa imeshuka, kahawa ikaonekana si jambo lolote, lakini kwa miaka ya nyuma ndiyo imetusomesha, sasa kuna wave mpya ya watu kupanda mibuni. Niiombe TAMISEMI itoe maelekezo kwa Wakurugenzi wote hasa kwenye maeneo ambayo tunapanda kahawa tuna tatizo la miche.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wilaya yangu ya Muleba kupata miche imekuwa ni kizungumkuti, tunao mgao mdogo ambao hautoshelezi mahitaji ya wananchi, niombe Ofisi ya Waziri Mkuu, watoe tamko kwenye maeneo ambayo yana vichocheo, watu wana-appetite ya kulima tusiwakatishe tamaa. Kwa hiyo, kazi ya Serikali kama ambavyo imeshaanza iwape miche ya kutosha, iwape mbolea ya kutosha, tukapambane na majirani zetu ambao wanazalisha kahawa nyingi wakati wana eneo dogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wamejitoa, nadhani kazi ya Serikali tusirudi nyuma. Katika Wilaya ya Muleba tunatumia nguvu sana wakati wa kuvuna, kupambana na watu ambao wanafanya uchuuzi, hii naomba Ofisi ya Waziri Mkuu mtusaidie Muleba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kyerwa wamefanya vizuri sana, natumaini Waziri wa kilimo atakuwepo hapa. Kyerwa wanafanya vizuri sana miaka ya nyuma pale Muleba kulikuwa na mfuko unaitwa nyantalo ritolwa, mkulima kama ana shida, anayo kahawa yake, alikuwa anakwenda kwenye AMCOS wanampa pesa, akivuna akapelekea kwenye chama cha msingi ile hela wanakata, ile nyantalo ritolwa tulipoanza kucheza nayo hakuna chama cha AMCOS ambacho kina pesa ya kuwasaidia wakulima ambao wanayo kahawa lakini msimu haujafunguliwa, matokeo yake wanatokea watu wa katikati pale, ambao ni wachuuzi ambao tunapambana nao. Ninashauri Serikali yangu sikivu twende Muleba pale, yale tuliyofanya Kyerwa na Muleba tukayafanye, wale ambao ni wachuuzi tuwasajili wajulikane walipe kodi, tuwape na leseni, lakini ile biashara irasimishwe na tuje na utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona Kyerwa wanafanya vizuri, Mheshimiwa Bashe akiwa Waziri wa Kilimo alifanya vizuri sana. Ninamwomba na Waziri wa Kilimo aende Muleba atusaidie pale, yale tuliyoyafanya Kyerwa tuyalete Muleba ili wananchi wafurahie jasho la kazi yao bila kubugudhiwa na bila kupoteza mapato ya Serikali na bila kufanya magendo. Tusipokuja na mfumo huo magendo yataendelea na tutaendelea kupambana na wananchi pasipo sababu yoyote ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvuvi, Muleba kwetu na Mkoa wa Kagera kama ilivyo kwa mikoa mingine, kazi ya uvuvi ni kazi ya kuwaingizia wananchi kipato na ndiyo sekta zinazotusaidia kujenga uchumi jumuishi, kwa sababu zinahusisha watu wengi kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tulilonalo na tumeliimba miaka nenda rudi, ni uvuvi haramu, nashauri Wizara ya Uvuvi tukaunde mamlaka ya uvuvi ambayo itasaidia kupambana na uvuvi haramu ili maziwa yetu, mito yetu, bahari zetu ziwe na samaki badala ya kuwa na maji ambayo hayatusaidii sana kwa sababu tuna mito, tunahitaji samaki kwenye maziwa yetu, tunahitaji samaki kwenye bahari yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo usinigongee kengele, ninaunga mkono hoja na ninakushkuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia. (Makofi)