Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ninaanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kupata nafasi hii ya leo. La pili, ninasema kwamba, ninampongeza sana Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa uwasilishaji wa taarifa nzuri na bajeti ya ofisi yake. Taarifa hiyo inaonekana kabisa imebeba maono makubwa na mipango mikubwa ya Serikali kwenye kila sekta. Tuna uhakika, kama itasimamiwa vizuri nchi yetu itazidi kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuwapongeza na kuwashukuru sana Mawaziri wa Sekta mbalimbali, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu. Mkuu wangu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, pamoja na Mkuu wangu wa Wilaya kwa sababu, wanasimamia vizuri utekelezaji wa majukumu mbalimbali miradi ya maendeleo katika eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii pia, kumpongeza na kumshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyoendelea kusimamia uhimilivu wa Serikali hii katika kutekeleza majukumu mbalimbali kwenye miradi ya maendeleo na shughuli za kijamii. Pia, ninachukua nafasi hii kumpongeza Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais, kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka kuwa, tarehe 17 Julai, 2025, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amezindua Dira ya Mwaka 2020 - 2025. Katika mipango yetu tunayoipanga sasa hivi tuna uhakika kwamba, kuanzia tarehe Mosi Julai, tutaanza kutekeleza sehemu ya dira hii, ambayo tutaenda nayo kwa kipindi cha miaka 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dira yetu tumepanga kwamba, mpaka kufikia 2050, pato la Taifa litakuwa limefikia kiwango cha dola trilioni moja, lakini pia, mchango wa Sekta Binafsi katika pato la Taifa tutakuwa tumefikia 70%. Sasa, ili kuweza kuijua dira yetu ya miaka 25 na kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba, tunaitekeleza, ninaiomba Wizara ya Mipango na Uwekezaji iweke mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali ambao watatusaidia kusimamia na kuhakikisha kwamba, dira hii inatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika nchi mbalimbali kwa mfano, majirani zetu wa Nchi za Afrika Mashariki wamezingatia na kutumia sana sekta binafsi ili iweze kusaidia kuhakikisha kwamba inachangia kwa kiwango kikubwa katika pato la Taifa. Kwa mfano, ukichukua ndugu zetu na majirani zetu wa Kenya, pato la Taifa linachangiwa kwa 55.94%, wenzetu wa Uganda pato la Taifa linachangiwa na sekta binafsi kwa 80%, lakini wenzetu wa Rwanda sekta binafsi inachangia 55%, wenzetu wa Burundi 17%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi Tanzania ukiangalia kwa mwaka 2025 sekta binafsi zimechangia katika pato la Taifa 21%, mikakati yetu ifikapo 2050 tuweze kuchangia 70% kwa kupitia sekta binafsi. Katika mchakato huo niiombe sana Wizara na Ofisi yako Waziri Mkuu uendelee kusimamia kuhakikisha tunaweka miundombinu safi, pia tunatengeneza njia mbadala ambayo itasaidia sekta binafsi kufanya kazi yake vizuri na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika taarifa ya Waziri Mkuu amesema katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 miradi 927 imeorodheshwa, ambayo ina thamani ya dola za Kimarekani bilioni 11.08 imesajiliwa na tunategemea katika miradi hiyo ikitekelezwa nchi yetu itaweza kuingiza dola za kimarekani milioni 672. Hiyo ni mipango mizuri na niiombe Serikali iendelee kusimamia ili kuhakikisha kwamba tunaanza kutekeleza mpango wetu wa Dira ya 2050 kwa speed kubwa kuliko hata ilivyopangwa huko nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mikakati mikubwa sana ambayo Serikali imeendelea kuweka katika kutekeleza miradi mbalimbali na kuzingatia kwamba tunafikia malengo ya dira yetu, lakini ninaomba niishauri Serikali katika maeneo matatu. Eneo la kwanza kama nilivyoanza kusema, ni kuhakikisha kwamba tunasimamia sekta binafsi ili iweze kuzalisha na kujenga miundombinu mbalimbali kwenye mipango na miradi ya maendeleo ili tuweze kufikia malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ukiangalia matumizi makubwa ya fedha za Serikali inatumika kununua bidhaa za chuma kutoka nje. Ukiangalia katika hesabu za mwaka 2025 Serikali ilitumia dola za Kimarekani milioni 738 kwa ajili ya kuagiza chuma kutoka nje. Ili kuweza kuondokana na changamoto hii, ninaiomba Serikali iweke msisitizo na kuhakikisha kwamba tunaanza kutekeleza Mradi wetu wa Chuma wa Liganga ili tuweze kuzalisha chuma tuweze kukitumia kwenye mambo mbalimbali ya maendeleo na kujenga miradi mbalimbali na iweze kusaidia kuokoa fedha ambayo inatumika kuagiza chuma, iweze kufanya kazi zingine na kuendeleza miradi ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mafuta tumeona kabisa kwa mwaka 2025, Serikali ilitumia dola za Kimarekani bilioni 3.16 kuagiza mafuta na bidhaa zinazoendana na mafuta, lakini sisi tunayo faida kubwa katika nchi yetu, tunayo gesi ya LNG ambayo inazalishwa katika Mikoa ya Kusini. Kwa hiyo ninaiomba Serikali katika kipindi hiki cha mpango wa Dira ya miaka 25 tuhakikishe kwamba tunasimamia na kuzalisha gesi kwa wingi ili tuweze kutumia katika majukumu mbalimbali ya kuzalisha umeme, kuendesha magari pia na matumizi ya nyumbani. Tukizingatia kufanya hayo tutapunguza sana kuagiza bidhaa hii ya mafuta kutoka nje na itatusaidia fedha hizo kuweza kutumia katika kutekeleza miradi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwenye sekta ya kilimo, wakati Waziri Mkuu anawasilisha taarifa yake alieleza bayana kwamba, Serikali imefanya mambo mazuri nasi tumeyaona. Kwanza, imetoa ruzuku ya pembejeo na kuhakikisha kwamba pembejeo zinapatikana kwa wakati pia uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara unaendelea. Serikali pia imeendelea kutoa mbegu bora pamoja na ruzuku kwenye mbegu, Serikali imeendelea kupima afya ya udongo na imeendelea kusimamia na kuhakikisha kwamba wananchi wanazalisha chakula cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo, kuna agizo lingine ambalo Waziri Mkuu alilitoa kwenye taarifa yako kwamba, kuzingatia kwenye vipimo wananchi wasiuze mazao ambayo yapo kwenye lumbesa, vilevile wananchi wasikopwe mazao yao. Katika taarifa ya Waziri Mkuu, ukizingatia mwaka 1974, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliandika kitabu kinachoitwa ‘Mtu na Maendeleo’, katika kitabu kile ilizingatia kwamba inatakiwa ili kuweza kupata maendeleo ni lazima tuzalishe chakula cha kujitosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika takwimu zetu uzalishaji wetu wa chakula ni tani milioni 22, lakini matumizi yetu ni tani milioni 18. Kwa hiyo, kuna ziada ya tani 30 ambazo zinazidi katika uzalishaji huo, sasa niseme kwamba naona kwamba muda umenipita, lakini nisisitize kwamba Serikali isimamie kuhakikisha kwamba inaimarisha masoko ya ziada ya chakula kinachozalishwa na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi wa Ruvuma wamekopwa mahindi yao na Serikali, mpaka sasa hivi hawajilipwa fedha zao. Sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu aliposema wananchi wasikopwe na vyama vya ushirika, lakini leo wananchi wale wamekopwa mahindi na Serikali, kwa hiyo nimwombe asimamie ili wananchi wale waweze kulipwa na waweze kuendelea kuzalisha mahitaji mengine kwa ajili ya chakula pia kwa ajili ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)