Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika ofisi hii nyeti kabisa ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi Wakristo kwenye Maandiko Matakatifu, kwenye Biblia, Bwana Yesu ametufundisha somo la kumshukuru Mungu kwa kila jambo. Somo hilo tunalitafsiri pia, kwenye maisha ya kawaida, tunafundishwa kuwa na moyo wa shukrani kwa kila jambo ambalo Mungu ametutendea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa salamu hizo ninaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama Cha Mapinduzi kwa namna ambavyo, kwenye jimbo langu, kwa kiwango kikubwa wamejitahidi sana kuwasaidia walipakodi wa jimbo langu katika Sekta ya Elimu, Afya, Maji, Miundombinu, Kilimo, pamoja na sekta zingine. Ninaishukuru sana Serikali, wananchi wangu wanashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo bado ninamwomba kaka yangu, Profesa nguli kabisa, Waziri wangu, mtu mnyenyekevu na kwa kweli, ninampongeza amepata Manaibu Waziri wanyenyekevu sana. Ninamwomba Profesa, Jimbo la Ikungi Magharibi ni jimbo lenye jiografia ngumu sana, kuna watu wanatoka kilomita 240 kufika Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilipoingia madarakani mwaka 2015 jimbo langu lilikuwa na zahanati kama saba za vijiji, lakini tulianza juhudi na wananchi tukajenga maboma ya zahanati karibu jimbo zima. Kwa kweli, ninaishukuru sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, wametusaidia kutuletea fedha tukayamaliza yale maboma. Ninamwomba sana kaka yangu Mheshimiwa Shemdoe, wananchi wa Jimbo la Ikungi Magharibi kuna Kijiji kinaitwa Mayaha, tumejenga boma la zahanati kwa miaka nane sasa, tunaomba Serikali watuletee fedha tumalize boma la walipakodi hawa. Ninamwomba sana Naibu Waziri aandike hicho kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Kijiji pia kinaitwa Mwankalaja. Mimi nilipoingia madarakani, kama Mbunge, nilianzisha harakati za ujenzi wa shule ya msingi, tukajenga shule kwa kujikongoja kwa kutumia fedha za jimbo. Hali ya hewa ya kule, sisi tunapakana na Bonde la Wembere, shule imesombwa watoto wana miaka miwili hawana shule. Nilikuja Wizarani nikakaa na wataalam nikawaomba watuletee fedha tujenge shule ya msingi. Ninamwomba kaka yangu Mheshimiwa Shemdoe, watoto hawa wa Kitanzania wanakosa haki ya msingi ya kwenda shule. Ninajua Serikali yetu imefanya mambo mengi makubwa, ninaomba Shule ya Msingi Mwankalaja itengewe fedha tuweze kuikamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, hili kwa sababu, nimefurahi nilisema nitalizungumza, lakini imemwona Waziri Mkuu pia, ameingia. Kwa sababu, Waziri Mkuu ana-coordinate Serikali yote ninaomba, tuna Barabara ya kutoka Singida – Sepuka – Ndago – Kizaga, barabara hii inapita katika kata karibu nne za Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba tuletewe fedha ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Tulifanya sherehe kubwa tukawaalika wananchi wakajaa, lakini barabara hii haikujengwa mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe ushauri wa jumla katika Sekta ya Nishati, ambayo pia, ipo coordinated chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa ninakiri Serikali yetu imechukua hatua za makusudi na kimkakati kuhakikisha kwamba, Taifa letu linabaki salama katika upatikanaji wa mafuta, excellent work, kazi njema sana. Ninaipongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua hizo nzuri zilizochukuliwa, sisi kama Wabunge, sisi kama sauti ya wananchi, tuna sababu ya kuitaka Serikali na kuishauri iende hatua 100 mbele, ili kupunguza mzigo mkubwa wa walipakodi wa Tanzania katika dhahama ya kipindi hiki cha mafuta. Ninamwomba na ninatoa ushauri kwa Serikali, pamoja na hatua nzuri walizozifanya wenzetu wa TPDC, wamefanya kazi nzuri sana kuhakikisha kwamba, tunapata uhakika wa mafuta ya mwezi Mei, Juni na Julai, ni jambo jema sana TPDC wamelifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua wanaweza wakakutana na mazengwe mengi sana kwa sababu, ninajua biashara hizi zinawapa watu wengi faida. Wakati mwingine watu wanaweza wasipende sana kuona kwamba, Watanzania wanashushiwa mzigo wao, wanataka wa-maximize profit bila kujali Taifa linaumia kwa kiasi gani kwa maana tuna taarifa, hata juzi baadhi ya meli zilitaka kuanza kuwa diverted; zilikuwa zinaleta mafuta, wakataka kuzi-divert, ili kusudi kuumiza watu, wao wa-maximize profit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza sana Wizara. Nina taarifa wametoa maelekezo meli zishushe mafuta nchini ili kuwashushia Watanzania mzigo, ninawapongeza sana Wizara. Huo ndiyo uzalendo, huko ndiko kulipenda Taifa, huko ndiko kuipenda nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa ushauri, ninaiomba Serikali, kwa nini tusijenge storage facility ambazo tutakuwa tunaweka mafuta mengi nchini, wakati wa dharura kama huu unapojitokeza tunaweza tukachukua mafuta hayo na kuyatumia na kuyauza kwa nchi jirani, hili tumewahi kulizungumza hapa Bungeni. Tunashindwa nini sisi kuwa hub ya kuwa na akiba ya mafuta na kuweza kuuza Zambia, Mozambique pamoja na nchi nyingine zinazotuzunguka? Tunashindwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mungu ametupatia nchi ambayo ipo katika mikakati ya kijiografia ambayo tuna uwezo wa kufanya hivyo na kujikuta akiba tuliyonayo, tukipata shock kama hizi tunajikuta kwamba, Taifa letu haliingii katika matatizo. Kwa hiyo, ninatoa ushauri Serikali, Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninamwomba kaka yangu achukue point tano muhimu wakati huu, achukue point tano muhimu. Mheshimiwa Waziri Mkuu aende akakate matumizi ambayo hayana umuhimu, yote ya Serikali kuanzia mwezi Aprili, Mei mpaka Julai, fedha zitakazopatikana aweke ruzuku kwenye mafuta, mafuta yashuke bei, tuwasaidie Watanzania waweze kupata unafuu ili kusudi uchumi wa Taifa usiweze kuyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu, afanye Rais wetu aendelee kuwa popular President kwa kufanya matukio ambayo yatawagusa Watanzania. Hapa tukitaka kumung’unya maneno tutakuwa hatumsaidii huyo Rais, ambaye tunasema kwamba, tunampenda. Kumsaidia Rais wetu ni pamoja na kutoa ushauri wa kijasiri, Serikali wachukue hatua za kimkakati za kuhakikisha, kama itashindikana hata baadhi ya tozo waziondoe wakati huu, ili Watanzania wapate matunda ya kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan kwa kishindo kikubwa katika uchaguzi uliopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu akapunguze posho za Serikalini huko baba yangu, akaondoe vikao ambavyo havina tija wakati huu, ili fedha watakazoziokoa waziweke ruzuku kwenye mafuta tuweze kuwasaidia Watanzania. Watu wetu wa TPDC tayari wameshachukua hatua kuhakikisha kwamba, mafuta safari hii yanaagizwa na taasisi yetu ya Serikali ili kusudi tusiwe na mashaka kwamba, mafuta yanaweza yasiwepo nchini. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hiyo, hilo ninatoa ushauri na ninakwambia, ukienda kulifanya utaona nchi itakavyotabasamu na atakuwa amechukua point tano muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza sana kuhusiana na mambo mazima ya bulk procurement. Hivi kwa nini tusifike muda, tulikuwa na nia njema kwenye bulk procurement, turuhusu kampuni nyingi zi-compete kwenye mafuta kwa sababu, ukiangalia kwa trend ya sasa hivi ni only kampuni nne tu. Hizi zote ukifuatilia kwa undani, ukisoma, wanafanya ma-cartel, bei ya mafuta inakuwa kama vile watu wanaipanga. Kwa nini tusiruhusu katika Taifa letu kampuni nyingi ziruhusiwe kuingiza mafuta, kazi ya Serikali iwe kuangalia ubora na kuchukua kodi kutoka Mamlaka ya Serikali ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninajua muda hautoshi, lakini ninaishukuru sana Serikali na ninaendelea kumtia moyo Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kuna watu wanasema mambo mengi, wengine wanataka hata kufikia stage kulichonganisha Bunge na Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani hakuna Mbunge hata mmoja wa kuthubutu kuwaza mambo kinyume na Rais wetu tuliyemchagua na kumpigania. Kuna watu kazi yao ni kutunga majungu na kupitia hayo wanataka wapate fedha, ili kusudi ionekane eti Bunge lina mgogoro na Rais. Hatuna mgogoro na Rais Samia na Bunge hili, sisi Wabunge wa CCM, tutamlinda Rais wetu toka ameingia madarakani mpaka anamaliza muda wake wa Kikatiba, tutamlinda sisi humu ndani. Wale wanaopeleka majungu, hapa kuna Wabunge eti wanataka kupiga sijui vote of no confidence, hakuna Mbunge hata mmoja wa Chama Cha Mapinduzi atahangaika kupoteza muda, kazi yetu itakuwa ni kumlinda Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wale ambao wamezoea kufanya kandarasi ya kutunga majungu, ili wapate fedha, kuumiza watu wengine, sisi Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi tutamlinda Rais wetu kwa wivu mkubwa. Tutamlinda kwa jicho pana na Mungu atusaidie, wapika majungu wote Bwana Yesu awape laana kubwa. Tunataka Rais wetu apate utulivu, hatutaki majungu, mara kuchonganisha Bunge, mara kuchonganisha Wabunge, kwa faida ya nani tunafanya haya mambo? Tumwache mama yetu apate utulivu aongoze hii Serikali, aongoze hili Taifa, amalize muda wake. Mungu aweze kulipatia baraka Taifa letu na kuacha tabia ya majungu ya kutaka kuigonganisha Serikali na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafikiri nimeeleweka. Ninashukuru sana. (Makofi)