Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kupata nafasi. Ninaomba kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu, lakini ninaomba nijikite zaidi upande wa TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hii ziara anayoifanya sasa hivi ya kupita halmashauri zote, kupita na kwenye majimbo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa hapa Bungeni tangu mwaka 2000. Kwa hiyo, nimekuwa kwenye halmashauri hasa. Ninaangalia hizi halmashauri zetu tangu mwaka 2001. Serikali lazima ielewe kwamba wanapeleka pesa nyingi sana kwenye halmashauri zetu za wilaya, lakini niseme ukweli, Waziri Mkuu alivyopita amegundua mambo mengi yanayofanyika kwenye halmashauri zetu. Amagundua kasoro, amegundua na nguvu za halmashauri, lakini hayo aliyoyagundua kutoka kwenye halmashauri yatalisaidia sana Taifa, kama atarudi na timu ya kuyarekebisha yote aliyoyagundua kwenye halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilikuwa hapo tangu mwaka 2001 mpaka leo, nimekaa na wenyeviti wa halmashauri wengi, nimekaa na wakurugenzi wengi, ukweli pesa za Serikali zinazokwenda kwenye halmashauri; ninamwomba Waziri wa TAMISEMI arudi akaangalie vizuri pesa zinavyokwenda na zinavyotumika kwenye halmashauri zetu. Mwenyewe kwa miaka yote hiyo niliyokaa, kuna vitu vingi vinanisumbua sana, lakini ninaona inatosha, nisizungumze zaidi ya hapo. (Makofi)
mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba niongee suala la pili. Leo nitaongea zaidi kwa upande wa Jimbo langu la Same Mashariki na upande wa Wilaya yangu ya Same. Ninaomba kuongelea suala la elimu ya msingi na sekondari. Ninakwenda upande wa Kifungu namba 143, ukurasa wa 57. Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu pamoja na kukamilisha maboma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri na ninaipongeza sana Serikali kwenye upande wa kujenga na kukarabati shule za msingi, na sekondari. Niseme ukweli, Jimboni Same Mashariki nina shule za msingi 89, lakini 12% ya shule hizo zina uchakavu mkubwa sana. Nikimaanisha kwamba shule 13 za msingi, uchakavu wake ni mkubwa mno na ni hatarishi kwa maisha ya wanafunzi kwenye hizo shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwomba Mkurugenzi afanye tathmini ya zile shule. Alipita akafanya tathmini ya kutosha, akazitaja shule, akanipa kimaandishi na nimempelekea Waziri wa TAMISEMI. Shule ambazo zina uchakavu na ni hatari watoto kuendelea kuishi. Kuna Shule ya Mtii, Shule ya Kidaru, Msoroha, Maganda, Bendera, Makasa, Mtundu, Lugulu, Kanza, Bwambo, Kwasekingo, Msasa, Uzambara na Ramu. Hizi ni shule 13 ambazo Mkurugenzi mwenyewe ameziweka kwamba ni shule zenye uchakavu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kwa unyenyekevu, wakarabati hizi shule ambazo Mkurugenzi akiandika kwamba, zina uchakavu mkubwa yeye mwenyewe ameshakiri; ninaiomba Serikali kwa unyenyekevu mkubwa, hebu wakarabati hizi shule. Kwangu zinanipa shida kwa maana nikifanya ziara kwenye zile shule, nikiziona zile shule na mimi ni mwalimu. Kwanza wakiniona mimi, kama Mbunge, wanaona jukumu la kujenga shule ni la kwangu, kwa hiyo, unakuta walimu wanalalamika, wanafunzi wanalalamika na wazazi wanalalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani wetu wa Kata pia wanapata shida sana kwa sababu, wanalaumiwa kwa sababu, wao wanaishi kule na wengi hawakurudi, Madiwani wangu wa Kata waliadhibiwa kwa sababu ya uchakavu wa shule za msingi. Jamani ninaiomba Serikali, zile shule ambazo zimefika mahali zina uchakavu mkubwa, tafadhali sana, zipate ukarabati. Ninakiri kwamba, wanazikarabati, lakini shule kama 13 zote zina uchakavu mkubwa na zilizobaki sina shule bora zaidi ya tano kwenye jimbo langu. Ninafikiri Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amenielewa na atalichukua kama mimi ninavyolichukua. Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niongee suala la pili, ninarudi Same huko huko. Wilaya ya Same ni kubwa sana, ninafikiri kama Mkuu wangu wa Mkoa yupo anakiri. Wilaya ya Same inaketi kwenye takribani 40% ya Mkoa wa Kilimanjaro, ni wilaya kubwa mno kiasi kwamba, hata huyo Mkuu wa Wilaya hana uwezo wa kuiangalia; anaingalia ndiyo ninakiri, lakini Mkoa wa Kilimanjaro Wilaya yangu mimi ya Same imeketi kwenye 40%. Kuna wilaya ndani ya mkoa imeketi kwenye asilimia nane ya Mkoa, sasa unaona ni kiasi gani Wilaya ya Same inabidi iangaliwe sana kwa sababu, ni rahisi kutokupata maendeleo kwa sababu, ya ukubwa wa wilaya ile. Serikali hapa ninaomba mniangalie sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wilaya kubwa kama hii, mimi kama Mbunge wa upande wa Mashariki nina uhakika na Mbunge wa upande wa Magharibi angekuwepo angezungumza hili; tunaomba Uwanja wa Ndege wa Same ujengwe. Ule uwanja wa Same ni wa kimkakati kwa sababu, umepakana na Mkomazi National Park sasa iwapo ule uwanja wa ndege utajengwa, kwanza utaboresha sana hii Mbuga ya Wanyama ya Mkomazi. Hilo ndilo jambo la kwanza ambalo ninaiomba Serikali iangalie umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa Same kwamba, upo kimkakati, uko pale japo hauna hali nzuri, hauna uwezo wa kusaidia hata kandege kadogo kutua kwa sababu, uwanja ule wa ndege upo mpakani mwa Mkomazi National Park. Serikali ikichukua hatua za kuujenga uwanja ule tayari, automatically, inaboresha utalii ndani ya Mkomazi National Park. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkomazi National Park ni ya kipekee duniani kwa sababu, ina mbwa mwitu ambao hawapo mahali pengine na ina faru weusi. Kwa hiyo, watalii wengi wanaoingia nchini wanawafuata wale faru weusi na mbwamwitu. Naiomba Serikali ione umuhimu mkubwa wa kukijenga kile Kiwanja cha Ndege cha Same, wachukue kwamba, ni mkakati wa kuboresha utalii kwenye Mbuga ya Wanyama ya Mkomazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watakapojenga pia,huu uwanja wa Same wataleta maendeleo sana kwenye wilaya, ambayo ndiyo kubwa kwenye Mkoa wa Kilimanjaro kwa sababu na sisi tutakuwa na mambo mengi ya ujasiriamali na kusafirisha mizigo. Mimi ninalima tangawizi, 72% ya tangawizi ya nchi hii, kwa hiyo, uwanja huu wa ndege utasaidia usafirishaji kwa haya mazao hasa kwa sababu, tangawizi nyingi inakwenda Kenya na Kongo. Sasa ule uwanja wa ndege utasaidia hata usafirishaji wa mazao, kama zao la tangawizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninainyenyekea Serikali, ninaichukulia hii ni bajeti ya kwanza ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, ninaanza kwa kuomba Uwanja wa Ndege wa Same. Nitarudia hili neno, kila nikisimama, ni Uwanja wa Ndege wa Same kwa faida ya maendeleo ya Wilaya ya Same.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninakushukuru sana. (Makofi)