Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi ya kuchangia mbele ya Bunge lako Tukufu na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitachangia katika maeneo mbalimbali, lakini nitajikita sana katika eneo la Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Mchango wangu wangu utajikita katika maudhui matatu, nitapongeza, nitashauri na nitakuwa na maombi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Missenyi, Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikushukuru kwa mara nyingine kwa kunipa nafasi ya kuchangia, lakini kwa nafasi ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoendelea kusimamia Taifa letu, lakini tunaona mambo yanaendelea kusonga mbele. Nimpongeze sana amekuwa Mama hodari na shupavu kuendelea kuhimili vishindo vyote na akiwa ame-focus kwa malengo mahususi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze wasaidizi wake Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi; Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba; lakini pia niipongeze sana Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, chini ya nahodha, ndugu yangu, Profesa Riziki Shemdoe na Naibu Mawaziri wake wawili, Dkt. Jafar Seif na sasa hivi Dkt. Festo Dugange; chini ya utendaji mzuri wa Mtendaji Mkuu wa Wizara hiyo Katibu Mkuu, Adolf Ndunguru; Naibu Makatibu Wakuu wote na Wakurugenzi wote wa Wizara hiyo, ikiwemo na wasimamizi wa mikoa yote, Wakuu wa Mikoa, ma-RAS, Wakurugenzi wote na Wakuu wa Wilaya kwa kuendelea kusimamia utendaji kazi ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza nitajikita kwenye ushauri katika eneo la TARURA. Kwanza nipongeze sana juhudi kubwa za Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kusimamia maono yake na kauli anazozitoa thabiti. Hii inakuwa reflected katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2026/2027. Wakati Mheshimiwa Rais anafungua Bunge letu hili, aliahidi kuongeza bajeti ya TARURA ili tuweze kutengeneza barabara na kusaidia wananchi wake katika meneo yetu. Leo sisi ni mashuhuda katika bajeti hii Mheshimiwa Rais ameongeza bajeti kutoka shilingi 944,000,000,000 ya mwaka wa fedha 2024/2025 na leo tunaenda shilingi trilioni 1.2 katika mwaka wa fedha 2026/2027. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaona kwamba ni kazi rahisi, lakini ni kazi ngumu kuhakikisha kwamba fedha inaongezeka zaidi ya shilingi 200,000,000,000 kwa bajeti ya awali. Mheshimiwa Rais akaenda mbali akahakikisha kwamba bajeti hiyo, fedha ambazo zinatumika katika nchi hii ni fedha za ndani. Kwa hiyo, unakuta imetoka shilingi 710,000,000,000 fedha za ndani na leo tuna shilingi 817,000,000,000 ongezeko la shilingi bilioni 116.9. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala siyo la kusema kwa sauti ndogo, ni kwa sauti kubwa kwa mapenzi mema ya Rais wetu. Hapa tuna uhakika kwamba fedha zetu za ndani, sasa zinaenda kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo yetu na hiyo itasaidia wananchi wote kuwa na usafiri mzuri, lakini kuongeza hata mazao yanayotoka mashambani na hivyo kuinua uchumi wa wananchi wetu. Hiyo ni kazi nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninaendelea kumpongeza kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi ya pili katika eneo la TARURA; tulikuwa na madeni Mwaka wa Fedha 2024/2025 madeni ya wakandarasi yalikuwa zaidi ya shilingi 782,000,000,000, lakini Rais amelipa zaidi ya 57%, shilingi bilioni 446.6 na hiyo unaona kwamba ni nia ya dhati ya Rais kuhakikisha kwamba analipa wakandarasi ambao wanaendesha miradi chini ya TARURA ili waendelee kufanya kazi nyingine nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo nishauri; baada ya kuongeza bajeti na baada ya kulipa madeni ya nyuma ambayo yalikuwa yanasumbua sana katika maeneo yetu, niombe sasa yale madeni machache yaliyobaki yaweze kuwekewa mkakati mzuri na yaweze kulipwa bila kuathiri bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2026/2027. Hii 1.2 trilion tuione kwenye kujenga miradi yetu ndani ya maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo, kuna maeneo mengine ya kushauri. Tunaangalia katika halmashauri zetu, lazima tuainishe pia hizi fedha tunazipata wapi. Tunaona katika mikopo ya 10%, kazi nzuri imeendelea kufanyika, lakini kuna component ya marejesho ambapo mpaka mwaka jana tuna zaidi ya shilingi 152,000,000,000 ambazo zipo kwa ajili ya marejesho, lakini bila kuathiri sheria yetu ya mikopo ya 10% ambayo iendelee kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha za marejesho baada ya kupitia taarifa mbalimbali ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tunaona ni fedha zipo ambazo Serikali inaweza ikaona kwa jicho ambalo ni la busara, ikazielekeza katika eneo lingine, zikasaidia kufanya miradi ambayo ina tija kwa Taifa letu. Ninashauri katika eneo la TARURA, tuangalie, lakini kupunguza madeni ili tuweze kumpa mwanya Rais wetu, kumpumzisha aweze kutafakari mengine mazuri kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kushauri katika eneo hilo, tuweze kuainisha maeneo hayo na hizi fedha zikipatikana basi TARURA itakuwa ina chanzo kizuri cha kupata fedha ili tuendelee kujenga barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili ni eneo la fedha za makaa. Tumevuka na fedha za bakaa zaidi ya shilingi 722,000,000,000 na fedha hizi kuna fedha ambazo zinatokana na mapato ya ndani na zingine za nje. Tunashukuru kwamba wafadhili wakati mwingine wanachelewesha fedha, lakini fedha hizi za bakaa zikishavuka zinaenda kutumika sambamba na bajeti ya mwaka husika. Hii imekuwa ikileta pressure kubwa katika utekelezaji wa miradi katika maeneo ya halmashauri zetu na mikoa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili tunaona pressure kubwa na watekelezaji wetu wakiwa na fedha hizi, wanaonekana kama vile wana suala ambalo wanatakiwa wakimbizane nalo likamilike bila kujali ubora wa miradi na value for money ya miradi hiyo. Niombe sana, tunatambua ipo Sheria ya Mlipaji Mkuu wa Serikali, Sura ya 439. Ukiangalia Kifungu cha 20(2) kimempa mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kwamba, fedha za bakaa zikivuka mwaka wa fedha zisizidi zaidi ya miezi sita ya mwaka unaofuata. Baada ya hapo zikivuka, Mlipaji Mkuu wa Serikali amepewa mamlaka ya kuzichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi unakuja katika maeneo yetu kwamba, watu wana hofu kwamba fedha hizo zikivuka mwaka zitachukuliwa. Hii nchi ni ya kwetu na sisi ni tunashauri, tuangalie ni vikwazo gani ambavyo vinawasibu wenzetu wanaotekeleza miradi, kuanzia ofisi za mikoa na halmashauri zetu. Tunao Mfumo wa NeST unaendelea kufanya kazi vizuri, lakini una changamoto. Wakati mwingine mtandao wa shida, lakini Mfumo huo ndiyo utumiwa na local fundi kuomba miradi, wakati mwingine hata lugha inayoongelewa mle kwenye mfumo mpaka waende kuelimishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kuna mikoa mingine mpaka leo, baadhi ya wakuu wa mikoa wanakuja wanasema, katika mkoa wangu kupata mafundi ni kazi ngumu sana. Kwa hiyo, niombe pamoja na sheria hii ipo, lakini isiwepo kama kigezo cha fedha za bakaa ambazo zitabaki na zikavuka mwaka unaofuata zikachukuliwa, ili wananchi wetu waendelee kujengewa miradi yao kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala lingine, niombe kushauri kwenye mgawanyo wa fedha rasilimali zinazokusanywa na halmashauri. Nipongeze kwa kazi nzuri, halmashauri zimeongeza mapato ya ndani na tunaona katika bajeti hii, tunaenda kukusanya zaidi ya 1.9 trillion kutoka 1.6 trillion iliyokuwepo. Hii ndiyo usimamizi madhubuti wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia na kuhakikisha kwamba mianya yote ya uvujaji wa mapato, lakini vyanzo vipya vimeainishwa na tunaona usimamizi mzuri wa ofisi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, mikoa na wilaya zote wameendelea kusimamia mapato vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika eneo hili ninaomba kushauri, kuna maeneo ambako halmashauri zetu zinafanya vizuri, lakini maeneo mengine yanajikita katika majukumu ambayo ni kama subsidiary. Tuache yale mawanda ambayo yameainishwa katika utekelezaji wa miradi ya halmashauri. Kwa mfano, unakuta halmashauri inatenga bajeti kubwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi, unakuta halmashauri inatenga bajeti kubwa kwa ajili ya kuendesha timu za mipira, unakuta halmashauri inatenga fedha nyingi kwa ajili ya kujenga shule za Kiingereza; lakini halmashauri hiyo haina zahanati, haina matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri, kazi hizo zinazofanyika ni nzuri, lakini lazima tuangalie ile core function ya halmashauri zetu ili tuweze kuhamia katika maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika meneo haya niendelee kushauri kitaifa, lakini sasa kwa sababu umeshanigongea kengele ya kwanza, hebu nikimbie kwa waajiri wangu huku Jimbo la Missenyi nisije nikawaacha bila chochote. Tunaona ofisi yetu ya TAMISEMI inaenda kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo huduma za jamii. Tunashukuru imeendelea kufanya kazi kubwa, lakini ninaomba kusema kwamba na Wilaya ya Missenyi bado tuna uhitaji wa shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna sehemu zingine ambazo shule ziko umbali wa kilometa 20 na zina msongamano mkubwa wa wanafunzi. Kwa hiyo, niombe katika Wilaya ya Jimbo la Missenyi, katika Kata ya Mutukula, Kata ya Kyaka tunaomba sekondari mpya ili wananchi hao waweze kupata shule nzuri na watoto wetu waweze kusoma. Vilevile, zipo shule mpya tumejenga nzuri ila umbali, niombe tuweze kupata hostel kuhakikisha kwamba wanafunzi wetu wanakaa katika eneo lao ili wasome vizuri na ufaulu uweze kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijajua ndiyo dakika za mwisho au ni ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)