Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

Hon. Mabula Johnson Magangila

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi ya kuongeza pale ambapo Waheshimiwa Wabunge wamechangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Ninaomba nikusaidie kidogo, jina langu ni Mabula Magangila kutoka Jimbo la Msalala, Mkoani Shinyanga, Wilaya ya Kahama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, kwetu sisi Wanamsalala kwanza kabisa, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi njema kabisa ambazo anafanya kwa Taifa letu. Kwetu sisi siyo tu hotuba, kwetu sisi Mheshimiwa Rais amegusa maisha ya Wanamsalala, lakini kabla ya Wanamsalala ninaomba nisemee sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ni Rais ambaye amekusudia kuleta mageuzi makubwa kwa sekta binafsi. Ni Mheshimiwa Rais huyu ambaye ameingia madarakani nchi yetu ikiwa inakusanya shilingi trilioni 18, leo hii tunakusanya shilingi trilioni 32, mapato haya hayatoki nje ya wafanyabiashara ni Rais huyu ndiye aliyeboresha mazingira na kuweka mazingira wezeshi ya wafanyabiashara. Rais huyu ndiye aliyekataa kamatakamata ya wafanyabiashara, ni Rais huyu ndiye aliyeweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa vibali katika sekta yoyote unayotaka kufanya biashara, ni Rais huyu ndiye aliyethubutu kutunga sera nzuri kabisa, hasa katika sekta ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapozungumza hapa Awamu ya Sita ndiyo ambayo migodi mingi mipya imeanzishwa. Wachimbaji wadogowadogo na wanaojifunza kuchimba wamechimba, wanaojua kuchimba wanachimba, wenye leseni wanachimba, wanaotaka kushirikiana na wenye leseni wanachimba, awe ni mtu ambaye anataka kwenda kuokota ukwale, wale akinamama wanapata dhahabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu hii ya Sita umeanzishwa mgodi pale Sengerema, Mgodi wa Nyanzaga. Ni katika Awamu hii ya Sita umeanzishwa mgodi kule Kabanga Nickel ambao unamilikiwa na Tembo Nickel, katika Awamu hii ya Sita. Leo hii tayari pilot plant ya madini ya uranium imekamilika, Awamu hii ya Sita, lakini kwenye graphite tayari tuna Faru Graphite, tuna Lindi Jumbo tayari uzalishaji umekwishaanza. Ni Rais huyu ndiye ambaye ameruhusu haya yote yafanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya yote kufanyika katika sekta hii binafsi naomba Wizara ya Fedha, haya mambo yote aliyoyafanya Mheshimiwa Rais kwa utashi wake Bunge hili tukubaliane yawekewe sasa Sheria kali, ili yasije tena yakabadilika na kupeleka huzuni kubwa kwa wafanyabiashara. Tungependa kusudio hili la Mheshimiwa Rais la kuboresha sekta hii binafsi na kuifanya Serikali yake kuwa ni sekta wezeshi na siyo sekta inayo-control na kuzuia maendeleo ya Watanzania. Tukatunge sera nzuri, tuweke Sheria nzuri za kuendelea kuweka hali hii ambayo Mheshimiwa Rais amekusudia isichezewe na mtu yeyote atakayekuja hata baada ya yeye kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya madini, tumeweza kuanzisha migodi mipya, lakini ni migodi ambayo ilifanyiwa utafiti miaka mingi nyuma, twendeni sasa kupitia Wizara yetu ya Madini, Mheshimiwa Rais amekusudia kuweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi, ili kukuza sekta binafsi. Twendeni tukaweke vivutio hivyo, tukaongeze utafiti. Kampuni nyingi za utafiti, hasa zinazomiliki leseni kubwa za utafiti ziliacha kutafiti. Tunapoacha kutafiti tunaua matarajio ya kuwa na migodi mingine mikubwa kama Geita, kama Barrick, North Mara na Bulyanhulu, ambayo ilitafitiwa miaka mingi nyuma. Twendeni tukae na hawa wawekezaji, tuangalie ni kwa namna gani tutawavutia watafiti migodi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii sisi Msalala tunanufaika na mwekezaji mmoja tu, Bulyanhulu, ambaye ameweza kutuchangia CSR ya kujenga barabara ya lami kutoka Kahama kwenda mpaka kule Kakola, kilometa 71, shilingi bilioni 101. Hivi leo hawa wawekezaji wetu tukiwavutia zaidi, wakatafiti migodi mingine, wakaanzisha migodi mingine, tukafungua migodi mingine mikubwa zaidi kwa kushirikiana na wachimbaji wetu wadogowadogo tutapata CSR kiasi gani; hata hizi pesa tunazohangaika kutafuta, kwa ajili ya miradi yetu ya TARURA inawezekana TARURA na wenyewe wakajenga barabara nyingi za lami kuliko za moramu. Twendeni tukaimarishe sekta binafsi tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, ili tuhakikishe tunapa pesa nyingi zaidi, kwa ajili ya ku-finance miradi yetu ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Msalala kwa kumchagua Mheshimiwa Rais kwa kishindo. Mimi Mbunge wao ninawaahidi sitawaangusha, sisi kule tunasema jambo moja tu, Msalala moja, maendeleo kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)