Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASHA R. BARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa ninamshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuweza kwa mara ya kwanza kunifikisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuweza kuniteua leo Asha Baraka mnayemjua kila siku yupo katika mziki wa dance Twanga pepeta leo nimekuwa Mbunge, ninawatetea wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamsifia sana Rais wetu kupitia hotuba yake, Rais wetu ameweza kupita sehemu tofautitofauti na hakuweza kubagua, ameweza kubadilisha watu tofauti na ukiangalia hii hotuba yake hakuna mahali alipoacha. Kwanza kabisa nizungumze tu kwa upande wa akinamama; ameweza kumtua mama ndoo kichwani na pia ameweza kumtua mama kuni kichwani kwa kupitia nishati safi na salama ya gesi. Leo akinamama wengi majumbani wanatumia gesi ambayo ni nishati safi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu pia amekuwa mstari wa mbele sana kuhakikisha anaunganisha biashara kubwa. Leo sisi wanawake unaweza ukatoka Dar es Salaam kwenda Tabora, kwenda Kigoma na kadhalika mpaka Mbeya kwa kutumia barabara na unaweza kuendesha gari yako bila ya kuwa na matatizo yoyote, kwa sababu njia zote zipo ni lami tupu tunakwenda salama na zinaunganisha wafanyabiashara. Wafanyabiashara wa nchi za nje; kwa sisi tunaotoka mipakani, wanaweza kuleta biashara kufikisha Dar es Salaam au kutoa Dar es Salaam kufikisha Burundi, Rwanda na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichambua hii hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu, ukurasa wa 35, Rais wetu ameweza kuchangia kiasi kikubwa sana katika njia za sanaa, utamaduni na michezo. Mheshimiwa Rais, ni mwanamichezo, yeye amekuwa mstari wa mbele sana. Kwa mfano, ukiangalia aliweza kucheza film, kacheza sinema ambayo wote tumeiona na imesababisha kuingiza watalii wengi sana hapa nchini kupitia Royal Tour.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais pia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba anatoa motisha kwa wanamichezo. Wanamichezo mbalimbali wa hizi timu zetu kubwa na hususan timu ya Taifa, amekuwa mstari wa mbele kwa kutoa motisha, tunaita sisi wanamichezo goli la mama ambalo limesababisha watoto wetu au vijana wetu kupata ajira na kupambana kuhakikisha anapambana katika mpira ili aweze kucheza katika timu ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo Mheshimiwa Rais, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan amepambana katika riadha, kama mnavyoona mwaka jana mmeona tumekuwa na mwanariadha ambaye amechukua tuzo ya medali ya dhahabu. Kwa hiyo, hizo zote ni juhudi za Mama Samia Suluhu Hassan. Vilevile, hakuacha wanawake katika mpira, kuna michezo mbalimbali hasa mchezo wa mpira wa miguu sasa hivi vijana wetu wa kike pia wanaweza kucheza mpira nchi za nje na wanapata ajira na wanaingiza kipato kwa kupitia hela za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu pia ameweza kuinua mpira wa ngumi ambao ulikuwa umesahaulika, sasa hivi ngumi nayo imekuwa ni ajira kubwa watu wanapigana huko wanapata pesa. Kwa hiyo, katika hii michezo yote, michezo ni pesa, michezo imekuwa ni pesa imekuwa na thamani kubwa hapa Tanzania. Pia, hakuacha kurudi nyuma kwa watu wenye uhitaji maalum, kuna michezo ambayo inapitia Olympic; michezo ya Olympic ambayo wanakwenda watu wenye uhitaji maalum kupitia TOC ambayo ni Tanzania Olympic, pia, Rais wetu hakuweza kuiacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kwa wale wanaocheza basketball kuna timu ambayo imekuja juu sana, inacheza mashindano ya kimataifa inaitwa Dar City imeweza kumfanya Hashimu Thabiti ambaye alikuwa anacheza basketball nje ya nchi naye anacheza katika hiyo timu kuhakikisha kwamba Tanzania nayo inaingia katika mashindano ya kimataifa ya basketball. Huyo ndiyo Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ukurasa huohuo wa 35 Rais, amesema kwamba tunaendeleza maandalizi ya ujenzi wa studio za kisasa ambazo tutatengeneza film bora na kama umeona mwaka jana Mheshimiwa Rais aliambatana na wasanii wa film kwenda Korea kuhakikisha kwamba wanapata mafunzo ya jinsi ya utengenezaji wa film ili na wao waje kutengeneza film zenye ubora hapa Tanzania. Hilo amelifanya kwa dhati katika njia za michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais pia anatutengenezea ukumbi wa kisasa, kumbi ambazo zitakuwa zinapiga burudani, tukiachana na mambo ya kwenda kupiga burudani kwenye kumbi kubwa ambayo tunalipa sisi wasanii kama shilingi milioni 30 mpaka milioni 12 kwa ukumbi lakini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye anatujengea kumbi ambazo wasanii watakuwa wanafanya matamasha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais pia, Samia Suluhu Hassan, ninaipongeza sana hii hotuba yake na ninaiunga mkono mia kwa mia. Tunakwenda kwenye AFCON, sisi Tanzania kwa mara ya kwanza, mashindano ya AFCON 2027 japo wengine walizungumzia, lakini nitaizungumzia kwa mapana zaidi. Juzi kama mmeona kwenye TV Mheshimiwa Rais alikuwa Arusha na Mheshimiwa Makonda mwenye Jimbo lake la Arusha Mjini na Rais mwenye dhamana ya utamaduni, kuna viwanja vinajengwa vya kuingiza watu takribani 30,000 ambavyo vitaingiza watazamaji, lakini hapohapo sisi akinamama, watu wa bajaji na watu wa bodaboda watafanya biashara kutumia michezo ya AFCON na kama unavyomjua pia Mheshimiwa Makonda huwa harudi nyuma unaweza kusikia pale nyama bure, leo tunachoma nyama tu Arusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimpongeze pia Naibu Waziri Mwana FA na Katibu Mkuu kuhamasisha michezo ya AFCON; na yeye hakurudi nyuma mwaka jana wote ulikuwa unamwona kwenye goli la mama Mwana FA yupo, safari za timu ya Taifa yupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa mara ya kwanza kwa kutuma ndege ya Air Tanzania kwenda kuwapokea vijana wetu waliofanya kazi nzuri katika mashindano. Vilevile, ameweza kuwaalika pale Ikulu akakaa nao pamoja wakabadilishana mawazo na vijana wametuhakikisha kwamba AFCON 2027 watafanya kazi ya ziada na kama mnaona pia juzi, Mheshimiwa Makonda alikwenda kupokea bendera ya AFCON akiongozana na Rais wa TFF pamoja na Waziri mwenye dhamana yake. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Makonda kwa kazi hiyo pamoja na watu wa Wizara wote kwa ujumla akiwepo Katibu Mkuu wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu, nina mengi ya kusema lakini watu wengi wameshazungumza, mengine nitakuwa ninarudia zilezile point zao lakini ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tusiache kumsemea, tunaomsemea ni sisi Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiyo tunatakiwa tumseme na watu wajue Rais amefanya nini, wengine hawajui, wengine hawatembei. Tuwaombe pia wananchi waweze kutembea kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine kwa biashara na waangalie vitu ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amefanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, ninakushukuru sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako. Sasa ninamwita Mheshimiwa Josephine Joseph Kapoma, ajiandae Mheshimiwa Asha Omar na tutamalizia na Mheshimiwa Mabula Magangila.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata fursa hii ya kuchangia katika Bunge lako hili Tukufu. Kwanza ninapenda kushukuru kwa kupata baraka ya uhai lakini pia, ninapenda kuwashukuru akinamama na wananchi wa Morogoro kwa kunipa dhamana hii kubwa. Kipekee, ninapenda kuishukuru Kamati Kuu kwa kunipendekeza na kuniona ninafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende moja kwa moja kwa maslahi ya muda, lakini pia kwa sababu ni mara yangu ya kwanza, nimeisoma hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu na ninaomba nikueleze, hotuba hii inasomwa na kila mtu na kama unavyojua kitu kilicho kibaya hakiwezi kusomwa na mtu, lakini inasomwa na hiyo inaonesha ni kiasi gani hotuba hii imeshiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia alikuwa anasoma hotuba hii Watanzania wote macho yao yalikuwa hapa. Ni hotuba ambayo inaeleweka na inaweza ikasomwa na kueleweka hata na mtoto mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme machache. Nimebahatika kufanya ziara ya kikazi kabla sijawa Mbunge katika mikoa 11 ya Tanzania, nimefanikiwa kutembea kwa siku sita tu nikiwa ninaendesha. Katika mikoa 11 hii, barabara ambazo zilikuwa hazijakamilika hazikuzidi kilometa 60; hii inaonesha ni kiasi gani tumepiga hatua kubwa katika miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimebahatika kwenda kwa ndugu zangu Kigoma, nimepita Kasulu, Kibondo, nimeishi kule mwaka 2018, lakini mwaka jana, 2025, nimepita pale nimekuta mpaka wana hoteli ambazo zina presidential suit, lakini nikikumbuka miaka ya 2018, 2016 kama kulikuwa kuna guest ya bei kubwa, basi ilikuwa ni shilingi 30,000. Nimewatembelea ndugu zangu wa Geita na Runzewe, kule ni kama umelala Abu Dhabi, Dubai, hii inaonesha kabisa ni kiasi gani kama nchi tumepiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, maendeleo hayapimwi kwa macho, lakini kwa kuona. Katika sehemu nyingi hizo, kama nilizozitaja za Kanda ya Ziwa, Geita, Runzewe, nimebahatika kuona kumbi za starehe na za sherehe kubwa. Hii inaonesha ni kiasi gani tunaendelea kufunga harusi na kufanya sherehe kubwa kubwa kwa sababu uchumi umekaa mahali pake. Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia, anatosha na anatosha tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nirudi katika Mkoa wangu wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro mama, Mheshimiwa Dkt. Samia, hatuna deni naye na kama mnavyojua Mkoa wa Morogoro ni katika mikoa ya kimkakati, mama aliahidi kwamba, Mkoa wa Morogoro tutafufua viwanda. Toka mama ameingia, Mheshimiwa Dkt. Samia, tumefanikiwa kufufua kiwanda cha tumbaku cha Mkwawa Recce. Mwaka 2022, kwa takwimu za haraka, Mkwawa imeweza kuajiri wafanyakazi zaidi ya maelfu na kinaendelea kuajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe sasa hivi kimejengwa Kiwanda kikubwa cha Sigara cha Serengeti ambacho kinategemewa kwenye kuajiri wafanyakazi wengi. Kwa manufaa haya ya ufufuaji wa viwanda hivi ni kwamba, dhahiri zao la tumbaku linaenda kuongezeka. Historia inaonesha msimu wa 2025 tumeweza kuzalisha zao la tumbaku kwa zaidi ya kilo milioni 1.85, haya ni mafanikio makubwa na hii inaonesha kwamba, tunakoenda ni kuzuri zaidi ya tunakotoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hayo tumefanikiwa kujenga Kiwanda cha Mkulazi cha Sukari, pale Mvomero. Kiwanda hiki kinatoaa zaidi ya ajira 5,000 na kwa mustakabali huu, maana yake ni tutaenda kuongeza kilimo cha miwa. Siyo hivyo tu, kuna upanuzi ambao umefanyika wa Kiwanda cha Sukari kule Kilombero, hii pia, itachochea kilimo cha miwa na ajira. Hii yote inaonesha ni kiasi gani Tanzania ya jana siyo Tanzania ya leo. Kipekee, kama Mwanamorogoro, ninasema Mheshimiwa Rais ameahidi kuacha tabasamu kwa Watanzania, ninataka kumhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba, Wanamorogoro tabasamu tayari tunalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe kusema ukija kwenye mikopo ya 10%, mwaka 2021 kwa record, Morogoro tulifanikiwa kutoa mikopo ya shilingi bilioni 3.5, lakini kufikia mwaka 2025 tumefanikiwa kutoa mikopo ya 10% ya kiasi cha shilingi bilioni nane na wanawake zaidi ya 14,000 wanufanika. Hii inaonesha kwamba, uchumi wa mtu mmojammoja na uchumi wa watu kwa pamoja ni kiasi gani unaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, ninaishukuru pia, Serikali yetu kwa kutuona Wanamorogoro. Ninajua wote ni mashahidi, wiki iliyopita kaka yangu, Mheshimiwa Aweso, alikuwa Morogoro pale, tumepata fedha nyingi sana, kwa ajili ya maji Mji wa Morogoro, zaidi ya shilingi bilioni 81. Kwa pesa hii Morogoro tutakuwa na maji mengi mpaka tutagawia majirani zetu Dodoma na Dar es Salaam. Hii yote ni kazi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu anatekeleza kwa vitendo, sisi Wanamorogoro tunamuahidi ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu, kama alivyotangulia kusema Mheshimiwa Waziri Mkuu jana, Mama ameonesha dira, sisi kama watendaji tuna kazi kubwa ya kwenda kusimamia maono haya makubwa ambayo Mama ametuletea. Mimi kama Josephine Kapoma ninatamani mwaka 2030 Bunge hili tusije kujadili changamoto, lakini tuje kujadili pesa nyingi tuliyonayo ni nchi gani tunatakiwa kuwakopesha. Ninajua hiyo inawezekana, kama tukitembea na maono ambayo yapo katika hotuba hii iliyosheheni kesho iliyo njema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivyo, ninaomba kuunga hoja hii. Ahsante. (Makofi)