Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikushukuru kwa kuniona ili niwe sehemu ya kuchangia hotuba hii nzuri ya Mheshimiwa Rais. Kwanza, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuwa ndani ya Bunge hili Tukufu, ninaomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai na mimi kuwepo mahali hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitumie nafasi hii kipekee kabisa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndio Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi, Halmashauri Kuu kwa kuniona na mimi mtoto wa mfugaji niwe sehemu ya Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wananchi wa Monduli kwa kunipa heshima ya kunipa kura za kutosha na kumpa Mheshimiwa Rais Samia kura za kutosha ambayo zimeniwezesha mimi kufika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajikita kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo kimsingi imejitafsiri yenyewe vizuri na imejielekeza vizuri haina jambo ambalo linaweza likamshinda mtu yeyote kuitafsiri kwa sababu hotuba imejitafsiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanamonduli tuna sababu ya kusimama kifua mbele na kumsemea Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya miaka minne ndani ya Jimbo la Monduli. Kwanza kuna wengine ambao hawafahamu miaka ya nyuma kabla ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kushika nafasi ya Urais tulikuwa inapofika kila mwaka Januari tunaanza kuwachangisha wananchi shilingi 10,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunakuta wanafunzi tunawapeleka shule kwa awamu ya kwanza na awamu ya pili ili tutengeneze madarasa, lakini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani mwaka wa kwanza tu akatupelekea madarasa ya kutosha kwenye shule zetu za sekondari na hatukuwa na mchango tena kwenye mwaka huo wa kuchangisha wananchi. Kwa hiyo, unaona ni jinsi gani alivyoanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akaendelea kila mwaka na ndani ya miaka minne ya utangulizi wa Mheshimiwa Rais tukajengewa zaidi ya madarasa 109, tukajengewa mabweni zaidi ya tisa, tukajengewa vyoo vya kutosha 64, tukajengewa nyumba za walimu 30. Hiyo ni kazi ya Mheshimiwa Rais alipoingia tu ndani ya miaka minne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi tu; mnakumbuka miaka ya nyuma tulikuwa tunajenga sekondari zetu kwa kuchangishana, kukimbizana, kushikana, lakini Mheshimiwa Rais alipoingia madarakani akatujengea shule za kisasa tano kwenye Kata ya Meserani, Lepurko, Mswakini na Mto wa Mbu kwenye Kata ya Migungani. Shule za kisasa yenye zaidi ya shilingi milioni 600. Hiyo ni kazi nzuri iliyofanywa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ndiyo maana ninasema hotuba ya Mheshimiwa Rais imejitafsiri vizuri na haina kazi ngumu ya kuitafsiri kwa sababu kazi imefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu; ninataka niseme mafanikio kwa sababu nilipata fursa ya kuwa sehemu ya kusimamia hayo mafanikio nikiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kwa zaidi ya miaka 10. Kwa hiyo, haya ninayoyazungumza, atakayezungumza huko pembeni akasema hayana ukweli aende kwenye Jimbo la Monduli aangalie matunda na kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu; Mheshimiwa Rais alipoingia alikuta vituo vya afya zaidi ya viwili ambavyo ni Mto wa Mbu na Makuyuni havikukamilika, lakini ndani ya muda mchache akakamilisha akaweka na ambulance; vile vituo vya afya vile vikakamilika. Hatujakaa sawa akatujengea kituo cha afya cha kisasa kilichoko NAFCO, kilometa 54 kutoka Monduli Mjini mpaka eneo hilo ambayo kimsingi wananchi wengi wa maeneo ya Lokisale, Naalarami na Lemooti walikuwa wanapata changamoto ya kuja kwenye hospitali ya wilaya, lakini tunavyozungumza sasa tuna kituo kizuri cha kisasa cha afya kilichokamilika kilichokuwa na kila aina ya vifaatiba vilivyopo ndani ya hospitali ile na ambulance mpya ya kisasa ipo kwenye kituo kile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu; hospitali ya wilaya ukifika sasa hivi, niliwaambia watu wengine, wananchi wetu walipokaa kwenye foleni kumpigia Mama Samia kura walikuwa wana sababu za msingi za kumpigia kura kwa sababu hospitali yetu ya wilaya sasa utadhani ni hospitali ya mkoa. Ilikuwa asubuhi nasikia hapa watu wakizungumza juu ya kuhifadhi watoto njiti, hospitali yangu ya wilaya ina vile vitanda vya kuhifadhi watoto njiti 11. Kwa hiyo, kwenye Wilaya ya Monduli tume-advance kwa kiasi hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale ukikuta maabara ya kisasa ambayo ukiilinganisha na mkoa havina tofauti. Hiyo yote ni kazi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye upande wa afya. Wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani tulikuwa tuna uhitaji wa watumishi wa afya 341, lakini ndani ya kipindi hiki kichache cha Mheshimiwa Rais, tumeshaletewa watumishi wa afya 221. Unaona ni jinsi gani Mheshimiwa Rais anafanya kazi yake. Unapokuta mtu tukizungumza haya anaona kama tunajifurahisha; hatujifurahishi. Nenda Monduli uone kazi kubwa iliyofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo; ukienda kwenye shule za msingi unaona ni jinsi gani tulikuwa tunapata wakati mgumu. Unakuta tuna madarasa hayajapauliwa, Mheshimiwa Rais alipaua yote na bado akatuletea fedha Monduli Juu tukajengewa shule ya kisasa ya zaidi ya shilingi milioni 480 ambayo watoto wa Wanamonduli, watoto wa wapigakura wa Monduli walikuwa wanapata wakati mgumu kwenda shule panapotokea mvua, kuruka korongo, lakini sasa watoto wale wanapata furaha kwa sababu Mheshimiwa Rais amewajengea shule nzuri ya kisasa pale Monduli Juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, twende kwenye maji. Kuna mradi mzuri; niipongeze sana Wizara ya Maji, iliitafsiri mapema sana hotuba ya Mheshimiwa Rais. Unaona ni jinsi gani mradi kutoka kwenye miinuko yale ya Mto wa Mbu kushuka mpaka Vijiji vya Esilalei na sasa inaelekea mpaka kwenda Otukai mradi ambao uligharimu shilingi bilioni 1.9. Leo ukifika pale Esilalei na wengi wa viongozi wanapokuja wanapoingia kwenye ule mradi; umeshaanza kufanya kazi, umekamilika karibu 95% na wananchi kwenye vile vijiji wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu; tuna miradi miwili mikubwa ambayo ninataka niisemee kidogo. Kuna Mradi wa Vijiji Saba ulioko Makuyuni ambao mradi huo ulisainiwa mwaka 2024. Niiombe Wizara ya Maji, mradi ule umeshaanza na mkandarasi yuko site. Ningefurahi kwa kuwa wananchi wangu wanatamani kutumia au kunywa maji ambayo Mheshimiwa Rais aliwaahidi na ambao umeanza. Niombe mradi ule kwa sababu ukienda hata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais ameelezea kwamba, anatamani miradi mikubwa yote iliyoanzishwa ikamilike mpaka itakapofika 2030. Ninaamini kwa sababu mradi umeshafikia hatua nzuri utakwenda kukamilika kabla ya kufika 2030.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu; Mradi wa Vijiji 18 uliosainiwa 2014 wenye gharama ya karibu shilingi bilioni 20, niiombe Wizara hiyo kwa sababu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais na yenyewe imetafsiriwa vizuri kuhakikisha mradi unakamilishwa. Mradi ule na wenyewe ukamilike kwa wakati ili wananchi wa Monduli waendelee kufurahia matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu, Jemedari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara hiyo iangalie kwa makini na ninashukuru Wizara hiyo yuko mtu makini, yuko mtu mchapakazi atahakikisha kwamba, tafsiri ya hotuba ya Mheshimiwa Rais anakwenda kuisimamia vizuri na kuhakikisha tunakwenda kupata hayo maji kwa wakati mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa ninasoma hii hotuba ya Mheshimiwa Rais, ukijaribu kuangalia kila eneo alilolitaja, mimi nitajikita kwanza kwenye eneo moja hili la mifugo. Umeona Mheshimiwa Rais pale ameelekeza kwenda kutengeneza maeneo ya malisho kutoka hekta milioni 3.6 kwenda hekta milioni sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaamini kabisa kwamba Waziri mwenye dhamana na Mifugo atakwenda kutafsiri na kueleza kiundani juu ya maeneo ambayo tunakwenda kuongezewa kwa ajili ya ufugaji ili kuondoa zile tofauti kati ya wakulima na wafugaji kuhakikisha kwamba, hili tatizo linaondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwenye hilo eneo Mheshimiwa Rais ameelekeza vilevile, kuhakikisha kwamba kunajengwa mabwawa, kuhakikisha kwamba migogoro baina ya wananchi na baadhi ya maeneo, (na Waziri anajua fika Monduli ina mgogoro fulani ambao kimsingi siyo mzuri) ninaamini tunakwenda kuumaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niseme neno moja tu la mwisho. Tumbo lililomzaa Mama Samia Suluhu Hassan limebarikiwa, Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)