Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia katika Hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Kwanza ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwingi wa utukufu. Katika kipindi changu hiki cha awamu ya tatu ya Ubunge ninasimama hapa leo kwa mara ya kwanza. Nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini vilevile ninawashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kwa kunipa fursa hii. Ninataka kuwaahidi mbele ya Kiti chako kwamba yajayo yanafurahisha zaidi na sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hotuba nzuri ya mfano. Sambamba na yeye Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi Makamu wa Rais, pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ninawapongeza sana kwa kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ile ukiisoma kwa kweli inaleta raha kwa sababu imesheheni Wizara zote na kila mahali ambapo unasoma na kulinganisha hali halisi ya utekelezaji uliofanyika kwa kweli unasema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Rais ambaye ni tunu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Rais mwanamke kwa kweli ametuvisha nguo sisi wanawake wa Tanzania. Ametuheshimisha kwa sababu alipokuwa anapokea kijiti hiki wengi walipata mashaka Rais mwanamke ataweza? Ni kwa sababu ya desturi tuliokuwa nayo toka awali kwamba marais wote waliopita ni marais wanaume. Sasa leo hii tunaye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametuvusha na anaendelea kuikimbiza nchi katika sekta mbalimbali kufuatia maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia katika hotuba yake maeneo mbalimbali ambayo ameyazungumza na kuendelea kutoa maelekezo mbele zaidi kwamba, tunatarajia kwenda mbele zaidi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya barabara, hakika unamwona Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuunganisha wilaya na wilaya, katika kuunganisha mikoa na mikoa katika miundombinu ya barabara na katika kuunganisha nchi yetu na nchi jirani. Nani kama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona vilevile katika nchi yetu miradi mingi imeendelea kutekelezwa. Hata sasa tunapozungumza wakandarasi wako kazini wameshapewa pesa na kazi zinaendelea kila mahali; hongera nyingi sana kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miundombinu ya barabara vilevile ninataka nizungumzie katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2025-2030, tayari katika Mkoa wa Ruvuma imeshajieleza katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwamba, Barabara ya Likuyufusi - Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 inakwenda kuanza kujengwa kwa lami msimu huu. Katika urefu huo, tayari pesa imeshapelekwa ya ujenzi wa lami kwa kilometa 60; nani kama Samia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la barabara ninaona kabisa, ninamwona Samia katika Barabara yenye urefu wa kilometa 305 inayotoka Mtwara - Pachani inapita Luchili inakwenda Lingusenguse inapita Lusewa hadi kule Narasi na hatimaye kufika Tunduru. Hii ni barabara ya kimkakati ambayo ni barabara itakayobeba zaidi ya vijiji 37 - 70 ambayo kimsingi wananchi wanaozunguka barabara hiyo ni wananchi wanaojishughulisha na masuala ya kilimo, lakini ni wananchi ambao wanajishughulisha zaidi na masuala ya uzalishaji. Kwa hiyo, ninaiona nchi ya Tanzania ikifunguka katika nyanda za juu kusini kwa kasi kubwa sana. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nizungumzie suala la maji. Ndugu zangu ukisoma katika kitabu hiki cha hotuba yake kuna maeneo unakwenda kukuta kwamba nchi yetu ya Tanzania katika sekta ya maji imekua kutoka 84.1% mpaka 96.1% kwa maeneo ya mijini. Vilevile, unatazama katika eneo la vijijini unakuta imekuwa katika eneo hilo kutoka 70% mpaka 86%. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu zangu tuna kila sababu ya kuwa na wivu na Rais wetu. Rais wetu anafanya mambo makubwa. Kwa sisi ambao tumetembea nchi mbalimbali tunataka tuseme walioko nje na wengine ambao wako humu ndani wanaweza wasijue kwamba, kwa nini tunasema Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumekwenda kwenye nchi mbalimbali unaangalia unakuta mpaka unajiuliza hii nchi toka imepata uhuru mpaka hapo ilipofikia hivi itapambazuka lini? Hali ni mbaya. Ukiangalia kwenye miundombinu ya barabara, miundombinu ya usafirishaji wa anga unakuta hali ni mbaya, lakini sisi tunacho chanda chema mkononi lakini hatukioni, hatukioni ndugu zangu. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya vitu vikubwa na anastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika sekta ya afya vilevile tunaangalia kila mmoja hapa kwenye maeneo yake aliyotoka kuna zahanati, kuna vituo vya afya, kuna hospitali za wilaya, kuna hospitali za kanda; jamani tumpe nini Samia? Nani kama Samia? Ni Rais wa mfano na tunatakiwa tumtie moyo ili Rais wetu aende kufanya vizuri zaidi ya hapa alipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kuzungumzia masuala ya kilimo. Ukienda kwenye kilimo sasa sisi watu wa Nyanda za juu Kusini ndiyo wabobevu katika sekta ya kilimo na ndiyo tunalisha nchi hii. Hakika katika sekta ya kilimo, mama ametutendea haki. Amepeleka ruzuku kuanzia kwenye mbegu, amepeleka ruzuku kwenye viuatilifu na amepeleka ruzuku kwenye mbolea. Tumpe nini Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma mbolea ilikuwa bei juu, mnakaa vikao vya ukoo kujadili namna gani tutapata mbolea, lakini sasa hivi ukienda kwenye eneo hilo ni raha mustarehe. Watu wanavuna mazao yao, wanayauza mapema anaondoka ameuza mazao, anaingia dukani anachukua pembejeo za kilimo, anaenda zake shambani. Hapo vipi? Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hamtanielewa lakini ninachokieleza maana yake ninachechemua. Ndugu zangu suala ambalo pengine ningelishauri Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi Serikali sikivu, ni kuendelea kutafuta masoko ya mazao ya wakulima wetu ili wakulima wetu waweze kwenda kuwekeza kwenye eneo hilo uwekezaji wenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwa kipindi ambacho Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani bei ya mazao imezidi kusonga mbele. Yako baadhi ya mazao bado yana changamoto, lakini ninaamini kwa sababu jina lake ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea kutafuta suluhu ya namna ya bei ili wananchi wake na wakulima wake waweze kufanya uwekezaji kwenye eneo hilo uwekezaji wenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ninataka nizungumzie zao la kahawa. Mwaka jana watu wa Wilaya ya Mbinga wamenufaika kwa bei kubwa sana ya kahawa kutoka kwenye bei ya gunia shilingi 250,000, wameuza mpaka shilingi 900,000. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wako imara, wanaendelea kuhangaika na kilimo kwa sababu tayari wameona kwamba kahawa sasa ni mkombozi. Wametoka kwenye nyumba za nyasi sasa hivi wanaezua na wanakwenda kubandika bati. Nani kama Samia? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nani kama Samia?

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa muda wako umeisha

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Astaghfirullah! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja ahsante sana. (Kicheko/Makofi)