Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuweza kuchangia Hotuba hii ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa mwezi Novemba wakati anazindua Bunge. Ninashukuru sana kwa kupata hii nafasi na ninaanza kwa kuwashukuru sana wananchi wote wa Jimbo la Ludewa kwa kunipa heshima kubwa na kunichagua kwa kipindi cha pili ili niweze kurejea Bungeni ili niendelee kuwatumikia. Kwa kitendo hicho ninawaahidi wananchi wa Ludewa kwamba nitaendelea kuwa sauti yao, nitawasemea na nitaendelea kuwa karibu nao wakati wote. Mwenyezi Mungu tu anijalie uhai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Ludewa si wepesi sana kumwamini Mbunge kumpa vipindi viwili. Mara ya mwisho mwaka 1995 Mbunge aliyetoka ndiye aliyekuwa amekaa awamu tatu. Tangu wakati huo, miaka 30, hakuna Mbunge amepata awamu mbili. Kwa hiyo lazima niwashukuru sana wananchi wa Ludewa kwa heshima kubwa na ya kipekee waliyonipa mimi kuwatumikia. Ninawafahamu watu wa Ludewa, kwamba wao wanapenda matendo matamu, hawapendi maneno matamu. Niwaahidi kwamba watashuhudia vitendo ili waendelee kuniamini na kunipa ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisoma Hotuba ya Mheshimiwa Rais kurasa zote 44. Nimepitia kipengele kwa kipengele, nimeona ameonesha sasa kwa kipindi hiki cha miaka mitano ni mambo yapi anakwenda kuyapa kipaumbele katika kuwatumikia Watanzania. Kwa hiyo na sisi kama Waheshimiwa Wabunge, tunampa ahadi kwamba tutampa ushirikiano. kwa yale ambayo yako kwenye nafasi yetu tutatoa ushirikiano wote ili yaweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeon, ukisoma ukurasa wa 11, amezungumzia, alitoa ahadi ya ajira kwa vijana, alitoa ahadi ya ajira 7,000 kwenye sekta ya elimu na ajira 5,000 kwenye sekta ya afya. Kwa hiyo ninashukuru sisi Ludewa tumepokea watumishi 108, tunasubiri wa idara ya elimu msingi. Elimu sekondari tumepokea watumishi 45, afya 47 na wengine wanaendelea kuripoti. Kwa hiyo ninamshukuru sana kwa kutekeleza ahadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda vilevile ukurasa wa 13, Mheshimiwa Rais amezungumzia jambo la vijana. Amezungumzia na ametoa takwimu kwamba 60% ya Watanzania ni vijana. Tumpongeze sana kwa kuunda Wizara Maalum ya kushughulikia masuala ya vijana na kumteua Waziri kijana ambaye ameanza vizuri, ameanza na mguu mzuri. Kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiangalia kundi la vijana lina changamoto nyingi. Hawa ndiyo wana changamoto ya kukosa mitaji kwa ajili ya kuendeshea biashara na shughuli mbalimbali; ndilo kundi ambalo hatimiliki zile fursa za vyanzo vya uchumi, ni kundi la vijana. Pia ndiyo walio kwenye changamoto ya madawa ya kulevya na msongo wa mawazo. Vijana wanakabiliwa na matatizo mengi na wengine wanakuwa na ujuzi ambao wakati mwingine si hitaji kwenye soko. Kwa hiyo natoa wito kwa Serikali hasa Wizara ya Elimu, Serikali imefanya reforms nyingi sana kwenye elimu ya msingi na sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwenye elimu ya juu twende sasa tukaangalie kule tuweze kufanya reforms, tupitie kozi zote zinazotolewa na vyuo vikuu, tuangalie mahitaji ya soko yanakwenda vipi. Wizara ya Elimu ianzishe kitengo maalum cha Information Center ili wale vijana ambao wanakusudia kwenda kusoma elimu za juu wawe na ufahamu ni nini kinachohitajika kwenye soko. Hii itakuwa muhimu katika kusaidia vijana wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile na kule kwenye soko la ajira kuwe na fairness. Wale ambao wanafaulu usaili waweze kupewa nafasi kulingana na uwezo wao ili hata kusiwe na watu wanapiga simu bwana Mheshimiwa Mbunge nimefanya usaili nisaidie connection. Kwa hiyo connection tuzipunguze ili haki iweze kutendekea kwenye soko la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nimeona amelizungumzia ni eneo la Dira ya Taifa. Amezungumzia na ameonesha pale umuhimu wa miradi ile mikubwa ya kimkakati ambayo inaweza kupaisha uchumi huu. Vilevile dira hii ameonesha wazi kwamba utekelezaji wake unahitaji rasilimali fedha nyingi. Kwa hiyo nitoe wito kwa wasaidizi wake wote upande wa Serikalini waweze kubuni vyanzo vingi vipya vya mapato ili tuweze kuongeza bajeti za TARURA na bajeti za TANROADS kwa sababu kule vijijini Watanzania wengi, zaidi ya 70% ni wakulima. Wana mazao yao, wawe na urahisi wa kutoa kule kwenye shamba maeneo ya uzalishaji kuyapeleka kwenye soko. Kutakuwa na faida kubwa na wengi wataingia kwenye sekta hiyo
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hata kule jimboni Ludewa tukaanza na zile barabara ambazo zinaunganisha tarafa. Kwa mfano Madope pale kwenda Madilu mpaka ukaingia kule Mundindi, ile barabara ni muhimu sana. wenzetu wa TARURA waje na mbinu mpya na teknolojia mpya ya kuboresha hizi barabara ili ziweze kuhimili magari yenye uzito wote. Barabara ile ni barabara yenye uchumi mkubwa, magari yanapita hadi tani 30. Kwa hiyo ni muhimu sana tukaangalia eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija vilevile kuangalia Mheshimiwa Rais amezungumzia masuala ya viwanda, ukurasa wa 23, kuongeza uzalishaji kwenye viwanda. Sisi kule Ludewa kuna mwekezaji anaitwa HWTZ, anakusudia kujenga kiwanda cha kuchenjua chuma kutenganisha chuma na titanium, lakini vilevile kujenga kiwanda cha kuzalisha bidhaa zinazotokana na chuma ambazo zimekamilika. Kwa hiyo ni viwanda vikubwa vina ajira zaidi ya 1,500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji huyu anakabiliwa na changamoto kubwa sana, kwanza barabara upande ule wa Itoni Lusitu Serikali imeanza na iliweka mkandarasi. Tunaomba sasa pale paweze kukamilishwa ili mwekezaji huyu aweze kupitisha vifaa vyake na kuanza kwenda kujenga viwanda vyake. Pia akikamilisha viwanda aweze vilevile kusafirisha bidhaa. Ni mwekezaji mkubwa sana ambaye ameshatwaa eneo la ekari zaidi ya 711, ameshalipa fidia zaidi ya shilingi bilioni 2.5. Uwekezaji wake una thamani ya shilingi 3,000,000,000,000, dola bilioni 1.5, kwa hiyo ni uwekezaji mkubwa, atajenga bandari Ziwa Nyasa ili aweze kwenda kuchukua malighafi za viwanda vyake Malawi na Msumbiji pamoja na kupeleka bidha kwenye nchi hizo. Huko tayari alishapewa maeneo, ameshaanza utekelezaji. Kwa hiyo, ninaomba upande wa Serikali mwekezaji huyu aweze kupewa ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hii ya umeme hasa kwenye kituo cha kupoozea umeme, kwa sababu kwa sasa kipo Madaba na hii inasababisha kukatika sana kwa umeme hata wananchi wanapata kero kubwa sana; ile transmission line kutoka Madaba kuja Ludewa ina uwezo wa kusafirisha megawatts na ilihali viwanda vinahitaji megawatts 30. Kwa hiyo ninaomba sana hii ya Barabara Itoni – Lusitu ikamilike na Kituo cha Kupoozea Umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninapongeza sana Hotuba na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)