Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ili nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa fursa hii ya uhai. Pia, kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Rais kama Mwenyekiti wangu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa kwa kuniteua ili niingie kwenye kinyang’anyiro cha Ubunge na hatimaye wananchi wa Kasulu Vijijini wakaamua mimi niwe Mbunge wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais. Ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kipindi chake cha miaka minne ambacho kimekuwa ni cha neema kwa Taifa letu la Tanzania. Kipindi ambacho tumeshuhudia safari ya kipekee, safari ambayo inafanana na ile safari ya wana wa Israel wanatoka Misri wanaelekea Kanaani. Sasa, Mheshimiwa Rais, ametukuta tuko jangwani hatimaye tunayo matumaini punde si punde tutafika Kanaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutoa hotuba nzuri, hotuba iliyojaa matumaini, hotuba ambayo ni dawa na hotuba ambayo imejaa dhamira ya dhati kama kiongozi, maana kama kiongozi wajibu wake wa kwanza anawaongoza wananchi wake, lakini pia atawasaidia wananchi kwa kupunguza changamoto zinazowakabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kipindi chake cha miaka minne ameonyesha mwelekeo wa kiuongozi wa Taifa ambao nimetangulia kusema tunaelekea Kanaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kiongozi pia ametatua changamoto zetu zinazotukabili kama Watanzania ambazo zingine zilikuwepo na zingine zimeibuka wakati tupo kwenye safari. Changamoto hizo Mheshimiwa Rais amepambana nazo kuhakikisha safari yetu inakuwa ni rahisi na nyepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kipindi chake cha miaka minne ametatua changamoto mbalimbali. Ukizungumzia nishati, umeme mpaka vijijini. Ukizungumzia afya, zahanati na vituo vya afya mpaka vijijini. Ukizungumzia elimu, shule zimejengwa, zikiwepo shule za kimkakati za wasichana. Pia, ukizungumzia kwa maana ya uchukuzi na ujenzi, barabara zimejengwa, pia kuna meli mpya zimejengwa. Kuna ndege mpya zimenunuliwa. Ukija kwenye kilimo utamkuta tena Mheshimiwa Rais pembejeo, wananchi wetu wanafurahia ni shangwe vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utazungumzia pia msukumo wa Serikali kuwekeza fedha nyingi kwenye kilimo ikiwemo kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji. Katika haya hivi ndivyo vilikuwa vikwazo vikubwa ambavyo ukiangalia vingetukwamisha sisi kwenye safari yetu kama Taifa kufika Kanaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumze pia kidogo kwenye baadhi ya vipaumbele vya Mheshimiwa Rais, lakini pia nishauri. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake amezungumzia sekta ya uzalishaji. Kwenye hotuba yake amegusa kilimo, pia amezungumzia na viwanda. Ninamuunga mkono kwenye hili pia ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuziona sekta hizi mahsusi za uzalishaji kitaifa. Taifa letu na nchi yetu tunalo eneo kubwa la ardhi ambalo linakidhi kilimo, ufugaji, pia tuna maeneo ya kutosha ya kujenga viwanda vya kimkakati ambavyo vinaweza vikatutoa kama Taifa kutoka hatua moja kwenda nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nisisitize kwenye kilimo. Ningeshauri kama Taifa tuwe na vitu vichache vya kimkakati. Kwa mfano, tunaweza tukasema tunapambana na kilimo na viwanda kama Taifa, tuhakikishe tunasukuma sekta hizi mbili kufika mahali kama Taifa katika kipindi cha miaka mitano kama Mheshimiwa Rais alivyoeleza kwenye hotuba yake. Kwenye kilimo tunaweza tukaweka msukumo kwenye mazao ya kimkakati, tunaweza tukachagua mazao kadhaa ya biashara kwa mfano chai, pamba mkonge, lakini pia na tumbaku. Mazao haya yanaweza yakatupatia fedha nyingi ya kigeni kama Taifa, lakini pia itatusaidia kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kwenye kilimo. Kuna changamoto nyingine kwenye issue ya masoko. Ninaomba niishauri Serikali ikiwezekana tujitahidi kuongeza nguvu kwenye matumizi ya TEHAMA ili kurahisha wananchi wetu ku-access masoko hata wakiwa vijijini. Kwa mfano, Wizara ya Kilimo inaweza ikawa na software application ambayo uki-click kwa mfano mahindi au uki-click mchele, utaona mchele Dodoma unauzwa kiasi gani, kama ni maharage utaona Dar es Salaam yanauzwa kaisi gani, utaona kama ni Kongwa au wapi maeneo mengine ili mwananchi atofautishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye Jimbo langu mimi ilifika sehemu maharage yanauzwa mpaka shilingi 1,000, lakini wakati huo huo ukija Dar es Salaam ni shilingi 3,500 na ukija Dodoma shilingi 3,000. Kwa hiyo, mwananchi aki-click mambo yanakwenda vizuri anaweza akajua kitu gani cha kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumaliza ninaomba nishauri pia kwenye suala la ajira na upotevu wa mapato. Ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu. Ahsante sana.