Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja hii ya Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipohutubia Bunge hili la Kumi na Tatu, mnamo Tarehe 14 Novemba. Kwanza kabisa ninaomba nitoe shukrani kwa Mwenyekiti wangu wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na Kamati Kuu, amekuwa sababu ya kuwepo katika Bunge lako hili Tukufu, Bunge la Kumi na Tatu, kuendelea kuwawakilisha akinamama wa Manyara. Kwa dhati ya moyo wangu ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Watanzania wote kwa ushindi wa kisindindo na wa kihistoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema ni ushindi wa kihistoria kwa sababu, toka tumeingia kwenye vyama vingi 1992 na uchaguzi wa kwanza 1995, hadi leo sijawahi kuona awamu iliyovunja rekodi kwa ushindi mkubwa namna hii na ninaomba Mungu kama rekodi hii itaendelea kuvunjwa katika chaguzi zinazokuja. Hongereni Watanzania na hongera Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania hawaambiwi tazama. Kulikuwa na sababu kubwa ya ushindi mkubwa kama huu. Watanzania hawawekewi maneno mdomoni, wanajua kazi kubwa kabisa aliyoifanya Mheshimiwa Rais katika kipindi chake alichokuwa madarakani. Kote amewekeza katika sekta za kijamii, kiuchuki, sekta binafsi na vichochea uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupa mfano mdogo tu, tukisemea sekta ya kijamii. Ukienda afya kila mtu anaona uwekezaji mkubwa uliowekwa kwenye afya; zimejengwa zahanati nyingi, vituo vya afya vingi, ukiangalia 2020 vituo vya afya vilikuwepo 8,458, lakini mpaka Disemba 2024 vimekuwepo 9,826, lakini hospitali za halmashauri 50. Hospitali na vituo vya emergence vimekuwa vimefika 116 pamoja na ununuzi wa dawa, vifaa tiba na mambo kedekede pamoja na kuajiri watumishi wa afya. Hata majirani zetu sasa wanatamani kuja kutibiwa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imekuwa sababu ya kupunguza vifo vya akinamama wakati wa uzazi. Kulikuwa na vifo 556 kwa vizazi 100,000 kwa mwaka 2020, lakini hadi kufikia Disemba, 2024 vimeshapungua mpaka 104 kwa vizazi 100,000. Hiyo ni kazi kubwa sana iliyofanyika na Dkt. Samia, lakini vifo vya watoto kutoka 67 kwa watoto 1,000 mpaka 43 ni kazi kubwa sana imefanyika. Hongera Dkt. Samia na hongereni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye sekta ya elimu hiki kitu kinachoitwa elimu bure watu wasione ni jambo dogo. Kumekuwa na Watanzania ambao wanashindwa kuendelea na elimu ya sekondari. Ninafahamu kuna wazazi wamekuwa wanaona ni adha kubwa sana. Mimi ni shahidi, wanafunzi wanavyofika darasa la saba, kuna wazazi wanawaambia wakaandike madudu ili wasifaulu na Serikali ikawasumbua wale wazazi kuwashinikiza walipe ada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imeleta unafuu mkubwa, wanafunzi wanasoma na kwa kuona hivyo, ndiyo maana Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza fedha kwenye eneo hilo toka shilingi bilioni 312 katika mwaka wa 2020 hadi shilingi bilioni 796 kufikia mwaka jana, 2024. Hiyo ni kazi kubwa sana, lakini kumekuwa na ongezeko la shule za msingi, shule za sekondari, madarasa na matundu ya choo kila sekta. Ninampongeza sana kwa kazi kubwa iliyofanyika hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maono yake sasa ya kubadilisha mtaala wa elimu na kuleta hizi shule za amali. Huu unaweza ukawa muarobaini kwa vijana kupata skills, wanavyomaliza elimu warudi kule kuweza kujiajiri na kufanya kazi. Ninaomba Serikali katika eneo hili waweke miundombinu ili wanafunzi wanaokwenda huko wasiende kupotea. Pamoja na walimu na ma-facilitator ambao wakimpika mtoto kwenye amali atoke hapo ana skills na knowledge ya kuweza kujikwamua na maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya umeme; kwanza ninaipongeza sana Tanzania, kwa sehemu kubwa kwa mapato ya ndani tumeweza kujenga mradi mkubwa sana wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambapo tunatarajia kupata megawatts 2,115 na umefika 99% ni kazi kubwa sana iliyofanyika ndani ya Serikali hii. Hii itaongeza upatikanaji wa umeme kwenye vyanzo vingine, ili zile ndoto za Samia Suluhu Hassan za kusema tufikie uzalishaji wa megawatts 8,000 zifikiwe kwa sababu, mahitaji ya Watanzania mpaka sasa hivi ni chini ya megawatts 2,000. Kwa hiyo, kumbe siku moja tutakuwa na ziada ya umeme, tutauza nje na hiki kitakuwa chanzo cha mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kupeleka umeme vijijini na kwenye vitongoji; kwanza ninapongeza kwa sababu, vijijini tayari tumefikia 99%, lakini huko kwenye vitongoji bado tuko kwenye 51% kutoka vitongoji 64,359, ambavyo vimekwishapata umeme ni vitongoji 32,827 ni hiyo 51%. Kupeleka umeme kwenye vitongoji hakika kumepunguza kazi kubwa kwa akinamama (women workload), wamekuwa wanahangaika na nafaka kwenda kusaga mjini, kutuma bodaboda, mara waende na punda. Sasa hivi mashine za kusaga zipo kwenye vitongoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa sababu kubwa ya kupunguza kitu kinaitwa rural urban immigration kwa vijana. Vijana walikuwa wakimaliza la saba na vyuo vikuu ni lazima wakimbie kijijini waende mjini na ndiyo Gen Z wanaoongezeka. Gen Z ni wasomi, akikaa kule kijijini hana cha kufanya, umeme hakuna, hawezi kupata exposure ndiyo anakimbia huko, lakini imesaidia sana pia, vijana kujiajiri; wana ma-salon na ma-grill.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yangu sikivu, hivi vitongoji vilivyobaki waweze kuvi-cover kwa muda mfupi wapate umeme lakini pia wafungiwe kwa bei ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kuona tabasamu kwenye nyuso za Watanzania lazima tuje tuwekeze kwenye sekta za kiuchumi ambazo Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, hizi zikiwa ni kilimo, mifugo na madini, kote huko ili hizi huduma za jamii ambazo zimekwishawekwa kama elimu, afya na maji Watanzania wawe na uwezo mkubwa wa kuvimudu ili Watanzania tusijigawe, tusiwe katika cluster kulingana na wealth. Kwa sababu sasa hivi kuna mtu anapata huduma ya afya kwa gharama kubwa, mwingine kwa gharama ndogo, wengine elimu wanachagua, siku moja Watanzania waweze kumudu hii huduma wakiwa tayari wana hali nzuri ya kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kilimo, kuna fursa nyingi sana huku kwenye kilimo, ni sehemu nzuri sana ya uwekezaji na ndiyo maana Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia kwenye kiti ameipaisha bajeti ya kilimo mara nne. Bajeti ilikuwa shilingi bilioni 294 hadi sasa hivi tunatekeleza bajeti ya shilingi trilioni 1.2 ni kazi kubwa sana imefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna potentials nyingi. Huku Tanzania siyo sehemu ya kusema tunakosa mashamba ya kulima. Kuna hekari zaidi ya milioni 44 zinazofaa kwa kilimo na tumeweza kutumia chini ya 40%. Kuna maeneo yanafaa kwa umwagiliaji, hekari milioni 29, zilizoendelezwa ni milioni moja, hizi zote ni fursa za uwekezaji katika sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bado kuna fursa ya kuzalisha pembejeo hususan mbegu. Zaidi ya nusu ya mbegu zinazotumika hasa za mahindi tunaziagiza kutoka nje, kwa hiyo, hapa kuna fursa kubwa, tunayo mashamba, tunazo potentials na conducive climate ya kuweza kuzalisha mbegu. Kwa mfano, kuna mashamba ya ASA, haya yanaweza wakapewa hata vijana wakatuzalishia mbegu na tukauza nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa nyingine iliyoko kwenye kilimo of course tunajitosheleza kwa chakula, lakini kuna vyakula bado tunaingiza kwa fedha za kigeni, kwa mfano ngano. Watanzania tunatumia zaidi ya tani milioni moja ya ngano, lakini 90% ya hii ngano inatoka nje na tunanunua kwa fedha za kigeni. Sisi tunaweza kuzalisha kati ya tani 100,000 na tani 200,000. Tunayo mashamba Basutu, Ngano Limited, Serikali ione ni namna gani hii ni fursa tuwekeze tujitosheleze kwa uzalisaji wa ngano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye mafuta mahitaji ya Watanzania ni tani 650,000 tunaweza kuzalisha tani 300,000, hizi ni fursa. Tunayo mazingira very conducive kuzalisha alizeti, michikichi na ufuta, tuwekeze maeneo hayo. Tunayo sugar gap, mahitaji yetu ya sukari ni zaidi ya tani 470,000 na sisi tunazaisha kwenye tani 360,000, haya ni maeneo kwenye kilimo yanafaa kuwekezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la mifugo kuna maeneo mengi sana ambayo tuna fursa ya uwekezaji. Kwa sababu tukisema sisi ni wa pili Afrika kuwa na mifugo mingi lakini bado hatujaweza kui-exploit kutoka kwenye mifugo tukapata kipato.
MWENYEKITI: Ninakushukuru sana Mheshimiwa, muda wako umeisha.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)