Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOHNSTON J. MUTASINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia afya njema na tunaendelea na michango yetu sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niwashukuru sana Wananchi wa Jimbo la Bukoba Mjini kwa kunichagua kuwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini na kwa heshima kubwa sana niwashukuru kwa kumchagua Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninapenda kuchangia katika hotuba ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nimesoma kitabu kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka ukurasa wa 40. Nimeitafakari sana Hotuba ya Mheshimiwa Rais, ni hotuba ambayo inatoa maono na mwanga kwa Mheshimiwa Rais anataka nini na anataka nchi iendeje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya na katika Jimbo letu la Bukoba Mjini, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenda mambo makubwa sana na ninaweza nikasema ni muujiza ambaye hajawahi kutokea katika jimbo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ametuletea shilingi bilioni 9.016 katika barabara za TARURA ni jambo ambalo halijawahi kutokea katika jimbo letu la Bukoba Mjini na sasa anakwenda kuongeza pesa katika barabara za TARURA. Sasa anapokwenda kuongeza pesa katika barabara za TARURA niwaombe, TARURA sasa zile kilometa 133.87 ambazo wilaya yangu ya TARURA pale Bukoba Mjini imeziomba ili iweze kuzihudumia, niombe sasa waende kuziangalia ili mwananchi anayeishi Bukoba ziweze kumsaidia na kupandisha uchumi wake na hii ndiyo sera ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara inayotoka Kahororo kwenda Makongo hadi Ntoro. Hii Barabara inakwenda kwenye eneo ambalo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema anakwenda kukuza sekta binafsi. Kule kuna watu ambao wanachimba kokoto wanapiga mawe na inaenda ziwani. Niombe sasa tuweze kuiangalia ili iweze kutengenezwa, ina urefu wa kilometa 4.73.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuleta miradi mikubwa na ya kimkakati katika jimbo letu ambayo ina thamani ya shilingi bilioni 40.04 katika Miradi ya TACTIC. Tunakwenda na tunajenga soko kubwa la Bukoba Mjini pale. Tunajenga Stendi yetu ya Kyakairabwa na tunajenga barabara kilometa 10, lakini tunakwenda kuweka taa 412. Hili ni jambo la kihistoria ambalo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amelifanya katika Jimbo letu la Bukoba Mjini ninasema mama ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la miundombinu sasa anatujengea barabara ya njia nne ambayo inaingia katika mji wetu wa Bukoba Mjini. Ametutumia shilingi bilioni 12 kwa awamu ya kwanza ambapo anajenga kilometa 1.6 likiwemo na Daraja la Kanoni. Niseme ahsante sana Wizara ya Ujenzi kwa kazi kubwa wanayoifanya katika miradi hii, maana thamani ya pesa anayotoa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi na kwa ajili ya kukuza uchumi wa Taifa letu sasa inaonekana wazi. Niombe miradi yote inayotekelezeka katika Wizara zetu, wanahabari watangaze mema ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mama ametenda mambo makubwa sana tumsemee, tuyaseme watu wajue Mama yuko site, Mama halali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama ametuletea shilingi bilioni 2.513 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali yetu ya Wilaya, Kata ya Nshambya. Kwa sasa tunaomba pesa kumalizia majengo yaliyobaki, maana hii shilingi bilioni 2.513 zimejenga vyumba 11. Sasa tumeomba pesa nyingine kwa ajili ya kujenga jengo lingine la hospitali kumalizia ambalo ni la ghorofa. Apewe nini Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo mema anayoyafanya katika Jimbo letu la Bukoba Mjini? Tunasema ahsante sana Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu ametuletea shilingi bilioni 2.8 shule za msingi na akaleta shilingi bilioni tisa sekondari. Tumejenga sekondari za kutosha, tumejenga shule za msingi za kutosha na sasa tunapoomba kuongezewa maabara na madarasa ni kutokana na uboreshaji wa huduma za elimu ambako wanafunzi wameongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema anakwenda kutujengea Uwanja wa Ndege wa Kyabajwa. Uwanja wa ndege katika Mkoa wetu wa Kagera ni uwanja muhimu na tunauhitaji sana na kwa kuanzia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatutengea shilingi bilioni 1.6. Niiombe Wizara ya Uchukuzi na Hazina watusaidie kupata hizi pesa za upembuzi yakinifu na kulipa compensation kwa wananchi wa eneo lile ili ujenzi huu uweze kuanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niyashukuru sana maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kazi yetu sisi ni moja kuyatafakari, kuyaishi na kutenda vile dhamira yake inataka. Niwaombe wasaidizi wake, Mama ana mambo mengi sana kwa ajili ya Watanzania, kwa mfano katika Jimbo langu la Bukoba Mjini ametutengea shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga kitega uchumi na jengo la machinga ili katika katika Jimbo letu la Bukoba Mjini ili machinga waache kuuza vitu wakitembea barabarani, wawe na sehemu yao na hapa ametenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo. Hapa anaangalia watu wote wa hali ya chini, ya kati na ya juu. Kazi yetu ni moja kumsemea na kuunga mkono juhudi zake anazozifanya katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga Stendi ya Bukoba Mjini ya zamani sasa inakwenda kumalizika. Ametenga pale hela za kutosha zaidi ya shilingi bilioni 3.8 na sasa tunaomba atutengee pesa iliyobaki ya kumalizia jengo la kitega uchumi katika eneo lile ili wananchi wote wanaoishi maeneo yale waweze kupata maeneo yao ya kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika njia nne tunayojenga pale Bukoba Mjini, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga shilingi bilioni 12, lakini ameongeza shilingi milioni 340 kwa ajili ya upembuzi yakinifu, kwa ajili ya Barabara kutoka pale Rwamishenye round about kwenda Kyakairabwa na kutoka Rwamishenye round about kwenda Magoti ambayo jumla ni kilometa 7.5. Niiombe Wizara ya Ujenzi upembuzi yakinifu ukamilike ili tuweze kupata pesa hizi za kuanza ujenzi wa barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nipende kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na njema anayoifanya kwa Taifa letu, lakini niwapongeze sana Mawaziri wanafanya kazi nzuri chini ya Waziri Mkuu na Mungu awabariki sana, ahsanteni sana. (Makofi)