Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

Hon. Hamisi Shabani Taletale

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Kwanza kabisa ninamshukuru Mwenyezi Mungu Azza wa Jallah kwa kunifanya nimerudi salama Bungeni, lakini pia ninakishukuru chama changu, Chama Cha Mapinduzi na nimshukuru Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Vile vile niwashukuru sana Wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kwa kunirudisha mara ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Morogoro Kusini Mashariki tuna neno letu tunasema Mheshimiwa Dkt. Samia anatosha wengine watatuchosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wabunge wa mikoani, sisi ni Mkoa ambao ulipata nafasi ya kwanza ya kutembelewa na Mwenyekiti wa Chama chetu na Rais Wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania. Alifika nyumbani kwetu pale Ngerengere kwa mara ya kwanza, lakini yale ambayo aliyoyaongea Ngerengere na ndiyo ambayo ameyaongea ndani ya hili Bunge. Niseme kidogo, sisi Wanamorogoro Vijijini, Wanamorogoro Kusini Mashariki tuna mengi ya kujivunia, tuna mengi ya kusema juu ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza na sekta ambayo ukiniona nimesimama ninaonekana yes big wa Kisaki amesimama, lakini Rais alipokuja jimboni akasema jina hili halikufai ninalichukua mwenyewe. Wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni ila kuna kauli imetoka Mheshimiwa Dkt. Samia si mnyonge tena. Kwa kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia si mnyonge tena shughuli yetu kumpa haki yake, Mheshimiwa Dkt. Samia apewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivyo, wakati amepita Morogoro Kusini Mashariki alielekeza Wizara ya Fedha, tayari tumeletewa bilioni nne na Mkandarasi ameanza kazi. Tunasubiria mchele kidogo uendelee, kazi iendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye Sekta ya Elimu. Ukitazama sisi watu wa vijijini tuna kila sababu na neno la kusema, nami niiombe Wizara ya Elimu kwa kuwa Rais ameyafanya makubwa shughuli yenu ni kwenda kuyatangaza yale ambayo Mheshimiwa Rais amefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mtaala wa Elimu tunasoma miaka 10, kwenye hii miaka 10 hii miaka minne kuna Mtaala wa Amali. Kwetu vijijini, mimi kwangu kwenye Kata yetu ya Tomondo Mheshimiwa Rais, ameleta Shule ya Amali maana unasoma Sekondari baada ya hapo unasoma ufundi kuanzia form one mpaka form four. Leo hii ukitoka hapo unakuwa una cheti cha form four na una cheti cha ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais ameangalia dunia inataka nini? Dunia inataka utaalam ujuzi. Kwa hiyo, ujuzi unaanzia kuanzia form one mpaka form four. Leo hii Vyuo vya VETA vilivyojengwa nchini ndio maana kauli yangu ninairudia kwa kumwomba kaka yangu Profesa Mkenda na dada yangu Mheshimiwa Wanu kuongeza na kuwekeza kwenye matangazo kuitangaza Wizara ya Elimu ili kesho na kesho kutwa watu wajue nini kimepelekwa kule chini. Nina ushahidi, sisi sasa hivi hatuna changamoto ya kuchangisha changishana, Rais ameshusha hela za shule kule chini watu hawajui na ndiyo maana wanayasema wasiyoyajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nipende kusema kwamba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutuletea vijana wawili machachali kwenye Wizara yetu ya Michezo. Maana kuna mmoja anafoka, mmoja anahubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ina Mchungaji na Mwanamziki; kwa hiyo kwa hili unaloliona tumeona sura nzuri na mwanzo mzuri wa AFCON. Tumwombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya michezo, sisi Wanamorogoro Mkoa kwa ujumla ukiangalia soka la hii nchi hatusemi kwa sababu ninavutia ngoma kwangu, soka la hii nchi sura ya kubwa iko Mkoa wa Morogoro. Tuiombe, dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kubwa sana kwenye kuwekeza michezo, viwanja vya michezo Morogoro sisi tia maji, tia maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wizara ya Michezo Mheshimiwa Rais ametuletea SGR kama kuna treni inayojaa nchini ni treni ya Dar es Salaam – Morogoro, kama tunakwenda kwenye AFCON lazima tuwe na parking ya michezo pale, hata wachezaji wanaokuja mazoezi watacheza Morogoro Mjini, Mbugani watakwenda Mikumi. Ninajua hili suala ni dogo sana kwao Mawaziri hawa wawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hajakosea kumweka Mchungaji, kumweka na mwana Hip hop, ana maana yake. Maana hii sisi tunatakiwa twende tukajivunie kwenye hii Sekta ya Michezo na kwa uenyeji wetu wa AFCON ya mwakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niseme jambo dogo hapa kama tunatazama wachezaji waliocheza juzi pale Morocco ni wachezaji wenye viwango vizuri, wachezaji wanacheza vizuri lakini kama sisi hatujaangalia utaratibu ambao wanafanya wenzetu kuchukua wachezaji wa nje ambao wenye uraia wa Tanzania, nani atafanya? Ninaamini Mheshimiwa Makonda anaweza, ninaamini Mwana FA anaweza. Waende wakamwombe Rais, mikono yake misafi, moyo wake mweupe kwenye michezo, ndiyo mwanamichezo namba moja nchini mwanamichezo ambaye ameonyesha sera yake ya kuinua michezo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunakuja kuwa wenyeji wa AFCON, sasa twende tukawachukue wale watoto wetu wengine ambao wako nchi za nje ambao ruhusa ya kisheria inawasumbua kurudi ndani. Naamini hilo linawezekana kwenu. Hakuna kitu kizuri kama kuchanganya ujuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwenye hili kama tunapata Rais mwenye maono haya ya Mama Samia wa leo hii, huyu Rais anazaliwa mara moja tu anatoka mara moja tu, kama tumempata huyu tumtumie vizuri. Michezo ni ajira michezo ni pesa michezo ni utajiri na yeye ameweka mguu kati kwenye michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoka kwenye michezo tunajua Mheshimiwa Rais ameleta pesa kwa ajili ya Mfuko wa Sanaa na anafanya vizuri. Utaratibu wa Mfuko wa Sanaa umekwenda kisheria sana. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya sanaa aende akamsaidie Rais kwenye hili. Wasanii wanategemea kupata pesa hapa, waende kama kuna utaratibu wa kisheria sisi ndiyo watunga sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Daktari Tale Tale, namshauri Mheshimiwa Waziri walete sheria hapa, tuwasaidie wasanii. Kama kuna utaratibu wa kukopeshwa hizi pesa ambazo Mheshimiwa Rais amezileta wapewe. Kama utaratibu huu ni mgumu tunauona ambao wameujenga, eti ninataka kukopa pesa ambayo ameileta Rais kwa furaha yangu ninataka niweke nyumba, si kila msanii ana nyumba. Hili neno nilisema huko nyuma na Mheshimiwa Rais juzi ametilia msumari kwenye hotuba yake amesema anataka wasanii vijana wawe na furaha: furaha sioy kukosa kile alichokileta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho ambacho ningependa kukisema na kupenda kukisifia kwa Mheshimiwa Rais wetu, mimi Hamis Shabani Taletale kwenye Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ametuletea Mradi wa Morong'anya wa zaidi ya bilioni 23, ule mradi unalisha maji vijiji zaidi ya 19. Kwenye Kata yetu ya Tomondo, tulikuwa tunakunywa maji ya Nzasa, leo hii tunakunywa maji baridi, nani kama Mheshimiwa Dkt. Samia? Halafu leo hii atoke mtu amseme Mheshimiwa Dkt. Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakunywa maji baridi kutoka vijijini, leo hii ameleta Mradi wa bilioni nne kwenye Kata yetu ya Mkambarani. Vile vile sisi tumekuwa hifadhi ya kupeleka maji mjini kutoka kwenye Bwawa la Kidunda. Leo hii tuna uhakika Watanzania wanaoishi Dar es Salaam wanakwenda kupata maji kutoka kwa sisi Wanamorogoro Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuyasema haya machache ninarudia tena Mheshimiwa Dkt. Samia siyo mnyonge na wala hatumnyongi, tunampa haki yake. Ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)