Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

Hon. Asya Sharif Omar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia siku ya leo kuweza kusimama katika Bunge letu hili Tukufu la Kumi na Tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze ku-support au kuchangia hotuba ambayo aliwasilisha Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 14 Novemba, 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi Taifa, kuwashukuru jumuiya yangu ya UWT Taifa, kuwashukuru sana wapigakura wa Mkoa wangu wa Kaskazini Pemba, Jumuiya ya UWT wanawake kwa kuendelea kuniheshimisha na kuendelea kuniamini kwa uadilifu mkubwa kuweza kunichagua na hatimaye leo nikasimama kuwa Mbunge. Sitawaangusha, na nitaendelea kufuata nyayo za Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kuwatumikia wananchi kwa unyenyekevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo katika hotuba ile ya Mheshimiwa Rais utajikita kwenye Wizara yetu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Lazima wananchi tumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametufanyia makubwa wananchi wa Tanzania tukiwemo wanawake. Ameweza kutoa shilingi bilioni 10.5, fedha hizi tayari zinapatikana NMB Bank na ni kwa malengo makubwa ya kutusaidia wanawake tukiwepo wafanyabiashara wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ile ya Mheshimiwa Rais ya tarehe 14 Novemba, ilijaa maono ya kiuchumi ambayo imekwenda kumnyanyua mwanamke na mfanyabiashara mdogo kutokana na maisha tegemezi. Shilingi bilioni 10.5 zile ambazo tayari zimeanza kuwanufaisha kwa wale wananchi ambao wamesajiliwa na wapo sahihi katika kukopesheka na tayari wameanza kunufaika nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hatuna cha kumlipa ila tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu atamvisha joho na huruma, lakini atampa malipo yake ya duniani na kesho tunapokwenda. Ametunyanyua wanawake, leo wanawake tumeondokana na maisha tegemezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi bilioni 10 ile imeenda kunufaisha babalishe, mamalishe, wasusi, wafanyabiashara ndogo ndogo, na bodaboda. Vijana wetu wote hawa wameweza kunufaika na pesa hizo. Nani kama Mheshimiwa Mama Samia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuseme ukweli, Watanzania Mheshimiwa Dkt. Samia ametuheshimisha. Kufuatia mkopo huu ambao umenyanyua hali zetu wanawake wa Tanzania tena wanyonge, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ametujengea uwezo wanawake mjini na vijijini, tena wadogo wadogo, tumeweza kukopesheka bila ya masharti magumu. Masharti nafuu yametupa fursa ya kupata fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, hadi hapa ninazungumza, kulikuwa na kilio kikubwa kwa wanawake wenzetu huko chini walikuwa wanapitia magumu. Wamenyanyasika, lakini Mama Dkt. Samia kawa mkombozi wa wanawake wa Tanzania na hasa wanyonge. Tunataka nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokitaka ni kuendelea kumwombea dua Mheshimiwa Rais wetu na tutamuenzi kwa nguvu zote kwa sababu ametuheshimisha wanawake. Kama tunavyofahamu, mwanamke ndio kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo, lazima niseme ukweli, ninampenda sana Mama Samia. Ninasema kwa hisia, wanawake leo tuliopo chini tumeweza kumiliki kujenga majengo sisi wenyewe. Kama haitoshi, sasa hivi tunasomesha watoto wetu. Kama haitoshi tumekuwa wafanyabiashara wakubwa, tunakwenda mpaka nchi za Kiarabu. Sisi wanawake tunapanda ndege tukishuka tunapishana na wakina baba. Ukija masokoni tunaongoza; ukija kwenye business tunaongoza; ma-pilot tunaongoza. Wanawake wote tunaongoza kwa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jeuri hii tumeipatia kutoka kwa Mama Samia, ameweza kutujengea nguvu ya uwezeshaji. Kwa nini tusiseme? Lazima tuseme, Mama Samia tunakushukuru umenyanyua hali zetu wanawake, tena wale wanyonge kabisa umetunyanyua. Leo ninavyozungumza, mimi ni Mbunge wa wanawake UWT, lazima nitetee wanawake wenzangu, lakini lazima nijenge heshima aliyotupa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani ilikuwa wanawake tunanyanyasika, ndoa zetu hazitulii, lakini shilingi bilioni 10.5 zimeenda kujenga heshima ya ndoa zetu. Ni kweli zimekwenda kujenga heshima ya ndoa zetu. Baba anahangaika na mambo mengine mpaka wanaogopa, maana yake akitoa fedha ya mboga, tunatoa fedha ya shule ya mtoto; akianza kujenga msingi, sisi tunanyanyua juu tunaezeka nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni shilingi bilioni 10.5, lakini imetujengea mazingira mazuri, tumekuwa na afya ndani ya majumba na ndoa zimeimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa wanawake tunahangaika na kaushadamu. Kaushadamu ilituumiza wanawake hasa wa vijijini, tulikuwa tunatolewa magodoro nje, tunatolewa vikombe vyetu, hatuna amani. Mume unampenda lakini unamchukia, lakini Mama Samia kajenga heshima ya familia zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza mchango wangu huu ninaomba sasa niseme, fedha hizo zipo na zinaendelea kutolewa NMB mjini na vijijini na riba yake ni ndogo, asilimia saba. Kwa hiyo, hii utaona namna gani Mama amekusudia kumnyanyua mnyonge na siyo tu kutoa fedha na fedha zinapatikana NMB. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, tuitumie fursa hii kuhakikisha wanawake hawa zinawafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, niseme ninashukuru sana. Ninaomba kuunga mkono Hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)