Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji katika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitaanza kuongea kwamba, mimi huwa kwenye ukweli ninazungumza ukweli, kwenye kona huko huwa siendi. Nitasema yale ya ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais katika Jimbo langu la Gairo kwa vitu ambavyo ametufanyia wananchi wa Gairo. Kwa mfano, tumepata madaraja ambayo yalikuwa yanaua watu kila siku. Nilimwomba mwaka juzi 2024 alipopita pale, tunashukuru madaraja yamekwisha ya shilingi bilioni 16, la mita 120 na la shilingi bilioni 11 la mita 80. Madaraja ya Chakwale na Nguyami yamekwisha. Ninamshkuru kwa kuweka barabara hiyo katika feasibility study kutoka Gairo hadi Kilindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru kwa Gairo kutupa barabara ya lami ya kilometa 57 kutoka Gairo mpaka Nongwe. Tunamshukuru kwa mradi wa maji wa shilingi bilioni 21 na shilingi bilioni 9.9, takribani shilingi bilioni kumi. Kwa hiyo, lazima niseme ukweli, tangu mwaka 2005 maana mimi nimeingia tangu mwaka 2005, na bado nipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya kustaafu kwa heshima, hiyo hakuna, kwa sababu mimi nilimtoa mtu, na mimi mpaka nipate kura mbili ndipo najua hapa sasa unastaafu kwa heshima. Kwa hiyo, kwa wale wanaoviziavizia bado nipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tangu niingie mwaka 2005, nimekaa na Mheshimiwa Kikwete na kabla ya hapo nimekaa na Mheshimiwa Mkapa, kama Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kupitia viti 20. Nimekaa na Mheshimiwa Magufuli pamoja na yeye, lakini lazima niseme ukweli. Katika kipindi cha Awamu ya Sita, Gairo na Tanzania imepata vitu vingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wakati wa nyuma wananchi walikuwa wanajenga wenyewe shule za msingi; wakati wa nyuma zahanati zote walikuwa wanajenga wananchi; wakati wa nyuma tulikuwa hatuna hospitali za wilaya, wengi wamezungumza, tangu Uhuru, watu walikuwa hawana hospitali za wilaya. Sasa, wakati wake tuna sekondari zinajengwa na Serikali, tuna zahanati zinajengwa na Serikali, tuna ambulance, kama Gairo ina ambulance takribani saba ziko pale. Kwa hiyo ni lazima tushukuru. Tuseme ukweli, kwenye mahali pa ukweli tuzungumze ukweli, kwamba kazi aliyoifanya huyu mama yetu ni kazi nzuri. Hata kama kuna mtu ana kinyongo, hicho ni kinyongo cha binafsi. Kwa hiyo, huwezi kumlazimisha mtu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukweli huo huo katika ukurasa wa 37 katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, amezungumzia uwajibikaji na utawala wa sheria; na amezungumzia kwa baadhi ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli katika nchi yetu, hapa amezungumzia habari ya watu wabadhirifu wa fedha ambazo zilikuwa ziende kwa wananchi, zinyanyue maisha ya wananchi, kama yeye lengo lake linavyotaka. Amezungumza kwamba kuna baadhi ya watu ambao ni mafisadi. Ninasema katika nchi hii sasa hivi mafisadi hawa siyo kwamba wanapiga kidogo, wanapiga kiuhakika. Ni walaji na ni walafi, na wanafanya vitu kama vile wananchi wa sasa hivi hawana elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tufahamu sasa hivi ukienda sehemu yoyote, hata kama kwenye kijiwe cha bodaboda utamkuta mtu wa chuo kikuu, utamkuta wa Form Six, utamkuta wa Form Four utamkuta wa Darasa la Saba na utamkuta na asiyesoma. Wakikaa pamoja pale wakianza kuongea wote wana kuwa wako University. Kwa hiyo, hawa watu siyo kwamba hawaelewi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta mtu yuko Serikalini ana GPA labda ya 2.5 halafu yule ambaye yupo bodaboda ana four. Halafu huyu jambazi anamtuma bodaboda, yule wa GPA 4, nenda kapeleke misumari pale, peleka hapa, halafu huyu naye mjanja anajua mshahara wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tujue. Hizi sheria za TAKUKURU kama ziko kidogo zimelegea, walete basi tubadilishe. Watu kila sehemu wanajengajenga majumba, nini. Watu wanaona. Tusizungumze sisi hapa kama Wabunge wa CCM ambao tuna uchungu, tuzungumze ya leo, kwamba, je, tunayozungumza leo tunajifurahisha leo? Je, ya mwaka 2030 nayo tunayasahau. Tukizungumza ya leo tujue kuna mbele huko, kuna mwaka 2030. Je tunakwendaje kwenye chaguzi zetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa tulikuwa tunamwomba Mheshimiwa, na sio Mheshimiwa Rais, kwa sababu Urais ni taasisi. Hata kama Mheshimiwa Rais anajitahidi vipi, lakini hawa watu wa chini yake wanamsaidiaje? Wanayaona haya mambo yanayofanyika, hao watu wa chini na wamekaa kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi mfanyabiashara sipendi ufisadi wala sipendi wezi, kwa sababu mimi ninafanya biashara kwa miaka mingi, ninahangaika, nanunua hiki, nafanya hiki halafu kinakuja kijitu kinaiba kinaingia kwenye biashara yako. Unakingoja kifilisike, kwa sababu kitafilisika tu, lakini tayari kimeshakudhuru ndani ya miaka mitano miaka sita kwenye ile biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu nimemwona kabisa kwamba anahangaika sana, na ameanza vizuri sana kwenye masuala haya. Sasa tunamwomba, kama ameanza vizuri kwenye masuala ya kuangalia watu wezi wa nchi, maana yake tusikae hapa tu tuna kazi ya kusema aah sisi, sisi, sisi, kwenye watu, wezi wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameanza vizuri, na tumeona ameita wale watu wa maadili na watu wa sehemu nyingine. Watu wa maadili siyo wanakuja kwa Wabunge, Mbunge mimi nakutana na fedha ya Serikali wapi? Sikutani nayo mahali popote, lakini Mawaziri na watu wa chini yao ndio wanaokutana na fedha ya Serikali. Kwa hiyo, kama ni vibaka, basi ni huko kwenda huko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameanza vizuri, nami ninampongeza, na aendelee hivyo hivyo, na amerudisha angalau imani kwa wananchi. Wamsaidie Mheshimiwa Rais. Rais hawezi akawa anaangalia mwizi yuko Gairo Halmashauri, akaangalie sijui yuko Bukombe, akaangalie sijui yuko Rorya, haiwezekani kitu kama hicho, na wawe wanafuata ushauri wa kitaalamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo vinahusika kwenye masuala ya ushauri, wachukue ushauri, waangalie. Maana wananchi wa sasa hivi sio wajinga, wanajua kabisa hili jengo ni la fulani, hiki kitu cha fulani, huyu yupo Serikalini ni mwizi aliyekubuhu. Wengine tena wanakwenda hata hawana aibu, utakuta wanawanunulia watu mishkaki, wanawanunulia nini. Kama hawana, wengine waje, mimi nitawaandikia wezi wote, maana na mimi ni Usalama wa Taifa wa kujitegemea, nipo hapa, wasiwe na wasiwasi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaambia, katika kitu kinachozungumza, na ndiyo maana mama amekizungumza hapa anataka usaidizi kutoka kwa wasaidizi wake. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais alikizungumza kwa uchungu sana. Je, wasaidizi wake wanafanya hizo kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko Mawaziri wasikae tu hapa wanangoja nani atakuwa Rais baada ya mwaka 2030. Hata sisi huku nyuma, mimi nilikuwa ninaongea na Mheshimiwa Maganga. Mheshimiwa Maganga atakuwa hapa, maana hata mimi nina-trot, maana lazima tujue, wasikae huko tu, kila huyu anataka hiki. Hata sisi huku nyuma tulikuwa tuna-trot. Nilikuwa ninaongea na ndugu yangu Mheshimiwa Jafari hapa, yupo mwingine hapa anataka Uwaziri Mkuu mwaka 2030. Msiwe na wasiwasi tutakuwenda huko. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, anafanya kazi nzuri. Ninaomba pale pale, na timu yake wote, na ninajua katika timu yake ya Mawaziri waliopo sasa hivi wengi ni wazuri, ila waangalie huku chini. Hata hapa Wabunge hawa wengine, usione hawapigi kelele, inawaingia kichwani, wanajua ninachokiongea na wanakielewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda sehemu fulani, utakuta jumba la fulani, jumba la fulani. Kuna mmoja hapa alijenga nyumba akaandika kabisa na jina lake fulani tower. Jamani, sasa huko tunafanyaje? Sisi wanatupa kazi ya ziada. Mtu anayekupenda atakwambia ukweli, mtu mnafiki atatoka hapa atapiga debe akitoka huko nje, aah tunaenda vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina mengi, nashukuru sana, ahsante sana. (Makofi)