Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuweza kuchangia leo kwa mara ya kwanza. Kwa kuwa ndiyo tumeanza Bunge hili na mimi ni mchungaji wa timu ya mpira wa miguu ya Bunge na mshauri wa kiroho kwa baadhi ya Wabunge wenye ugonjwa wa kiroho, baadhi siyo wote ambao wanapenda ushauri, nianze kwa kutamka maneno ya Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kitabu cha 1Timotheo 2:1-2 inasema: “Basi kabla ya mambo yote nataka dua na sala na maombi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote. Tunaanza kwanza kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka tuishi kwa utulivu na amani katika utauwa wote na ustahivu.” Neno lingine katika Warumi 13:1 linasema: “Na kila mtu na atii mamlaka iliyo kuu, maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu na ile iliyopo imewekwa na Mungu.” Nashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, tunamwombea Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo ya maandiko haya matakatifu, Mungu akampe hekima, maarifa, ulinzi na afya ili tuweze kuishi kwa amani, utulivu kama maandiko matakatifu yanavyosema. Andiko lingine Jeremiah 29:7 Inasema, “Kautakieni amani mji ule ambao nimeufanya mkachukuliwa mateka, mkauombee kwa Bwana kwa maana katika amani yake mji ule na ninyi mtapata amani.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niwaambie ndugu zangu, tunao wajibu wa kuliombea Taifa letu la Tanzania, kwa maana anasema katika amani yake katika Taifa la Tanzania, katika mafanikio yake, ndivyo na sisi tutakavyofanikiwa. Ndugu zangu haya ni maelekezo ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana kutuongoza. Sisi watu wa Kalenga tulimpa kura za kutosha yeye mwenyewe alivyokuja kule aliona bashasha, na tulifanya hivyo tulikuwa na sababu. Jimbo la Kalenga limekuwa na maendeleo makubwa, lakini hapa tunajadili bajeti ya Kitaifa, lakini ni mfano, ndiyo maana alivyokuja tulimpokea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye hiki kitabu kuna mambo mengi mazuri, yaani muda hauwezi kutosha kueleza, lakini nikianza na kwenye maji ambako mimi nimekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bunge lililopita, nimeiona nia iliyowazi sana ya Mheshimiwa Rais ya kufanya mapinduzi kwenye sekta ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaingia tulikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 640. Mpaka sasa tayari tumeshaweka kiasi cha shilingi trilioni moja kwenye sekta ya maji. Hiyo inaonyesha nia iliyonyooka, nia ya wazi ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba huduma hii ya maji inapatikana katika Taifa la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi karibu 1,000 ambayo inatekelezeka katika maeneo mbalimbali, miradi karibu 878 vijijini, miradi 217 ikitekelezeka mijini yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.3. Je, tumemaliza changamoto ya maji? Hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotufurahisha ni kuona nia ya Mheshimiwa Rais hata kwenye hii hotuba yake katika ule ukurasa wa 17 ameonyesha kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameathiri upatikanaji wa maji katika maeneo mengi hata ya Dar es Salaam hapa mmekuwa mkizungumza, lakini tunafurahi tunavyoona Rais ameanza kutekeleza mipango mikubwa ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, bwawa lile la Kidunda ambalo lilikuwa ni mipango ya Mwalimu Nyerere, Mama ameanza kulijenga. Kwa hiyo, niwaambia ndugu zangu wa Dar es Salaam, ndugu zangu wa Pwani na ndugu zangu wa Morogoro kwamba, baada ya kukamilisha bwawa hili ukanda huo tutakuwa tumemaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mipango ya kutumia maji kutoka katika Ziwa Nyasa, maana yake Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria katika mpango wake Rais wa kutengeneza ile gridi ya Taifa, maana yake hata ndugu zangu kule Kalenga, ndugu zangu kule Iringa tutawapelekea maji kwa mfumo wa gridi kama mnavyoona umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Watanzania wawe na matumaini makubwa na Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu mipango yote imeonyesha kwenye hotuba yake na sisi tuko hapa kusimamia kuhakikisha kwamba inatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwa sababu katika ahadi yake ya zile siku 100 alieleza kwamba ataajiri watumishi 12,000. Mimi nimpongeze na nimshukuru kwa sababu Jimbo langu la Kalenga katika Halmashauri yetu ya Iringa Vijijini mimi na Kaka yangu Mheshimiwa Lukuvi tumeshaletewa wafanyakazi 194 kuonesha kwamba alichokisema anamaanisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye bima ya afya, tayari tumeshapewa kitita cha 150,000 kwenye familia hizo. Ni hatua kubwa ambazo Mama ameanza kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta za uzalishaji, tukienda pale hasa nikizungumzia uvuvi na mifugo, tumeona mapinduzi makubwa kwenye kununua boti mbalimbali na uzalishaji wa vifaranga ambavyo vimekuwa vikitolewa kwa watu katika vizimba, Rais amekuwa akiweka ruzuku huko. Kazi kubwa zinafanyika na sasa anaeleza katika ukurasa wa 22 wa hotuba yake kwamba, tunakwenda kuongeza maeneo ya malisho kutoka heka 3,900,000 kwenda 6,000,000. Sasa hapa ni ushauri tu kidogo kwa wanaomsaidia Rais, malengo yake mazuri ameshaonesha hapa mwongozo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo tunaipata kwenye hili eneo la ufugaji pamoja na kuwa kwamba haya maeneo tunayatenga, lakini wafugaji wetu hawa wakina Chacha, kutoka kanda hizi za wafugaji, changamoto za kuhamisha hamisha mifugo kutoka eneo moja kwenda eneo lingine, hiyo ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotakiwa kukifanya sisi kama Serikali ni lazima tu-commercialize masuala ya mifugo, tufanye kuwa ufugaji wa kibiashara. Kwa maana hii, Serikali iwekeze fedha katika maeneo haya ambayo tunayatenga, tuhakikishe tumeweka majosho, tuhakikishe tumejenga mabwawa ili tukiwatengea haya maeneo, wawe na maji, wawe na majosho katika maeneo haya. Tukifanya hivyo, hawa watu wataacha kuhamahama, kwa sababu mara nyingi wanahama kutafuta majosho pamoja na kutafuta maji. Hii pia itatusaidia kujua idadi ya mifugo halisi tuliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo mingi hapa Tanzania haijulikani, watu wengi wafanyabiashara inawezekana baadhi ya Wabunge na wafanyabiashara nyingine wananunua hawa ng’ombe wengi wanawatupa tu huko porini. Hii ni biashara kubwa ya wafanyabiashara wengi kwa sababu wanapata faida, kwani kule hakuna kodi. Sasa tukiweza kuiratibu hii mifugo kwa namna hii, kwanza Serikali itaweka mfumo mzuri wa kupata fedha kutoka katika mifugo na tutakuwa tumewafanya wasiendelee kuharibu mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mengi, lakini mwisho nisisitize tu kwenye hili suala kwenye mambo ya habari na utamaduni pale. Nimeona mipango ya kujenga ukumbi wa maonyesho, lakini nilikuwa nashauri, hapa Dodoma tungejenga ukumbi mkubwa kwa ajili ya masuala haya ya makumbusho ili mambo yote ya kimila na tamaduni za mikoa yetu mbalimbali ziweze kupatikana katika eneo moja, watu waendelee kusoma na kuendelea kutambua historia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. ninaona kengele ya pili imeshagonga. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)