Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kipekee kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Vwawa kwa kuniamini na kunichagua kuendelea kuwawakilisha hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa na kwa heshima kubwa nitumie nafasi hii kumpongeza sana Spika wa Bunge letu, Naibu Spika, na ninyi Wenyeviti ambao tumewachagua leo ambao ndio mtakuwa viongozi wetu wa kuliongoza Bunge hili na kutuongoza sisi. Ninawapa hongera sana, sana, sana ili muweze kutekeleza majukumu ya Kibunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii kutoa mchango wangu katika hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa tarehe 14 Novemba, 2025. Hotuba ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni hotuba nzuri, hotuba yenye maono, hotuba yenye mtazamo mpana, hotuba yenye nia ya kuleta maisha mazuri kwa wananchi wa Tanzania. Hotuba ile ili-cover maeneo yote ya msingi ambayo kama tukiyawekea mikakati nchi yetu itapiga hatua kubwa katika kila eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kutumia slogan yake ya Kazi na Utu inaonyesha kwamba, anasema kwamba bila kufanya kazi, Taifa haliwezi kuendelea. Kwa hiyo, lazima Watanzania wote, tufanye kazi. Pia anasema, tunapofanya kazi tuheshimu na utu wa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mungu alimuumba binadamu, akampa macho, lakini yale macho hakumpa, ajiangalie yeye, alimpa macho ili aangalie watu wengine, aangalie mambo mengine ndiyo ayaone. Sasa maana yake kiongozi yeyote unapopewa Madaraka, kazi yako ni kuangalia watu wengine wanahitaji nini uweze kuwasaidia, na haya yameonekana katika maono ya Mheshimiwa Rais. Ninampongeza sana kwa namna anavyoiona na kuitazama nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimwangalia Mheshimiwa Rais anatamani Watanzania wawe na maisha mazuri, anatamani nchi yetu ipige hatua kubwa kiuchumi, kijamiii na kisiasa. Hayo yanajidhihirisha, kwenye hotuba yake, anasema: “Uchumi wa Tanzania ulikua kwa 5.6%,” lakini matamanio yake ni kutaka kuona uchumi unafika zaidi ya asilimia saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi kama Wabunge kwa kushirikiana na Serikali yetu tunatakiwa tuweke mikakati ya kuhakikisha uchumi huu unakua zaidi ya asilimia saba ili kusudi maisha ya Watanzania yaweze kuwa mazuri, kwa sababu ukikua chini ya asilimia saba, wakati kuna mfumuko wa bei, wakati idadi ya watu inaongezeka kwa 3.2% na mfumuko wa bei uko kwenye asilimia mbili, maana yake yale maisha mazuri tunaweza tusiyaone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuyaone maisha mazuri, lazima uchumi huu tusaidiane, tufikirie kwa mapana, ukue kwa zaidi ya asilimia saba, ndipo maisha yetu yatakuwa mazuri. Kwa hiyo, hilo kwa kweli ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa maono haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anasema ili maisha yawe mazuri lazima tuangalie sekta za uzalishaji, sekta zile zinazohusu watu wengi. Sekta za uzalishaji anasema ni kilimo, na hii inaonekana hata katika kipindi kilichopita, tuliona bajeti ya kilimo imeongezeka mpaka kufika shilingi trilioni 1.2. Ni matumaini yangu huenda tena ikaongezeka mwaka huu. Maana yake nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania walio wengi wako kwenye kilimo. Kwa hiyo, ukiendeleza kilimo maana yake utakuwa umeyaboresha maisha yao. Ukiendeleza kilimo ajira zao zitakuwa ni nyingi, ukiendeleza kilimo Taifa litapata fedha za kigeni, na ukiendeleza kilimo, uchumi wa Taifa letu utakua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema ukichukua sekta ya uvuvi, sekta ya mifugo, hizi ni sekta ambazo zina watu wengi. Hizi ni sekta ambazo anasema ziongezewe bajeti na sisi kama Bunge lazima tuunge mkono kuongezea bajeti kwenye sekta hizi za uzalishaji. Pia anasema, sekta ya madini iendelee kutoa mchango mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni moja ya nchi zilizobarikiwa kuwa na madini ya kila namna. Tuna madini mengi ambayo mpaka sasa hivi nina imani kama tumechimba hata 1/5 hatujafikia. Sasa ni lazima tuweke juhudi na maarifa kuhakikisha kwa kweli tunachimba haya madini, yanatunufaisha katika nchi yetu. Hiyo ni moja ya sekta muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa vivutio vingi vya utalii. Kwa hiyo, lazima tuweke mkazo kwenye sekta ya utalii. Sekta ya Utalii ina uwezo wa kutuingizia fedha nyingi sana. Nchi za wenzetu tunaona, nchi nyingine watalii ni wengi sana. Sasa hivi sisi ndiyo tumefika watalii karibu milioni tatu na sisi angalau tunasema tumejitahidi, lakini kwa vivutio tulivyonavyo, kwa maliasili tulizonazo, bado tunahitaji kuwekeza zaidi katika kuboresha sekta ya utalii ili iweze kuwavutia watu wengi zaidi na tuweze kunufaika kupata mapato mengi yanayotokana na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine zinapata watalii wanafika mpaka milioni 100 kwa mwaka. Nchi kama Ufaransa, Hispania na nchi nyingine zinapata watalii wengi sana. Katika Afrika nchi kama Morocco inapata zaidi ya watalii milioni 16. Nchi kama Egypt inapata watalii wengi. Tanzania ambayo ina vivutio, ni nchi ya pili duniani kwa vivutio, kwa hiyo, tunahitaji kuongeza mikakati ili kuvutia watalii zaidi, kujenga hoteli, kujenga vivutio mbalimbali ili tuweze kupanua wigo wa utalii hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweka mkazo, pia ametufundisha, anatuambia michezo siyo burudani tu, michezo pia ni Uchumi. Amewekeza nguvu kwenye michezo. Tumeona jinsi ambavyo amejitahidi sana ku-sponsor michezo yetu, ndiyo maana hata sasa hivi Tanzania kimichezo tumepanda. Tumeona hata timu zetu zimepanda. Anatuambia, michezo ni biashara kama biashara nyingine. Kwa hiyo, tunahitaji kuwekeza zaidi kwenye michezo, pia tutaimarisha afya zetu, na vile vile tutapata fedha nyingi zinazotokana na michezo. Ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sasa tunakuwa ndiyo host wa mashindano ya AFCON yanayofuata. Tanzania tunawekeza kwenye viwanja, kwa hiyo, ni lazima iende sanjari na kuwekeza kwenye vipaji vya vijana watakaoshiriki katika michezo hiyo waweze kutuletea faida zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo Mheshimiwa Rais ameleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya elimu. Anasema lazima tuwe na human development plan. Human development plan tunaiona ambavyo tumebadilisha kwenye elimu, tumeanza kwenye shule za msingi, shule za sekondari, tumekuja na mitaala mipya, na hii imekuwa adopted na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais anasema lazima twende zaidi ya hapo; vyuo vyetu vya kati, vyuo vikuu mitaala yao lazima ibadilishwe iendane na mahitaji ya leo ya kisasa ili tujue viwanda vyetu vinahitaji wataalam wa namna gani? Tunahitaji ujuzi wa namna gani ili hii nchi iwe na wataalam wa kujitosheleza na tuweze kupiga hatua kubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo, lazima tujenge miundombinu. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kule Vwawa alitupatia fedha tukajenga kilometa kadhaa za lami, na sasa inajengwa kilometa 21 kutoka Njiapanda ya Iyula kwenda mpaka Idiwili. Tunamwomba azidi kutupatia fedha zaidi tujenge barabara ya lami kutoka Vwawa kwenda Isalalo kutoka maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani tukifanya haya, tutawafanya wananchi wa Tanzania waishi maisha mazuri na tuweze kufikia malengo tuwe na furaha na tuweze kuifurahia nchi yetu na utamaduni wetu na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi, ahsante sana. (Makofi)