Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais wakati wa ufunguzi wa Bunge, tarehe 14 Novemba, 2025. Naanza kwa kusema kwamba, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ana karama ya uongozi.
Mheshimiwa Spika, ukitaka kujua kwamba, ana karama ya uongozi ni pale alipochukua nafasi ya Urais, katika kipindi cha miaka minne amehakikisha kwamba anatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2025 kwa kiwango cha hali ya juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wote tumeshuhudia mambo ambayo yamefanyika ndani ya kipindi cha miaka minne. Tumeshuhudia ujenzi na ukamilishaji wa SGR. SGR hii siyo suala la usafiri tu, ni pamoja na usafirishaji. Tumeona faida kubwa ya SGR, hasa kwa wenzetu wa Mkoa wa Dodoma, wanawake wamepata faida kubwa ya kusafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kufungasha biashara zao na hatimaye wanarudi kuja kufanya biashara Dodoma. Hiyo ni fursa kubwa ambayo wanawake wameipata na kuitumia.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, namwita Mheshimiwa Paresso aje kukalia Kiti.
Mheshimiwa Chatanda endelea tu.
Hapa Mwenyekiti (Mhe. Cecilia D. Paresso) Alikalia Kiti
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukamilisha ujenzi wa SGR. Tunamwomba aendelee kukamilisha maeneo yaliyobakia ya kutoka hapa Dodoma kuelekea Mwanza ili watani wangu wa Mwanza na wenyewe waweze kufaidi matunda ya SGR. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakupongeza kwa kupata nafasi ya Uenyekiti. Hongera sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kushuhudia suala la Bwawa la Mwalimu Nyerere. Bwawa hili la Mwalimu Nyerere limewezesha kuongeza umeme katika nchi yetu. Hapo mwanzoni umeme ulikuwa unakatikakatika, sasa hivi umeme unapatikana kwa muda wote. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kulisimamia kuhakikisha kwamba, Bwawa la Mwalimu Nyerere linakamilika na ndoto zile za Hayati Baba wa Taifa zinakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Rais wetu, na tunajua kabisa kwamba, suala la upatikanaji wa umeme linawasaidia sana wanawake wajasiriamali. Wanawake wale ambao wameanzisha saluni zao, na shughuli zao zinazohusiana na umeme, wananufaika kupitia mradi huu wa Bwawa hili la Mwalimu Nyerere ambapo umeme sasa unakuja bila kukatikakatika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia uzinduzi wa meli ya MV. Mwanza, Wananchi wa Mwanza, Kigoma na Kagera wamepata bahati ya uzinduzi wa meli hii ambayo itawanufaisha kiuchumi hasa ikizingatiwa kwamba, inakwenda hadi katika nchi za jirani. Kwa hiyo, wanawake watanufaika sana kupitia meli hii kwa ajili ya kwenda kutafuta na kufungasha mali kupitia kwenye nchi za jirani, hususan kule Uganda; watafungasha mali zao, watarudi kuja kuuza. Kwa hiyo, watajiinua kiuchumi kupitia hii Meli ya MV. Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia Mheshimiwa Rais katika kipindi cha miaka minne, ameweza kujenga shule za msingi kuanzia awali hadi sekondari, lakini kubwa zaidi alilolifanya ni kuhakikisha anajenga shule za sekondari za wasichana za mchepuo wa sayansi kwa kila mkoa, tunamshukuru sana. Tunajua lengo lake anataka mabinti waweze kupata elimu ili kuendana na elimu kidunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru tena Mheshimiwa Rais, katika mpango wake amesema kwamba, atajenga shule kila Mkoa, za wavulana za vipaji. Kwa hiyo, nalo hilo tunaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais katika mipango yake hiyo na tunaomba basi kila mkoa uandae maeneo kwa sababu, Rais ameshasema kwa vyovyote vile atatoa fedha ili kusudi shule hizo ziweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, katika kipindi chake cha miaka minne ameweza kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za Wilaya, za Mikoa, hadi za kanda. Hospitali hizi zimeweza kuwekewa mpaka na vifaatiba. Tunaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwarahisishia akinamama wa vijijini kwa kujenga hizi zahanati; walikuwa wanapata tabu kwenda mwendo mrefu kufuata huduma za zahanati kwa ajili ya kwenda kujifungua, lakini sasa wamekuwa na zahanati kwenye maeneo yao na vituo vya afya maeneo ya karibu na kuweza kujifungua karibu. Kwa hiyo, afya za akinamama na watoto zinakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kushukuru suala zima la maji, Mheshimiwa Rais alipokuwa Makamu wa Rais alisema kwamba, atahakikisha anamtua mwanamke ndoo kichwani. Jambo hilo hata alipoingia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi chake cha miaka minne, ameliendeleza kwa kununua mitambo ya kuchimbia visima vya maji kwa kila mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelewa kwamba, changamoto hii bado ipo, lakini haina ukubwa kwa kiasi hicho. Tunatambua kwamba, Mheshimiwa Rais, kupitia Wizara ya Maji, hususan kwa kijana wangu Mheshimiwa Aweso, watalisimamia hili, ili ziweze kutimia ndoto za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kumtua mwanamke ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalau kwa wale ambao tayari wameshafanikiwa kupata maji, imesaidia sana kurekebisha ndoa za wanawake na waume zao huko vijijini. Nilipokuwa nafanya ziara, nimekwenda kuzindua mradi mmoja wa maji, wanawake wale wamemshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwapelekea ule mradi wa maji kwa sababu, walikuwa wanapata shida ya kuondoka nyumbani saa kumi usiku, akimuacha mmewe amelala kitandani anakwenda kwenye maji, akirudi bado anapata mkongāoto kwamba, kwanini amechelewa kurudi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais amewasaidia kuimarisha ndoa zao kwa upatikanaji wa majisafi na salama huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ndugu zangu wananchi wa Tanzania tuendelee kumwombea Rais wetu, tuendelee kumsaidia Rais wetu ili aweze kutekeleza mambo mengine mazuri ambayo amejiwekea katika Mpango wa Maendeleo ambao tumeupitisha kipindi kilichopita cha miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukue nafasi ya kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, ahsante sana. (Makofi)