Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyoko Mezani, ambayo ni Hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Taifa letu. Nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, na wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi ya kusimama mbele ya Bunge siku hii ya leo.
Mheshimiwa Spika, pia, nawashukuru sana wananchi wa Urambo na familia kwa jinsi ambavyo wananipa ushirikiano mpaka napata nafasi ya kuendelea kuwa Mbunge katika jimbo hilo. Nawashukuru sana. Halikadhalika nimepata ushirikiano mkubwa wa Serikali ngazi zote za mkoa, wilaya na Chama chetu cha Mapinduzi katika kuhitimisha Ubunge wangu uliopita, lakini pia, katika kuanza awamu hii nyingine ambayo wamenipa heshima ya kuendelea kuwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, sisi wananchi wa Urambo tuna haki na wajibu wa kumshukuru Dkt. Samia kwa kazi kubwa ambayo ametufanyia kwa kupitia Serikali yake. Siyo rahisi kuyasema yote ambayo ametufanyia, lakini nitachukua machache ambayo kwa kweli, ni ushahidi wa jinsi ambavyo wananchi wa Urambo tumenufaika na huduma kubwa tuliyopewa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, shida yetu kubwa Urambo ni maji. Naishukuru sana Serikali, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia, imetupitishia mradi wa maji kutoka Lake Victoria. Tayari mabomba yameshafika, tenki kubwa limeshajengwa, tunachosubiri sasa hivi ni maji tu kuingia, halafu usambazaji uendelee. Tunaishukuru sana Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa ya pili tuliyokuwanayo, ilikuwa ni suala la umeme. Tulikuwa tunapata matatizo makubwa sana kupata umeme, ili tuweze kusaga mahindi, kukoboa mpunga na kadhalika, lakini Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia ilitupa shilingi bilioni 44, kituo cha kupoozea umeme tayari kinafanya kazi. Tunaiomba Serikali yetu, na hasa yeye mwenyewe, akipata nafasi, aje akizindue rasmi, lakini sasahivi umeme Urambo ni furaha tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ametusaidia Mheshimiwa Dkt. Samia, ametupa shilingi bilioni 13 kwa suala la afya. Kwa hiyo, tumejenga vituo vya afya na zahanati, tunashukuru sana. Pia, kwa upande wa elimu, wote ninyi ni mashahidi pamoja na Urambo kwamba tumepata madarasa mapya na walimu wameajiriwa. Kwa hiyo, tunashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, elimu pia, imepewa kipaumbele sana kwetu. Halikadhalika barabara, ninyi mnafahamu, sisi Urambo ni wa vijijini, lakini tulipewa shilingi bilioni 12 kwa ajili ya matengenezo ya barabara. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuliomba pia, tuongezewe barabara nyingine, hasa kwa kupitia TANROADS. Nashukuru sana, majibu yameshatolewa humu Bungeni kila mara nilipokuwa ninauliza. Tumepata barabara ya kutuunganisha sisi Watu wa Urambo na Sikonge. Tumepata barabara inayotoka Usoke inakwenda Tutuo Sikonge, itakuwa ni ya lami. Kila wakati ninapouliza, Naibu Waziri, Mheshimiwa Kasekenya, huwa anajibu kwamba tayari usanifu unaendelea.
Mheshimiwa Spika, tunategemea wakati wowote wilaya zinazotuzunguka pia zitakuwa na lami kwa sababu, tumeshapeleka maombi mengine ili tuendelee kupata huduma za barabara nzuri. Kwa kweli, tuna haki ya kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia kwa mambo mengi ambayo siyo rahisi kuyataja yote kama nilivyosema, lakini tunamshukuru sana na tunamwombea aendelee ili aweze kutuletea maendeleo zaidi.
Mheshimiwa Spika, ukichukua suala la maji, nimelizungumza hapa. Namshukuru sana Mheshimiwa Aweso, kila anaposimama huwa anataja kwamba, tutapata maji kutoka Lake Victoria. Kila ninapomwona yeye ananikumbusha na mimi ninamkumbusha kwamba, Mama Sitta maji ni lazima upate, utachekelea. Kwa kweli, nachukua nafasi hii kuiomba Serikali itusaidie maji yasambazwe. Yatatoka Lake Viktoria sawa, yatafika Urambo, yataingia kwenye tenki, lakini je, yanawafikiaje wananchi kule waliko?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunachoiomba Serikali, tunajua itakuwa ni gharama kubwa, lakini itakuwaje faida sasa kama maji yatafika Urambo, yaingie kwenye tenki, halafu yasisambazwe?
Mheshimiwa Spika, sisi tunajua kwamba, miundombinu ya maji ni ya siku nyingi na tunaamini kabisa haya yatakuja kwa nguvu, kwa hiyo, kupita kwenye mabomba ya zamani itakuwa siyo rahisi. Kwa hiyo, kwa heshima na taadhima naiomba Serikali ituletee mpango mkubwa wa kusambaza maji yafike kwa wananchi, ndiyo ombi langu kubwa ambalo nalileta leo. Pamoja na shukrani, lakini tunaomba maji yasambazwe yawafikie wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halikadhalika ukirudi kwenye maji hayo, Serikali hii imeona kwamba, kutegemea tu maji ya kutoka Lake Viktoria, hapana, tuongezee mabwawa. Wakatupatia shilingi bilioni sita, bwawa linajengwa eneo linaitwa Kalemela, halijakamilika. Nia ya Serikali ni nzuri, lakini tunachoomba sasa ni kwamba, lile bwawa la shilingi bilioni sita likamilike ili lichangie watu wapate maji zaidi kwa ajili ya kilimo, mifugo na matumizi ya nyumbani, lakini pia na ufugaji wa samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, tunaendelea kuishukuru Serikali na kuomba ile mitambo iliyoletwa, yale malori makubwa yenye mitambo ya kuchimbia maji, yaani visima, yaendelee kukaa kwenye maeneo yetu ili tupate visima vingi zaidi visaidiane na bwawa na maji ya kutoka Lake Victoria kwa sababu, kilio chetu kwa muda mrefu kimekuwa ni maji, na kwa kuwa sasa Serikali tayari imeshaanza kutusaidia, basi ikamilishe.
Mheshimiwa Spika, humu Bungeni nimeongea sana mpaka nafikiria kuongea tena wakati wa bajeti sijui, Waziri atanistahimili kwa sababu, Mawaziri wengi wamepita katika Wizara ya Maliasili na Utalii na nimekuwa nikiwaambia hapa kwamba, wananchi wanapenda sana maendeleo yanapoletwa kwao, lakini kitu kikubwa ni ushirikishwaji na elimu. Sisi kwetu kuna kata tatu: Nsenda, Ukondamoyo na Ugala ambao eneo lao limechukuliwa, limekuwa Hifadhi ya Msitu wa Mto Ugala.
Mheshimiwa Spika, nimeongelea sana, Mawaziri wote wanajua na wao wanaahidi kwamba litafanyiwa kazi. Tunaomba sasa lifanyiwe kazi. Wananchi wanashukuru kwa hatua zozote zinazochukuliwa na Serikali katika kuhifadhi misitu na kadhalika, lakini wanaomba maeneo.
Mheshimiwa Spika, tuliomba kilometa tano wapewe kwa ajili ya kuweka mizinga yao nimeenda mpaka kwenye kamati, wanajua, kamati ambayo nashukuru Mheshimiwa hapa amerudishwa kule. Nimekwenda kuwaona kwamba, wananchi hawakatai eneo lao kuwa hifadhi, lakini wanataka wapewe kilometa tano kwa ajili ya kufuga na kuweka mizinga ya nyuki. Wamezoea kupata asali na asali ni zao mojawapo ambalo tunalitegemea sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hili suala Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii achukue hatua ambayo itaonesha kweli, wamesikia kilio cha wananchi kwa sababu, kama nilivyosema, wanahitaji kuelimishwa, lakini pia, na wenyewe wanaomba waongezewe. Kwa hiyo, nitashukuru sana, kama suala hili litachukuliwa na kupewa uzito unaostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halikadhalika jambo lingine ambalo nimeliomba na bado narudia kuliomba ni kwamba, sisi ni majirani wa Ulyankulu, Shinyanga. Hawa ni majirani zetu kwa sababu, ukifika Ulyankulu, mbele tu kidogo pale Kashishi, unakutana na Kahama.
Mheshimiwa Spika, tumeomba tuunganishwe na barabara ya lami ili watu wa Shinyanga wanapotaka kwenda Mbeya wasiwe na haja ya kwenda Tabora. Wanakwenda Tabora kufanya nini? Wakatishe tu pale Kahama, wanakwenda Ulyankulu, wanatoka Ulyankulu wanakuja Urambo, wanakwenda Sikonge, wanaendelea kwenda Mbeya, Katavi na kadhalika. Kwanini wazunguke tena waende kwingine?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ombi letu sisi majirani ni tuunganishwe na barabara ya lami, tutafurahi sana kwa sababu, barabara inafufua maeneo. Kama mnavyoona barabara hii ya zamani iliyokuwa ya Manyoni, miji imechipuka kutokana na barabara ya lami ilivyokuja. Sasa hivi ukipita tu unaona mji kabisa umechipuka na sisi tunataka miji ichipuke kutokea huku Kahama inapita Ulyankulu kwa lami inakuja mpaka huku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nina kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kuiongoza Serikali yake na kujali mahitaji yetu. Kwa hiyo, tunaomba sana, kama nilivyosema hayo yaliyotangulia ya maji, Mwenyezi Mungu ambariki aendelee kutuhudumia.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)