Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili Tukufu katika Bunge hili la Kumi na Tatu, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia uzima na afya njema na Mwenyezi Mungu aliyeniweza kurudi katika Bunge hili la Kumi na Tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Taifa letu la Tanzania. Sisi Wananchi wa Mkoa wa Katavi tunampongeza sana na tunamshukuru sana kwa namna ambavyo ametupa kipaumbele katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo afya, elimu, kilimo na mambo mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sana nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ametupigania sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi katika kipindi chake cha uongozi wake ameweza kuacha alama kubwa sana ambayo wananchi wa Mkoa wa Katavi tutamkumbuka kwa jinsi ambavyo ametusaidia kutuunganisha katika gridi ya umeme ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hilo limetuwezesha wananchi wa Mkoa wa Katavi kuweza kuvutia wawekezaji kuja ndani ya Mkoa wetu wa Katavi na ukizingatia Mkoa wetu wa Katavi sisi ni wakulima wazuri na tuna biashara nyingi na hivyo kutokana na umeme kuwa wa uhakika sasa viwanda vingi vinakwenda kujengwa ndani ya Mkoa wetu wa Katavi. Hivyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wetu wa Katavi wanaendelea kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameboresha sekta ya afya, sekta ya afya tunajua inawagusa sana wananchi wote, lakini akinamama na watoto imewagusa kwa kiasi kikubwa. Kwa kuzingatia kwamba katika kipindi cha uongozi wake vifo vya mama na mtoto vimepungua kwa kiasi kikubwa ndani ya Mkoa wa Katavi hivyo tunampongeza sana na tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika hotuba ya Waziri Mkuu, nianze kwa kumpongeza Waziri wetu Mkuu kwa jinsi anavyofanya kazi alikuja ndani ya Mkoa wetu wa Katavi kufanya ziara na tuliona kazi kubwa anayoifanya hivyo tunampongeza sana, lakini tunampongeza kwa hotuba nzuri aliyoitoa katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunatambua Serikali na jitihada zake katika kuwezesha wanawake kiuchumi pamoja na vijana na watu wenye ulemavu. Katika suala la 10%, wananchi wa Mkoa wa Katavi hususani akina mama, vijana na watu wenye mahitaji maalum wanatoa shukrani za dhati kwa Serikali kwa jinsi ambavyo imesimamia halmashauri zetu kuwawezesha akina mama hao, vijana na watu wenye mahitaji maalum kuweza kupata mikopo ya 10%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wangu wa Katavi tulipoenda kuinadi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi; tulipokwenda kuomba kura, takribani zaidi ya shilingi 9,000,000,000 zilikuwa zimeshatolewa katika vikundi hivi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi kuiomba sana Serikali, bado kuna changamoto, tunahitaji katika mikopo ya 10% tuweze kufanya maboresho katika maeneo machache. Wako akina mama wenye watoto walemavu; akina mama hawa wanapokwenda katika vikundi vya kawaida vya akina mama wengine wamekuwa hawapati fursa na kutengwa kwa sababu wana watoto wenye ulemavu critical unaosababisha wao kutoshiriki vizuri katika shughuli za uzalishaji; hivyo, akina mama wale wengine huona kwamba wakiwaunga katika vikundi vyao hawataenda sambamba na wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ombi langu lilikuwa ni nini? Ombi langu lilikuwa ni kwamba tuangalie akina mama hawa ambao wanawalea watoto wenye ulemavu hususani ulemavu ule critical kwamba ikiwezekana waweze kuingizwa katika ile asilimia mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya LAAC, tulikuwa tukishuhudia kwamba baadhi ya fedha za watu wenye mahitaji maalum zilikuwa fedha zile haziishi. Kwa nini, sasa Serikali isije na mpango wa kuunganisha akina mama hawa katika ile asilimia mbili kwa kuwa wanapoteza sifa ya kuunganishwa na akina mama wenzao? Kwa kuwa wanatumia muda mwingi wa kuangalia watoto wao katika majumba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka nishauri; ni kutokana na Sheria ya Mwaka 2018, katika kifungu cha 37A sheria hii inasema kwamba mikopo hii itolewe ndani ya siku 90, siku hizi ni nyingi sana, tuombe Serikali iweze kuangalia. Kuna baadhi ya maeneo kama Mkoa wangu wa Katavi akina mama wanavyojaza mikopo hii unakuta mama ame-target kwamba afanye biashara ya mpunga, lakini unakuta mpaka muda wa msimu wa biashara umepita, ndio mikopo hii inatoka ndani ya siku 90 ikiwezekana mikopo hii iweze kufupishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tulikuwa tunaomba hawa Maafisa Maendeleo waweze kuwafuata akina mama hawa katika kata zao au katika tarafa kwenda kuwapa mafunzo badala ya kuwakusanya katika halmashauri ili waweze kuwapunguzia adha za kutoa nauli na gharama kubwa kwani wengine wamekuwa wakitokea katika maeneo ya mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine wananchi wa Mkoa wa Katavi, wamenituma kwamba wanaomba sana Serikali iendelee kuwaangalia katika kuunganisha barabara za mikoa na mikoa. Tunaishukuru Serikali tumeunganishwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kutoka Mpanda mpaka Tabora, tunaishukuru sana kwa kiwango wa cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi ya Wanakatavi tuunganishwe na Barabara ya lami kutokea Mpanda kwenda Kigoma kupitia Vikonge - Luafe mpaka Mishamo na Uvinza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tukiunganishwa kwa kiwango cha lami itakwenda kutufungua sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi tuweze kufanya biashara zetu vizuri. Ukizingatia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatujengea bandari ya kisasa, Bandari ya Karema ambayo imekwenda kutuunganisha sisi na wananchi wa Kongo ambapo tunakwenda kuwa ma-giant katika kufanya biashara, wananchi wa Mkoa wa Katavi. Hivyo, ombi letu ni kuunganishwa na barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara yetu ya kutoka Kibaoni – Sitalike; katika Jimbo la Kavuu tunalima sana mpunga, sote ni mashahidi. Wananchi wa Mkoa wa Katavi wanaotazama nikiwa ninaongea hapa, wanaelewa kwamba katika Jimbo la Kavuu ukienda utakuta watu wa nchi jirani wamekuja kufuata mchele wa Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile bado ni kizungumkuti; hata Mheshimiwa Waziri Mkuu, alivyokuja ametuahidi kwamba fedha zipo na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ile kilometa 51. Tuombe Serikali itusaidie kupitia Wizara ya Ujenzi, barabara hii iweze kukamilika kwani mkandarasi amekuwa akisuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya akina mama wa Mkoa wa Katavi, tunaendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; na nimalizie kwa kuwashukuru sana akina mama wa Mkoa wa Katavi kwa imani kubwa waliyonipa na kunirudisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninaahidi kwamba sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumshukuru pia Mkuu wa Mkoa wangu Mheshimiwa mama Mwanamvua Hoza Mrindoko, kwa kazi kubwa anayoifanya; lakini Mwenyekiti wangu wa UWT Taifa kwa kazi kubwa aliyoifanya, kuhakikisha kwamba tunapata ushindi. Ninashukuru sana. (Makofi)